RIDHIWANI AWAPATANISHA MBEGA NA MWAKALEBELA

Na Richard Mwaikenda, Iringa.

MJUMBE wa Kamati ya utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Ridhiwani Kikwete, amewapatanisha Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa mjini, kupitia Chama hicho, Monica Mbega na David Mwakalebela aliyeenguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, baada ya kuongoza katika kura za maoni.

Makada hao ambao makundi yao yamegawawinyiko, waliamua kuyavunja mbele ya Ridhiwani, uongozi wa CCM Iringa na wajumbe wa baraza hilo lililohudhuriwa na vijana wa makundi ya wagombea wote miongoni mwao wakiwmo wa wagombea wengine 10 walioshindwa.Jumla ya wanachama 12 waliwania nafasi hiyo, ambapo Mwakalebela aliongoza.

Ili kudhihirisha kwamba wamepatana, walikubali kupiga picha huku wakiwa wameshikwa mikono na Ridhiwani, kitendo ambacho kiliibua chereko chereko na shangwe katika kikao hicho kilichowashirikisha pia baadhi ya wazee makada wa chama hicho.

Baada ya kupewa fursa ya kuwasalimia wajumbe wa baraza hilo, Mwakalebela, alielezea kuwa baada ya kuenguliwa na NEC, alifuatwa na viongozi wa upinzania wakita ajiunge na vyama vyao, lakini alikataa kwani hakutaka kukigeuka chama chake.

"Nilifuatwa na viongozi wa Vyama vya upinzani kutaka niihame CCM na kujiunga na vyama vyao, lakini nilikataa kukigeuka chama changu, kwani nimekulia ndani ya chama hicho. Nilikuwepo CCM, nipo CCM na nitaendelea kuwa CCM," aliapa Mwakalebela huku akishangiliwa.

Mwakalebela, aliwaomba wote waliokuwa wanamuunga mkono wakati wa mchakato wa kura za maoni,kurudisha nyoyo zao na kuungana kumpigania kwa hali na mali mgombea wao Mbega ili ashinde kwa kura nyingi.

"Vijana ndiyo nguvu kazi, tuko vitani,naomba tuondoe tofauti zetu, tuungane pamoja na kuhakikisha mgombea wetu Mbega, Rais Kikwete na madiwani wanashinda kwa kura nyingi ili CCM ishike tena madaraka ya nchi,"alisema Mwakalebela.

Aliwaasa wanaCCM kutothubutu kuihama CCM, akidai kuwa ina sera nzuri yenye mafanikio kwa jamii, na kwamba wasijaribu kwenda kwenye chama ambacho sera na ilani zake hazifahamiki.

Awali, akihutubia katika baraza hilo, Ridhiwani, aliwataka wanaCCM, kabla ya kuamua kuwania uongozi ndani ya chama hicho, kujua kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuepusha migogoro inayojitokeza baada ya matokeo.

"Kabla ya kuanza kugombea lazima uelewe taratibu za uchaguzi ndani ya chama, na kama hujui basi hupaswi kugombea.Kila mwanachama ana haki ya kugombea lakini tuwe na subira ya mapendekezo kutoka ngazi ya juu,"alisema Ridhiwani.

Ridhiwani, alipongeza kitendo cha Mwakalebela, kukubali matokeo na kuamua kuvunja makundi na kuungana na mgombea Mbega katika kampeni ambapo aliwataka wale wote waliokuwa wakimwamini na kumuunga mkono warudishe nyoyo zao wajenge umoja kwa kushiriki pamoja kwenye kampeni.

"Wana Iringa, kipindi hiki si cha kugawanyika, kwani tunataka tupate ushindi wa kishindo ili tuunde dola tutekeleze ilani yetu kwa maendeleo ya wananchi.Tusahau yaliyopita, tugange yaliyopo na yajayo, lazima tukipiganie chama chetu,"alisema Ridhiwani.

Naye, Mgombea ubunge Jimbo la Iringa mjini, Mbega, alikipongeza kitendo cha Mwakalebela cha kukubali kuvunja makundi na kuungana na yeye kwenye kampeni za kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo.
mwisho

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.