JK AMPONGEZA NDIMBO KUTEULIWA ASKOFU WA MBINGA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo Jumamosi, Mei 14, 2011, amemtumia salamu za pongezi Padre John Ndimbo kufuatia uteuzi wake wa kuwa Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Mbinga, Mkoani Ruvuma.

Padre Ndimbo ameteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Mbinga na Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Bendicto wa XV1 na uteuzi wake umetangazwa jana, Ijumaa, Mei 13, 2011 na Msemaji wa Kurugenzi ya Mawasiliano, Jimbo la Katoliki, Mbinga, Ndugu Joseph Mwingira.

Katika salamu zake za pongeza Mheshimiwa Rais amesema: “Mhashamu Baba Askofu Mteule, nimefurahi sana kupokea habari za uteuzi wako kuwa Askofu wa Jimbo la Kanisa Katoliki la Mbinga. Kwa hakika, nimepokea habari hizo kwa faraja kubwa sana.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais: “Napenda, kwa dhati ya moyo wangu, kukupongeza sana kwa uteuzi wako. Uteuzi wako ni ishara ya imani kubwa aliyonayo Baba Mtakatifu Benedict wa XVI katika uwezo wako wa kichungaji na ni matokeo ya juhudi na kazi nzuri ambayo umeifanya katika maisha yako ya uchungaji. Nakutakia kila la heri, afya njema na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu ya wadhifa wako mpya. Nakuahidi ushirikiano wangu binafsi na wa Serikali yangu katika kuwatumikia wananchi wetu.”

Rais Kikwete amemweleza Askofu Mteule Ndimbo: “Nina imani kuwa utakuwa kiungo chema na muhimu kati ya Kanisa na Serikali katika jitihada zetu za pamoja kujenga jamii bora zaidi kupitia huduma mbali mbali za kijamii zinazotolewa kwa juhudi za pamoja kati yetu.”

Rais Kikwete pia amemueleza Padre Ndimbo kuwa uteuzi wake umekuja wakati muafaka ambapo jamii na umma wa Tanzania, unaonekana kuhitaji zaidi huduma ya kiroho.

Kabla ya uteuzi wake, Padre Ndimbo ambaye atasimikwa kuwa Askofu Juni 5, mwaka huu, alikuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Askofu Mteule Ndimbo aliyezaliwa Oktoba 12, mwaka 1960, Kipololo, Wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma , ana Shahada ya Hisabati ya Chuo Kikuu cha Consolacion cha Philippines aliyoipata mwaka 1993.

Askofu Mteule pia amepata kuwa mwalimu na mlezi wa Seminari Ndogo ya Likonde, mkoani Ruvuma.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DODOMA.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.