MAMA SALMA ATAKA BAO LIPELEKWE MASHULENI

Mama Salama Kikwete akicheza bao


NA MWANAKOMBO JUMAA
MAELEZO
12/05/2011

Mlezi wa Shirikisho la Mchezo wa Bao Tanzania (SHIMBATA) Mama Salma Kikwete ameshauri mchezo wa jadi wa bao upelekwe mashuleni ili kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi kufikiri katika masomo yao .

Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA amesema hayo leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati alipokabidhiwa bao la mchezo wa jadi na Rais wa Shirikisho la mchezo wa bao nchini Bwana Monday Likwepa. Wakati wa makabidhiano hayo Mlezi huyo wa SHIMBATA amesema mchezo wa bao huwasaidia wanafunzi wengi kuelewa somo la hesabati kwani hutumia akilizaidi wanapocheza mchezo huo.

“Nilipokuwa mdogo nilicheza michezo ya jadi mingi ukiwemo mchezo wa bao, lakini nasikitishwa kuona michezo mingi ya jadi haichezwi na watoto wa siku hizi na kuwa katika hatari ya kutoweka,” amesema.

Mama Salma Kikwete amesema, “baadhi ya watu wanaofikiria kuwa mchezo wa bao ni mchezo wa watu wavivu, ukweli mchezo wa bao sio mchezo wa watu wavivu bali ni mchezo kama michezo mingine na unafaa kuendelezwa.”

Ameeleza kuwa kama mchezo wa bao ungekuwa mchezo wa watu wavivu, Baba wa Taifa hayati Mwl. Julius Nyerere asingekuwa mchezaji na mpenzi mkubwa wa mchezo huo.

Rais wa SHIMBATA Bwana Likwepa ameeleza wakati wa hafla hiyo kuwa, lengo la kumkabidhi bao Mama Salma Kikwete ni kumkumbusha Mke huyo wa Rais, Serikali na jamii kwa ujumla kuwa nchini mwetu kuna michezo ya jadi ambayo inafaa Serikali kuipa kipaumbele kama michezo mingine.

Vilevile Rais Likwepa alikabidhi kitabu cha mchezo wa bao kilichoandikwa kwa lugha ya Kiitaliano pamoja na barua ya mwaliko kutoka Italia kwa SHIMBATA kushiriki shindano la kimataifa hapo baadae.

Mama Salma Kikwete baada ya kupokea kitabu hicho, ameshauri viongozi wa SHIMBATA kutafsili kitabu hicho katika lugha ya Kiswahili ili mchezo wa bao usionekane kwua ni wakitaliano.

MWISHO.




Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI