Cole: Mchezaji bora wa dunia atoke Tanzania

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester United ya England, Andy Cole amezindua programu ya kuendeleza vipaji vya soka kwa watoto chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars na kuwataka Watanzania kuitumia programu hiyo ili siku moja iweze kuitangaza Tanzania.

Mchezaji huyo alisema kuwa pamoja na kuzindua program hiyo, anataka siku moja kuona mchezaji wa Tanzania anakuwa mwanasoka bora wa Dunia.

Program hiyo ilizinduliwa kwa ushirikiano wa klabu ya Manchester na Kampuni ya Simu ya Airtel ambayo itafanyika katika ngazi ya Mikoa na Taifa na kuhitimishwa kwa Kliniki ya Soka itakayofanyika nchini Gabon na Tanzania chini ya Usimamizi wa Jopo la makocha kutoka Manchester United.
Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Makongo, Cole alisema: "Michezo ni sehemu ya maisha, nina imani Tanzania ikiwekeza katika michezo itafika mbali kimataifa na siku moja mchezaji bora wa Dunia atatoka Tanzania.

"Nimekuja Tanzania kwa ajili ya michezo naomba Watanzania watoe sapoti kwa vijana hawa wadogo ambao siku moja wataleta mapinduzi katika Soka la Afrika na hasa Tanzania," alisema Cole.

Mwakilishi wa Klabu ya Manchester United ambaye aliongozana na Cole katika uzinduzi huo, Nick Hamfrey alisema Watanzania wanatakiwa kutumia nafasi hii katika kuendeleza vipaji vya watoto kwani soka inahitaji maarifa na nia ya dhati ndani na nje ya uwanja.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Sam Elangallor alisema program hiyo itatoa fursa kwa vijana hao kuonyesha uwezo wao mbele ya mawakala wa Soka, Makocha sambamba na kupata fursa ya kujiendeleza zaidi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara alisema programu hiyo itaongeza msukumo katika mpango wa maendeleo ya soka nchini kwa sababu vijana wa Tanzania watapata msaada wa kitaalamu kutoka katika timu maarufu duniani.

Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Leodegar Tenga alisema miradi yenye lengo la kuibua vipaji na kuviendeleza ni muhimu kwa maendeleo ya soka hapa nchini na kuwataka Airtel kuwa bega kwa bega na klabu hiyo ya Manchester katika kuendeleza soka la Tanzania.

Andy Cole,39, hivi sasa anafanya kazi katika kituo cha mazoezi cha Manchester United kilichopo huko Callington huku akimalizia kozi yake ya ukocha, lakini kabla ya hapo alikuwa kocha wa washambuliaji katika klabu ya Huddersfield inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini England.
Cole alistaafu soka 2008 baada ya kuzitumikia klabu za Bristol City, Newcastle United, Manchester United, Blackburn Rovers, Fulham, Manchester City, Portsmouth, Birmingham City, Sunderland , Burnley na Nottingham Forest na kufunga mabao 187 katika Ligi Kuu ya England.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*