DK SIAME ASHINIKIZWA KUVUNJA MAKUNDI MBOZI

Na Richard Mwaikenda, Mbozi.

MGOMBEA ubunge Jimbo la Mbozi Magharibi, Dk. Lukas Siame,ametakiwa kuvunja makambi  na kuwaomba radhi wananchi aliowakosea wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kujenga umoja na mshikamano utakaokifanya chama kishinde kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 31,mwaka huu.

Alishinikizwa kufanya hivyo na uongozi wa CCM Wilaya ya Mbozi na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Ridhiwani Kikwete wakati wa mkutano wa ndani wa kuweka mikakati ya kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo uliofanyika juzi mjini hapa.

Ililazimika kumwambia hivyo, baada ya kubaini  kuendelea kuwepo  kwa makundi katika baadhi ya Tarafa  jimboni humo,hali ambayo inaweza kuhatarisha chama hicho kukosa  baadhi kura muhimu zinazohitajika kukipatia chama hicho ushindi wa kimbunga.

Jambo linginne lilowashitua ni kitendo cha mgombea huyo, kutamka wazi katika mkutano huo, kuwa yupo tayari kukosa kura za watu wasiokubali kuvunja makundi na kuungana naye katika kampeni na kwamba ana uhakikia kupata kura kwa watu wengine wanaomkubali.

"Naamini makundi yaliyojitokeza wakati wa kura za maoni tulizimaliza, na endapo kama kuna kundi halikubali kuvunja makundi , basi mimi niko tayari kuzikosa kura zao,lakini tutazipata kwa wengine wanaoniunga mkono,"alisema Dk. Siame..

Akihutubia katika mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Mgombea ubunge jimbo la Mbozi Mashariki kupitia chama hicho, Godfrey Zambi, Mgeni rasmi, Ridhiwani alielezea kuwa si dhambi wakati wa kipindi cha mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni kuibuka makundi, na kudai kwamba  hiyo ni demokrasia ndani ya CCM, lakini makundi hayo yanatakiwa kuvunjwa mara moja anapotangazwa mshindi.

"Si dhambi wakati wa kipindi cha uchaguzi, kuwepo mgawanyiko maana hiyo ndio demokrasia ndani ya CCM,kwani si lazima unayempenda wewe basi kila mtu ampende,lakini utake usitake mwana CCM atakayeshinda katika mchakato huo na ambaye uongozi wa juu utamjadili na  kurudisha jina lake,basi huyo ni wetu wote inatakiwa tumpiganie ashinde," alisema Ridhiwani.

"Kipindi cha kura ya maoni kilishapita, kinachotakiwa sasa ni wanaCCM kuwa na umoja pamoja na mshikamano utakaotuwezesha kukipatia chama chetu ushindi wa kishindo usioelezeka,"alisema Ridhiwani huku akishangiliwa. .

Ridhiwani, alikemea kitendo cha wapambe kuendelea kuwadhihaki wenzao waliokuwa kwenye kambi iliyoshindwa, na kuwataka waache mara moja tabia hiyo kwani haimsaidii mgombea,mwananchi na hata chama chenyewe.

"Wagombea na wapambe acheni kuwadhihaki na kuwakejeli wenzenu walioshindwa, tabia hiyo siyo nzuri, inawafanya wakichukie chama, tusahau yaliyotokea, tujirekebishe tulipokosea, tujenge umoja kwani kidole kimoja hakivunji chawa,"aliwaasa Ridhiwani.

Naye Mgombea ubunge Jimbo la Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, alitamba kuwa kwa jinsi anavyoendesha kampeni zake ni dhahiri CCM jimboni humo itapata ushindi si chini ya asilimia 90,kwa vile katika kampeni amewashirikisha watu bila kujali anatoka kundi gani na kwamba hana kundi bali alilobakia nalo ni kundi moja tu la CCM.

Pia, Mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Mbozi,Jobu Kabinja, alisisitiza kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi kwa kumtaka Dk. Siame asiendelee na tabia ya kuzikataa kura za watu wasiotaka kuvunja makundi, kwa vile kura hizo wanazihitaji.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo,Aloyce Mdaravuma, aliungana na viongozi wenzie, kwa kusema kuwa, wataungana na Dk. Siame kwenye kampeni kwa kuziomba kura kwa unyenyekevu hata kwa kulala chini mpaka kieleweke.

"Tutaingia kiume kwenye kampeni kwa kuzisaka kura katika Kata,vitongoji na nyumba kwa nyumba, hatutaki hata kura moja ipotee, kwani kura siyo zako ni za CCM,"alimazia kusema Mdaravuma.
mwisho

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.