MTOTO WA OSAMA AELEZA JINSI BABAKE ALIVYOUAWA

BINTI wa Osama Bin Laden ameeleza kwamba baba yake alikamatwa akiwa hai katika makazi yake huko Pakistani, kisha kuuawa kwa kupigwa risasi na makomandoo wa Marekani.Mtandao wa habari wa Uarabuni, Al-Arabiya ulimnukuu mmoja wa maofisa wa usalama wa Pakistani akieleza kwamba binti huyo mwenye umri wa miaka 12, alishuhudia tukio hilo na huku akieleza kwamba baada ya mauaji, mwili wake ulichukuliwa na kupakizwa katika helikopta.

Kwa mujibu wa maelezo ya binti huyo, makomandoo hao wa Kikosi Maalumu cha SEAL hawakupata msukosuko wowote baada ya kuingia na kumasa Osama.

Kwa mujibu wa Shirika la Fox News, taarifa hizo mpya zilizopatikana kwa binti huyo zinaeleza kwamba Bin Laden alikuwa na fedha na namba za simu kwenye nguo zake, wakati alipofikwa na mauti.

Iwapo taarifa hizo zitakuwa za kweli, hiyo ni dalili kwamba kiongozi huyo wa al-Qaeda alikuwa mbioni kuondoka katika makazi hayo iwapo kungetokea uvamizi.Ofisa mmoja wa Pakistani alikanusha taarifa zilizotolewa awali na Marekani kwamba kulikuwa na mapambano makali walipotaka kumkamata Osama, akisema kwamba hakuna hata risasi moja iliyofyatuliwa kwa askari wa Marekani wala kwa helikopta zao.

"Helikopta yao ilipata matatizo ya kiufundi na kuanguka, kisha mabaki yake kuachwa katika eneo la tukio," alisema.Taarifa zilieleza pia kwamba ndugu wa Bin Laden walionusurika wakiwamo watoto wake sita na mmoja wa wake zake, walipelekwa kwenye hospitali ya mjini Rawalpindi.


Bush amtosa Obama sherehe za mauaji ya Osama Bin Laden

Katika hatua nyingine, Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush amesusia mwaliko wa Rais Barak Obama kwenda katika Viwanja vya Ground Zero, jijini New York kusherehekea mauaji ya Osama bin Laden, msemaji wa rais huyo wa zamani wa Marekani, David Sherzer alisema.

“Rais Bush hatahudhuria mwaliko wa Alhamisi (leo), ameheshimu wito, lakini amechagua kutokuhudhuria shughuli hiyo ili aendelee kufaidi matunda ya ustaafu wake. Ataendelea kusherehekea na Wamarekani wenzake ushindi huo muhimu katika mapambano dhidi ya ugaidi,” Sherzer.

Ikulu ya Marekani bado haijathibitisha kama ilitoa mwaliko kwa Bush au hata kuzungumzia uamuzi alioufanya Rais huyo mstaafu.Wiki hii Rais Obama alizungumzia matumaini yake kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yaliyofanyika katika viwanja alivyokuwa akiishi Bin Laden yanaweza kuwa sababu kubwa ya kuliunganisha taifa hilo lililokuwa linakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwamo migogoro ya kifedha.

Wafuasi wengi wa chama cha Republican wamefurahia operesheni hiyo iliyofanywa chini ya utawala wa Obama wa Democrat.

Tangu kuondoka kwake kwenye Ikulu ya Marekani, Bush amekuwa haonekani katika hadhara za watu na pia amekuwa akiepuka kutoa maoni dhidi ya Obama ingawa mwaka jana alijitokeza hadharani akiwa na Rais mwingine mstaafu wa nchi hiyo, Bill Clinton na kusafiri pamoja hadi Haiti baada ya kutokea tetemeko la ardhi wakiwa wajumbe mahsusi wa Obama.

Wakati akiwa madarakani Bush aliutumia muda wake mwingi kumwinda Bin Laden. Siku chache baada ya Septemba 11, alijitokeza hadharani akiwa amesimama juu ya masalia ya majengo yaliyoharibiwa na Bin Laden na kuzungumza na wafanyakazi wa kikosi cha uokoaji.

Jumatatu iliyopita, Ofisa mmoja wa Ikulu ya Marekani alisema kuwa Rais Obama angetembelea eneo maarufu la Lower Manhattan leo ili ambako ndiko kilipokuwa Kituo cha Biashara cha Kimataifa (WTO) kilichoteketezwa na kubakia shimo kubwa maarufu kama Ground Zero ili kukutana na familia zilizopoteza ndugu zao katika tukio la mashambulizi ya Septemba 11, 2001 lililoandaliwa na Bin Laden.

Makazi ya Osama
Majirani katika eneo ambalo Bin Laden alikuwa akiishi, hawakuwahi kubaini kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba ndiye aliyekuwa akiendesha maisha yake katika makazi hayo.

"Nimekuwa nikienda kwenye nyumba yao. Alikuwa na wake wawili, mmoja alikuwa akiongea Kiarabu na mwingine alikuwa akiongea Kiurdu. Walikuwa na watoto watatu, msichana mmoja na wavulana wawili. Walinipa sungura wawili. Waliweka kamera kwenye geti la mbele ili waweze kumuona yeyote kabla hajaingia ndani ya nyumba yao," alisema Zarar Ahmed.

Ilibainika jana kwamba watoto wengine wa eneo hilo walianza kunufaika na mara nyingi walifaidika na uwepo wa kiongozi huyo wa kundi la kigaidi kwenye eneo hilo bila ya kujua... "Iwapo mpira ukianguka ndani ya ukuta wa makazi ya Bin Laden watoto waliokuwa wakiuchezea hawakuruhusiwa kuuchukua tena," muuzaji wa ‘ice cream’ wa eneo hilo, Tanvir Ahmed alisema: "Walikuwa wakipewa fedha badala yake; kati ya rupia100-150 (dola mbilui mpaka tatu) kwa kila mpira."

Kijana mwingine, Daniel Alvi alisema mara nyingi alikuwa akimwona mtu akiingia na gari nyekundu aina ya Suzuki akiwa na mbuzi, huku mtu mwingine aliyekuwa akipeleka maziwa akiishia getini na kupokewa wakati huohuo kabla hata hajapiga kengele.

Kwa mujibu wa wenyeji, magari hayo yalikuwa yakiendelea kusafiri kuelekea katika maeneo ya makabila ambayo wakufunzi wa al-Qaeda walikuwa wakifanya kazi zao.

"Kulikuwa na tetesi kwa majirani kwamba mtu aliyekuwa akiishi pale ni ndugu wa Baitullah Mehsud, alisema Daniel akimaanisha aliyekuwa Mkuu wa Kundi la Taliban, Pakistani ambaye kwa sasa ni marehemu.

"Niliwahi kwenda pale mara mbili nilipopiga mpira ukadondoka ndani ya ukuta lakini sikukuta mtu. Ninakumbuka kulikuwa na zawadi ya dola20 milioni kwa yeyote atakayemwona na kutoa taarifa, lakini sikuwahi kudhani kuwa ni yeye."

Vijana wawili kutoka katika makazi hayo walikuwa wakienda dukani mara mbili kwa wiki kwa ajili ya kununua mahitaji mbalimbali. Ununuzi wao mara nyingi ulihusisha mbogamboga, matunda, mchele, biskuti, jam, asali na ice cream kwa ajili ya watoto.

Muuza duka, Raja Shuja alisema vijana hao walikuwa werevu na muda wote walikuwa wakiuliza maswali kuhusu nini kinachoendelea katika maeneo hayo, pia iwapo kuna mtu mgeni aliyefika kwenye maeneo hayo.

Mmoja wa wauza magazeti alieleza namna alivyofikisha magazeti kwenye makazi hayo kila siku na kila mwisho wa mwezi alilipwa fedha zake kwa usahihi, mara zote akizipokea kwa mtu mmoja.

Makazi hayo ambayo yamepewa namba 25 kwenye mtaa huo hayakuwa na vifaa kama dishi la satelaiti, simu wala viyoyozi.Kwa mujibu wa mwandishi wa CNN, mimea ya bangi imekutwa katika maeneo yanayozunguka makazi yake, suala linaloibua maswali mengi.

Mwandishi huyo, Nic Robertson alisema mimea hiyo imezunguka kama maua ndani ya ukuta mkubwa unaozunguka makazi hayo, pia katika bustani za mbogamboga.Mwandishi huyo alieleza kuhuhudia kwa macho yake mmea huo ukiwa umetapakaa katika maeneo mengi yanayozunguka makazi hayo.

Japokuwa anaeleza kwamba huenda kuna baadhi ya watu walioupanda katika eneo lake, hata askari wa jeshi la Pakistani wamekuwa wakipita katika eneo hilo bila kujali.Katika miaka ya hivi karibuni, Bin Laden aliripotiwa kuwa na matatizo ya figo ambayo ilielezwa kwamba muda mwingine mmea huo hutumika kama kitulizo cha maumivu.



Add comment
Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA