SUALA LA RADA KUJADILIWA UPYA BUNGENI



Kizitto Noya, DodomaBAADA ya kutulia kwa muda, sakata la ununuzi wa rada, limeibuka tena na safari hii kwa sura tofauti, baada ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuazimia kulijadili bungeni katika moja ya vikao vyake vinavyoendelea.
Hoja hiyo jana ilifikishwa bungeni na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye alisoma kauli ya serikali dhidi ya hatua ya Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza kutoa fedha za tozo ya rada kwa asasi za kiraia.
Wakati wabunge wakiwa wamekubaliana kujadili suala hilo, tayari taasisi hiyo ya kutunga sheria imetuma wabunge wanne, wakiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai kwenda nchini Uingereza ili kufuatilia suala hilo.
Wabunge wengine walioambatana na Ndugai katika msafara huo ni Mussa Azzan, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Angella Kairuki, Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo.
Waziri Membe aliwaambia wabunge kuwa serikali inapinga utaratibu huo wa fedha hizo kurudishwa nchini kupitia taasisi za kiraia tena za nchini Uingereza kwa kuwa kufanya hivyo ni kulidhalilisha taifa."Tanzania ni nchi maskini, lakini haiko tayari kudharauliwa kiasi hicho kwa serikali yake, tasisi zake na asasi zake kutoaminiwa. kuruhusu hilo lifanyike ni kuruhusu kuibiwa kwa mara ya pili,"alisema Membe.
Membe alisema kitendo cha BAE kutaka kuzipeleka fedha hizo kwenye asasi za kiraia nchini Uingereza ili zije kufanyia shughuli hapa nchini ni kinyume na makubaliano yaliyofikia kati ya Serikali ya Tanzania, SFO na serikali ya Uingereza.
"Serikali hizi mbili zilikubaliana ni vyema fedha hizo za wananchi zirejeshwe nchini na zitumike kwenye sekta ya elimu. Mpango huo ni moja ya ushahidi muhimu uliotolewa mahakamanai kumshawishi Jaji kutoa uamuzi wa kuridhia makubaliano kati ya SFO na BAE,"alisema Membe
Waziri huyo alifafanua kuwa katika mpango huo, serikali ilidhamiria kutumia fedha hizo kununua vitabu milioni 4.4 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi, vitabu 192,000 vya kufundishia kwa ajili ya walimu wa shule hizo, madawati 200,000 kwa ajli ya wanafunzi 16,000, kujenga nyumba 1,196 za walimu na vyoo 200,000 kwenye shule za msingi nchini
Baada ya taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alisimama na kuomba mwongozo wa spika na kusema," Mheshimiwa Spika, tunaomba taarifa hiyo ya serikali ijadiliwe bungeni." Baada ya kusema hivyo takriban wabunge wote walisisimama kuuuga mkono kitendo kilichomfanya Spika Anne Makinda kusema atatafuta fursa kwa ajili ya kujadili suala hilo bungeni.
Akizungumza na TBC1 kutoka Uingereza jana asubuhi, Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alisema wamefika salama nchini humo na tayari wameanza mazungumzo na viongozi kadhaa wa nchi hiyo wakiwamo mawaziri. "Tumeshakutana na baadhi ya wabunge wa Bunge la Uingereza, naibu spika wa bunge hilo viongozi watendaji wa BAE na waziri wa serikali ya Uingereza," alisema Ndugai na kuendelea
"Mazungumzo yetu yanalenga kuishawishi serikali ya Uingereza kupeleka fedha hiyo kwenye serikali ya Tanzania badala ya kwenye mashirika ya umma kama walivyokusudia hapa awali. Tunaamini mazungumzo yameenda vizuri."Kwa mujibu wa Ndugai, hakuna mantiki kwa Uingereza kupeleka fedha hiyo kwenye mashirika ya Umma wakati iliyoibiwa na serikali ya Tanzania na kufanya hivyo ni kuwanyima haki watanzani walio wengi
"Tunaomba katika hili Watanzania wote tuungane ili fedha hiyo iletwe serikalini na bunge liweze kuipangia matumizi, tuwe pamoja kwani tunataka fedha hiyo iingizwe kwenye sekta ya elimu."Novemba 23 mwaka 2010 kwenye Mahakama ya Westminster, Kampuni ya BAE inayotengeza zana za k ivita ambayo iliilangua Tanzania rada kwa bei ya dola za kimarekani karibu 40 milioni, ilikiri kwamba imefanya kosa la kutoweka kumbukumbu za fedha na mahesabu katika mchakato wa mauzo ya rada kwa serikali ya Tanzania.
Kampuni hiyo iliomba kukaa mezani na Shirika la uchunguzi la Uingereza (SFO), kupata usuluhisho nje ya mahakama. Katika makubaliano hayo na SFO, BAE i lionyesha utayari wa kulipa wananchi wa TAnzania kiasi cha Pauni 30 milioni ikijumuisha gharama za kesi ambazo zingeamuriwa na Mahakama ya mwisho.
Kwa upande wake SFO ilikuwa kusitisha uchunguzi wote dhdi ya BAE na kwamba haitachukua hatua yoyote dhidi ya mtu yoyote kwenye kampuni hiyo iwapo italipa tozo hiyo katika makubaliano ambayo yangepata kwanza baraka za Mahakama Kuu (Crown Court).Lakini, kabla ya kuwasilisha makubaliano hayo mahakamani, SFO, Serikali ya Uingereza na Tanzania zilijadilaina na kukubaliana kuwa ni vyema fedha hizi za wananchi wa Tanzania zikarejeshwa kkupitia kwa serikali ya Tanzania ili zikatumike katia sekta ya elimu.
Baadaye makubaliano hayo yakaridhiwa na Jaji Bean wa Crown Court ambaye aliitaka BAE Systems iilipe Tanzania pauni 29.5 milioni na pauni 500,000 zilipwe kama gharama za uendeshaji wa kesi hiyo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU