TANZANIA MWENYEJI WA MASHINDANO YA PIKIPIKI YA KIMATAIFA

KWA mara ya kwanza katika historia, Tanzania itaandaa mashindano makubwa ya mbio za pikipiki yatakayojulikana kama Harley-Davidson Kilimanjaro Safari yaliyopangwa kufanyika kuanzia Februari 14 hadi 27 mwakani.



Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Five Stars inayoratibu mashindano hayo, Jean-Marc Chapel alisema Dar es Salaam jana kuwa zaidi ya watalii 70 watashiriki mbio hizo za aina yake.



Hivi karibuni, uzinduzi rasmi wa mashindano hayo ulifanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Ladislaus Komba, na kubainisha Serikali inajiandaa kusaidia mbio hizo, ambazo zitajumuisha pikipiki 43 na magari 10 yatakayosindikiza kutoa msaada.



Chapel alisema mbio hizo ambazo pia zitapita baadhi ya maeneo ya nchi jirani ya Kenya, zinaratibiwa na Kibo Travel Bureau na zitakuwa za kilometa 2,350 na zitafanyika kwa siku 11, wakati kilometa 770 zitapita Kenya.



Chapel alisema mbio hizo zitakuwa na madhumuni makubwa ya kutangaza utalii na vivutio vilivyopo nchini.



Harley-Davidson ni taasisi ya Marekani inayohusika na uandaaji wa mbio za pikipiki kila mwaka tangu mwaka 2004 katika maeneo tofauti duniani na Tanzania imepewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwakani.



Mbio hizo zitaanzia Dar es Salaam na kupitia Chalinze, Korogwe, Lushoto, Marangu, Arusha, Bonde la Ufa la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuvuka mpaka wa Kenya kupitia Namanga na baadaye kurejea nchini kupitia Horohoro, Tanga, Chalinze, Bagamoyo hadi Dar es Salaam.



Alisema mbio hizo pia zitaelekea Zanzibar kupitia kivuko cha Dar es Salaam na kurejea tena. "Mbio zitakutanisha watu mashuhuri na tayari wamejaza nafasi, lakini bado Watanzania wanaweza kujiandikisha kupitia Bodi ya Utalii," alisema Chapel.



Hata hivyo, alisema mipango inafanywa kuandaa vituo maalumu ili kuhakikisha mbio hizo hazitumiki vibaya katika kuchochea maambukizi ya malaria na ya virusi Vya Ukimwi.



Chapel aliwaomba Watanzania kuonesha ukarimu kwa watalii na msaada kila watakapohitaji njiani.



Katika kuhakikisha mashindano hayo yanapata mafanikio, Serikali pia imeunda kamati ambayo inajumuisha wajumbe kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Polisi, Uhamiaji, Idara ya Utalii ndani ya Wizara, Bodi ya Utalii, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mbuga za Wanyama ya Taifa.



Wengine wanaounda kamati hiyo ni kutoka Chama cha Mbio za Magari Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar.



Wadhamini wa mashindano hayo ni Sea Cliff Hotel, Arusha Hotel, Tsavo Inn, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Liberty Tv, Freeway, Atemi, Azam Marine Co. Ltd, Bavaria, Ocean Paradise Resort, Tanga Beach Resort, Tume ya Utalii Zanzibar (ZTC), Lushoto Highland Park Hotel na Lown's Hotel.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.