MUUZA DAWA ZA KULEVYA WA KIMATAIFA ANASWA

JESHI la polisi nchini limewakamata watu wanane wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine huku mmoja wa watuhumiwa hao, Mwanaidi Mfundo anayejulikana pia kwa jina la Naima Mohammed Nyakiniwa au Mama Leila aliyetajwa pia na Rais Barack Obama wa Marekani kama mtu hatari kwa biashara hiyo.
Kwa mujibu wa polisi, Leila ambaye ni raia wa Kenya amekatwa nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam akiwa na wenzake saba. Alikutwa na hati sita za kusafiria zikiwa na sura tofauti tofauti.Wiki iliyopita Rais Obama alitangaza watuhumiwa saba wa biashara ya dawa za kulevya waosakwa zaidi ambao wamezuiliwa kuingia Marekani.
Kwa mujibu wa gazeti dada la Mwananchi, Daily Nation la Kenya, Mwanaidi ambaye ni mama wa mabinti watatu, waliokulia eneo la majengo lenye historia ya uhalifu na ufuska, ana makazi mengine katika eneo la matajiri la Kitisuru, jirani na makazi ya matajiri ya Westlands, Nairobi.
Gazeti hilo lilieleza pia kwamba Nyakiniwa alitajwa kuwa miongoni mwa vigogo wa dawa za kulevya wa kimataifa na Rais Obama Jumatano iliyopita kwenye Baraza la Congress. Pia katika orodha hiyo walitajwa Mbunge wa Kilome, John Haroun Mwau, mwenye biashara za aina mbalimbali nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Marekani, Mama Leila anashughulika na biashara ya dawa za kulevya aina mbalimbali ikiwamo heroin ambayo huisafirisha Kusini Magharibi mwa Asia na cocaine anayoisafirisha kwenda Amerika ya Kusini.Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa alisema watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Juni 3, mwaka huu.
Pia Jeshi hilo limetoa orodha ya kiasi cha dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine zilizokamatwa tangu mwaka jana na idadi ya dawa hizo kwa mwaka huu inazidi idadi ya mwaka jana.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Nzowa alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kikosi kazi cha udhibiti wa dawa za kulevya, Juni mosi, mwaka huu saa nane usiku huko Mbezi Beach.
“Walikamatwa wakiwa na kilo tano za cocaine na lita 3 za chloroform. Wote wamefikishwa mahakamani, walikuwa katika harakati za kusafirisha kwa kuwa walikuwa wameshazifunga dawa hizo katika mifuko ya kahawa,” alisema Nzowa.Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Antony Arthur na Ben Machania kutoka Kenya pamoja na Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Haroun, Rajabu Mzome na Aisha Kungwi ambao wote ni Watanzania.
Nzowa alisema Mfundo, maarufu kwa jina la Naima Mohammed Nyakiniwa ni mfanyabiashara wa kimataifa wa dawa za kulevya na kwamba alikuwa akisakwa na nchi mbalimbali duniani.“Inawezekana walikuwa na kilo nyingi za dawa za kulevya ambazo walikuwa wameshazisafirisha, hizi dawa tulizozikamata zinaweza kuwa na thamani ya Sh200 milioni,” alisema Nzowa.Alisema kuwa Mfundo pia alikutwa na hati sita za kusafiria ambazo zilikuwa na jina moja lakini sura tofauti: “Sura zake sita tofauti ambazo zilikuwa katika hati hizo za kusafiria zilimfanya ashindwe kutambulika kirahisi katika nchi alizokuwa akienda,” alisema Nzowa.
Juni 3, watu watuhumiwa hao hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa shtaka la kuingiza nchini kilo tano za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya Sh225 milioni.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu Mustapher Siyani, Wakili wa Serikali, Patrick Malogoi alidai kuwa Juni Mosi, mwaka huu maeneo ya Mbezi Beach washtakiwa hao kwa pamoja kinyume na kifungu cha 16 (1) b (i) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, waliingiza nchini dawa hizo za kulevya.
Baada ya kuwasomea shtaka hilo, Hakimu Siyani aliwataka washtakiwa hao kutojibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shtaka linalowakabili hadi Mahakama Kuu ya Tanzania. Hakimu huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 15, mwaka huu itakapotajwa tena.Kuhusu mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya tangu mwaka jana, polisi imesema wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokamatwa tangu kipindi hicho wote ni raia wa kigeni.
Nzowa alisema mwaka 2010, kilo 190 na gramu 780 za heroine zilikamatwa na washtakiwa walikuwa 496, wasafirishaji 10, watumiaji 480 na wafanyabisahara 12 huku watu sita wakikamatwa, wanne raia wa Iran na wawili wa Afrika Kusini.“Cocaine zilizokamatwa zilikuwa kilo 64 na gramu 966, washitakiwa walikuwa 528, wasafirishaji watatu, watumiaji 521. Waliokamatwa walikuwa watu wanne ambao ni raia wa Liberia, Guinea, Ghana na Msumbiji.”
Alisema bangi zilizokamatwa zilikuwa kilo 22,904 na gramu 905, watuhumiwa walikuwa 9,739, wasafirishaji 400, watumiaji 9,329 na wafanyabishara wakubwa 10 na kwamba ekari 296 za mashamba ya bangi yaliteketezwa huku watuhumiwa wanne wakikamatwa.Alisema mirungi iliyokamatwa ilikuwa kilo 10,317 na gramu 502 na watuhimiwa walikuwa 1,351, wasafirishaji 200, watumiaji 1,146 na wafanyabiashara wakubwa watano.
Alisema mwaka 2011, dawa za kulevya aina ya heroin zilizokamatwa zilikuwa kilo 182 na gramu 402.39 na kwamba watuhumiwa walikuwa 1,080, wasafirishaji watatu, watumiaji 1,075 na wafanyabiashara wakubwa waliokamatwa walikuwa raia wawili wa Pakistani.Alisema Cocaine zilizokamatwa zilikuwa kilo 91 na gramu 906, watuhumiwa walikuwa 1,070, wasafirishaji 15, watumiaji 1,048.
“Wafanyabiashara wakubwa waliokamatwa walikuwa saba, watatu Wakenya, wawili Wanigeria na wengine ni kutoka Pakistani na Afrika Kusini,” alisema Nzowa na kuongeza:“Bangi zilizokamatwa ni kilo 17,257, watuhumiwa 1,000, wasafirishaji 20, watumiaji 970 na wafanyabiashara wakubwa 10. Mirungi iliyokamatwa ni kilo 15, watuhumiwa 40 na watumiaji 40.”
Awali, Nzowa alisema mwaka 2009, kilo 9 za dawa za kulevya aina ya heroine zilikamatwa na kwamba walioshtakiwa walikuwa watu 122, wasafirishaji watano na watumiaji 117.“Cocaine zilikamatwa kilo nne, washtakiwa walikuwa 108, wasafirishaji wawili na watumiaji 106.
Mirungi iliyokamatwa ilikuwa kilo 22,904, watuhumiwa waliokamatwa ni 365, wasafirishaji 20 na watumiaji 345. Bangi zilizokamatwa ni kilo 56,197, watuhumiwa 3382, wasafirishaji waliokamatwa walikuwa 200 ila watano ni raia wa Comoro na watumiaji walikuwa 3,182.”Alisema kuwa ekari 79 ziliteketezwa na watuhumiwa wenye mashamba waliokamatwa walikuwa tisa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.