JK AWAJIBU MAASKOFU

Mwandishi WetuSIKU moja baada ya Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), kumpa Rais Jakaya Kikwete saa 48 kuwataja kwa majina viongozi wa dini wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, Ikulu imewajibu ikitaka wale wanaojishuku wajisalimishe. Pia imesema wapo waliokamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu imesema kauli ya maaskofu hao kwa Rais ni ya kusikitisha na kwamba haikutegemewa kutoka kwa viongozi hao wa dini huku ikisisitiza kwamba wale wanaojishuku wajisalimishe badala ya kusubiri Rais awataje ndipo waanze kuchukua hatua.
"Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa kuuliza kama ni kweli, ni wa rangi gani? Unatakiwa kushtuka na kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumwondosha nyumbani kwako, hata ikibidi umuue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
"Rais ana nia njema sana katika kulielezea jambo hili na mwenye nia njema haumbuki."Taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imesema suala la dawa za kulevya alizozungumzia Rais Kikwete si jambo dogo la maaskofu hao kujitetea kwa kauli nyepesi ya kumpa saa 48 na kwamba wapo ambao wameshakamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, pia wapo wanaochunguzwa.
"Hivi karibuni wapo viongozi wa dini wamekamatwa kwa rushwa, ngono na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kinyume na maadili yasiyotegemewa na jamii kwa ujumla, wapo ambao wameshakamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, wapo wanaochunguzwa, tumeshawashuhudia na bado wataendelea kushuhudiwa," ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu na kuongeza:Ikulu imetaka yeyote anayejishuku kuhusika na biashara ya dawa za kulevya kujisalimisha mwenyewe, huku ikiitaka jamii kumfichua yeyote inayemshuku ili achunguzwe na sheria ichukue mkondo wake.
"Anayejishuku ajisalimishe mwenyewe, anayeshukiwa na jamii afichuliwe ili afanyiwe uchunguzi na hatimaye sheria ichukue mkondo wake lakini msisubiri Rais awataje hadharani ndiyo muanze kuchukua hatua."
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga imesema viongozi wa dini wanategemewa kuweka mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto hiyo ya dawa za kulevya inayozidi kuongezeka na kwamba kazi ya kupambana na dawa za kulevya haimhusu Rais peke yake, bali kila Mtanzania, popote alipo.
"Kazi ya kupambana na dawa za kulevya haimhusu Rais peke yake bali inamhusu kila Mtanzania, popote alipo katika nafasi yake na viongozi wa dini wananafasi kubwa sana kwa sababu wao wanasikilizwa, wanatoa ushauri na wanategemewa kuwa na maelekezo yanayompendeza Mungu," imesema Ikulu.
Imeeleza kuwa viongozi wa dini ni watu wanaotumainiwa katika jamii yeyote, ikizingatiwa kuwa wao siyo malaika ama watakatifu hapa duniani, kwani nao hutumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au hali isiyo tegemewa kabisa.Katika Hotuba yake kwenye hafla ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Mhashamu John Ndimbo kuwa Askofu wa Jimbo la Mbinga, Rais Kikwete alitoa ombi akiwataka viongozi wa dini wajihusishe kikamilifu katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Rais alisema: “Ni tatizo linalozidi kukua pamoja na jitihada za serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Athari zake kwa jamii zinaeleweka hivyo haihitaji kuzirudia.”
“Hata hivyo, niruhusuni niseme tu kwamba tusipofanikiwa kulidhibiti tatizo hili, hasara yake ni kubwa mno. Watoto wetu wengi wataharibika, uhalifu, hasa wa wizi na mauaji utaongezeka.
Taifa litaharibikiwa,” alisema na kuongeza:“Siku hizi kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya. Inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, lakini inasikitisha sana kuona kuwa biashara hiyo sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu.”
“Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana. Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini mnasikilizwa, nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndiyo walengwa wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.” Taarifa hiyo ya Ikulu ilisema kuwa inategemea viongozi wa dini watakuchukua onyo hilo la Rais kama ishara na kuanza kuifanyia kazi.
Polisi: Kauli ya JK ina ukweliMkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa amethibitisha kuwa baadhi ya viongozi wa dini nchini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.Kamanda Nzowa alikuwa akitolea ufafanuzi kauli hiyo ya Rais Kikwete kwamba baadhi ya viongozi wa dini wanajihusisha na biashara ambayo iliibua mjadala mkubwa baada ya baadhi ya maaskofu nchini kumtaka awataje wahusika ndani ya saa 48.
Maaskofu hao wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), walisema wamesikitishwa na kauli hiyo ya Rais Kikwete wakisema kama hatawataja kwa majina wahusika itakuwa ni aibu kwake na taifa.Kamanda Nzowa alisema kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na biashara hiyo akisema kitengo chake kimeanza kuwafuatilia."Wako wengine ambao wamefikishwa mahakamani lakini si rahisi kujua kwa sababu kwenye hati ya mashtaka unataja jina, kabila, umri na dini ili uweze kuapa," alisema na kuongeza:"Rais hawezi kutaja majina kwa sababu inatakiwa ukimtaja mtu umfikishe mahakamani kinyume na hapo mtu huyo anaweza kwenda kukushtaki kukudai fidia kwamba umemdhalilisha.
"Kamanda huyo alisema majina yanayotajwa ni mengi na pia yanahusisha viongozi wa serikali lakini akasema ofisi yake inawafuatilia ili kupata ushahidi."Tunapata information (taarifa) nyingi hata za viongozi wa serikali lakini tunafanya uchunguzi ili tupate ushahidi," alisema.Alisema Tanzania inatumika kama njia ya kupitishia dawa hizo na kiasi kikubwa kinachopitishwa ni heroine kwa sababu ina watumiaji wengi tofauti na cocaine ambayo inauzwa ghali na watumiaji ni wachache.
Hata hivyo, utekelezaji wa sheria kwa watu wanaokamatwa na dawa hizo umekuwa ukilalamikiwa kutokana na watu wengi wanaokutwa na hatia kupewa adhabu ya kulipa faini na kuachiwa huru.Kwa mujibu wa kifungu namba16 (i) a cha Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya, mtu anayepatikana na hatia ya kujihusisha na biashara hiyo, adhabu yake ni kifungo au kulipa fidia ambayo ni mara tatu ya mzigo aliokamatwa nao lakini adhabu nyingi zimekuwa zikitolewa kwa mtuhumiwa kulipa faini ya Sh10 milioni na kuachiwa huru.



Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*