SPIKA MAKINDA AZUIA WATU KUPITA KWENYE BARABARA

Joseph ZablonSPIKA wa Bunge, Anne Makinda anadaiwa kufunga njia inayounganisha eneo la Kijitonyama na Sinza, Dar es Salaam na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji.Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na baadhi ya wakazi wa sehemu hiyo zimeeleza kuwa kutokana na kufungwa kwa njia hiyo, sasa wanalazimika kutumia dakika 45 kufika Sinza kwa miguu badala ya dakika tano hadi 10 walizokuwa wakitumia awali.
Mkazi wa eneo hilo, Juma Mbegu alieleza kuwa njia hiyo imefungwa katika Mtaa wa Sahara, jirani na Kituo Kidogo cha Polisi cha Mabatini: "Njia hiyo imefungwa eti kuruhusu ujenzi wa nyumba yake ya ghorofa moja. Unajua mtu hadi agundue kuwa njia hiyo imefungwa, inambidi atembee kama dakika tano hivi ndipo akutane na uzio wa mabati."
Kwa mujibu wa Mbegu, kibao kilichowekwa mwanzoni mwa Mtaa wa Sahara jirani na Kituo hicho cha polisi kuonyesha kuwa barabara imefungwa, nacho kina utata kwani watu wengi wanajua kuwa imefanyika hivyo kwa magari pekee. Alisema kufungwa kwa njia hiyo inayopita jirani na Kiwanja namba 630 katika Kitalu namba 47, kinachomilikiwa na Makinda, kumesababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo na vitongoji vyake.
Mkazi mwingine ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema kutokana na kufungwa kwa njia hiyo, watu wanalazimika kuzunguka hadi Barabara ya Shekilango eneo la Afrika Sana, ili kufika eneo la Mori, mwendo ambao ni takriban dakika 45.
Kauli ya uongozi wa MtaaMwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kijitonyama, Philip Komanya alipoulizwa jana kuhusu suala hilo alisema hana taarifa ya kufungwa kwa njia hiyo."Sina taarifa na ndiyo kwanza nasikia kwako. Mbona hawajanifahamisha?" alihoji mwenyekiti huyo na kuongeza:"Njia hiyo imekuwa ikitumika pia wakati wa mvua kwani njia inayounganisha ile inayopita katika Kituo Kidogo cha Polisi Mabatini, huwa haipitiki kutokana na ubovu."
Mwenyekiti huyo alisema anachojua ni kuwa Mei mwaka jana, wakazi wa eneo hilo kwa kumtumia Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wao, Athanas Mapunda waliwasilisha maombi ya kutaka kufungwa kwa njia hiyo kwa sababu za kiusalama, ombi ambalo hata hivyo, lilikataliwa.
"Walileta ombi la kutaka hilo lifanyike lakini kikao cha kamati ya maendeleo ya kata kilikataa ombi hilo kwa sababu ni njia pekee katika eneo hilo ambayo inaunganisha maeneo mawili tofauti," alisema.Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, aliwashauri watafute jinsi ya kufanya ikiwa ni pamoja na kuweka lango la kuingilia katika mtaa huo na walinzi.
"Pia nilishauri waweke muda wa kupita kwa watu wote na muda wa kupita wenyeji tu. Niliwaambia waweke geti, walinzi na waaandike muda wa mwisho kupita kwa watu wa kawaida lakini siyo kufunga njia."
Mwenyekiti huyo aliahidi kufika katika eneo la tukio kujionea kinachoendelea akieleza kuwa kisheria, kabla ya kufunga barabara hiyo, mmiliki alipaswa kuwasiliana na ofisi yake.
"Ngoja nifike hapo baadaye nitakupigia. Unajua wakati mwingine kuna watu huwa wanatumia njia za mkato kwenda manispaa kuomba vibali bila kushirikisha mamlaka nyingine halali. Huu ni ukiukwaji wa utaratibu na ni kinyume kabisa na misingi ya utawala bora."
Kauli ya SpikaSpika Makinda alipigiwa simu kutoa ufafanuzi wa madai hayo. Hata hivyo, mara baada ya mwandishi kujitambulisha kwake na kabla ya kumweleza lolote alisema: "Naomba niacheni kwanza. Wasiliana na katibu, tafadhali sana."
Alipodokezwa kuwa suala lenyewe halihusu ofisi yake, bali yeye binafsi tena ni kuhusu kudaiwa kufunga barabara na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo, alikata simu.Baadaye Msaidizi wa Spika, Herman Berege alipiga simu na kukiri kufungwa kwa barabara hiyo akisema hatua hiyo imefikiwa kwa sababu za kiusalama na bosi wake alifuata taratibu zote.
Alisema Makinda alipeleka maombi ya kufanya hivyo katika Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni ambako kwa kuwashirikisha maofisa wa mipango miji na watendaji wengine, walikubali kuifunga njia hiyo. Alipoelezwa kauli ya mwenyekiti wa mtaa kwamba maombi hayo yalipelekwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata lakini yakakataliwa, msaidizi huyo wa Makinda alisema si kweli.
"Tulikwenda na hadidu za rejea za kikao kilichopitisha uamuzi wa kufungwa kwa njia hiyo na makubaliano yalikuwa ama yawekwe matuta, ziwekwe nguzo kuzuia magari au uzio. Barabara hiyo ilikuwa lazima ifungwe kuzuia vitendo vya uhalifu."Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Spika Makinda kutaka aishi nyumbani kwake awapo Dar es Salaam badala ya kukaa hotelini kwa gharama za Serikali.
"Lengo la mheshimiwa ni zuri tu, kunusuru pesa ya Serikali ambayo ingetumika kulipia anapoishi," alisema na kuongeza:"Alikopa kutoka taasisi tofauti ili kujenga nyumba hiyo na kulingana na hadhi yake, watu wa usalama waliona kuna haja ya kuifunga njia hiyo.""Nasisitiza kwamba utaratibu ulifuatwa na kama manispaa hawajaifahamisha serikali ya mtaa, hilo si kosa lake (Spika)."

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*