POULSEN;MWAMUZI KAHONGWA ATUMALIZE

Kocha wa Stars Jan Poulsen

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen alishindwa kujizuia baada
ya kushudia kikosi chake kikipokea kipigo kutoka kwa Jamhuri ya
Afrika Kati pale alipomshutumu mwamuzi wa mchezo huo kuwa alipewa
hongo kuiua Tanzania jijini Bangui.
Poulsen alitoa tuhuma hizo wakati alipokuwa akitoa mtazamo wake
kuhusu mechi yake dhidi ya Afrika Kati ambayo ilishudia Taifa
Stars ikipokea kipigo cha mabao 2-1.
"Nafahamu nimesema maneno hayo makali kwamba mwamuzi alipokea
rushwa na mwizi wa ushindi wa Taifa Stars, lakini ndivyo
alivyokuwa mwamuzi," alisema Poulsen.
"Katika mechi nzima mwamuzi alikuwa akiipinga Stars na
kuwapendelea wenyeji kwa kuwapa faulo nyingi karibu na goli letu."
Poulsen alisema alishangazwa zaidi na mwamuzi alipokataa bao la
pili la Stars ambalo lilifungwa na Athumani Machupa baada
kuunganisha krosi ya Mbwana Samata aliyewapiga chenga mabeki
wawili katika winga ya kulia na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.
Kutokana na maamuzi mabovu ya mwamuzi, Joseph Lamptey kutoka
Ghana, ilifika wakati kocha Poulsen alikuwa akivua koti lake na
kulitupa chini kabla ya kuliokota na kulitupa kwa nguvu kwenye
benchi la wanalokaa wachezaji wa akiba.
Poulsen alikuwa akionekana akipingana na maamuzi ya mchezo mara
nyingi yaliyokuwa yakitolewa na mwamuzi huyo, huku akionyesha
ishara mbalimbali za kuonyesha wachezaji wake walikuwa hawatendewi
haki uwanjani.
Mara baada ya pambano kumalizika mwamuzi wa mchezo na wasaidizi
wake walitolewa uwanjani huku wakiwa wamezungukwa na wanajeshi
wengi hadi kwenye vyumba vyao vya kubadilisha nguo, na kujifungia.
Viongozi wa Stars waliokuwepo kwenye msafara huo wenyewe pia,
walikuwa wakionekana kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi na
walisimama katika mlango wa kutoka kwenye uwanja kuingia kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo na walikuwa wakisikika wakimwambia
mwamuzi hakuchezesha kwa haki, lakini wakati huo mwamuzi alikuwa
akipitishwa na wanajeshi hao kwa haraka.
Akizungumzia kuhusu kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake,
Poulsen alisema anawaonea huruma vijana wake ambao walicheza kwa
kujituma ila hawakutendewa haki na mwamuzi uwanjani.
Alisema: "Kipindi cha kwanza vijana wangu walijitahidi, lakini
Jamhuri ya Afrika Kati walikuwa wakitumia faida ya kucheza
nyumbani na kuleta mashambulizi kwetu , lakini pia uwanja ulikuwa
siyo mzuri kwa upande wetu kwa sababu ya utelezi na sisi
tulijitahidi wasilisogelee goli letu, ila walipata bao moja,
ingawa sisi hatukuwa wazuri katika ushambuliaji katika kipindi
hicho."
Poulsen alisema katika kipindi cha pili ilibidi afanye mabadiliko,
kwa kumtoa John Boko na kumuingiza Mbwana Samata na alimtoa Mwinyi
Kazimoto na kuingia Athumani Machupa ambao walibadilisha mchezo
katika safu ya ushambuliaji.
"Wachezaji hawa walipoingia waliongeza nguvu kubwa katika
ushambuliaji na kuanza kuisumbua ngome ya Jamhuri ya Afrika ya
Kati na Stars ikapata bao la kusawazisha, na baadaye kidogo
Machupa akafunga bao la pili ambalo lilikuwa zuri ambalo
lingeifanya Stars kuwa mbele 2-1, lakini kwa ajabu lilikataliwa na
mwamuzi,"alisema Poulsen.
Kutokana na kupoteza mechi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Afrika Kati,
Poulsen alisema Stars bado ina nafasi ya kufuzu kushiriki Fainali
za Mataifa ya Afrika ingawa inakabiliwa na mechi mbili ngumu dhidi
ya Algeria na nyingine dhidi ya Morocco kuweza kujiweka katika
nafasi nzuri.
Naye Athumani Machupa ambaye alikuwa mfungaji wa bao hilo la pili
la Taifa Stars lililokataliwa alisema anaamini lile ni goli safi
na lilikuwa halina kasoro yoyote kwa sababu kila mtu aliyekuwa
uwanjani aliona na hata mashabiki wao walikaa kimya zaidi, lakini
mwamuzi alilikataa bao lile.
"Mimi nilichokifanya nilikwenda tu kuugusa ule mpira sikumgusa
golikipa wala kumchezea faulo kwa sababu yeye golikipa wakati
anatoka mimi nilikuwa nilishaugusa mpira siku nyingi upo nyavuni
ila kipa wao alichokifanya aliruka na kujiangusha miguuni mwangu
na refa akasema kipa ameguswa kwa hiyo ni faulo," alisema Machupa.
Taifa Stars inatarajiwa kuondoka leo nchini Afrika Kati majira ya
saa saba mchana kupitia Cameroon halafu Kenya kabla ya kutua Dar
es Salaam saa tano na robo usiku.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI