ZITTO;SHIBUDA NI MSALITI, HAAMINIKI



KITENDO cha Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda (pichani) kupingana na sera ya chama chake kuhusu suala la posho za vikao (sitting allowance), kimeichefua Chadema ambayo imemuita msaliti ikisema, "adhabu yake ni kufukuzwa.
"Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliliambia Mwananchi mjini Dodoma jana kuwa, alikerwa na kauli iliyotolewa na Shibuda ya kwenda kinyume na msimamo kambi hiyo kupinga posho za vikao kwa wabunge na wafanyakazi wengine wa umma.
Mbowe alisema kwamba kwa kauli yake ya juzi ya kuunga mkono posho ilidhihirisha kwamba mbunge huyo ni msaliti wa kambi hiyo, hivyo sheria zitafuata mkondo wake.
"Kutokana na tukio la jana (juzi) bungeni, Shibuda kutusaliti katika suala la posho za vikao, taratibu za kisheria zitafuata mkondo wake kwani utovu wa nidhamu haukubaliki katika kambi yetu, hata katika chama chetu,"alisema Mbowe na kuongeza:
"Suala la posho si la mtu binafsi, lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi wa 2010 ya chama chetu na kama kuna kiongozi hafahamu hili basi hakustahili kugombea ubunge kwa sababu naamini Ilani ya Uchaguzi, Shibuda anayo."
"Posho zilijadiliwa na kupitishwa katika vikao maalumu vya chama, kwa hiyo kama Katiba yetu ya chama inavyotuongoza, Shibuda alitakiwa kulipinga katika vikao hivyo sio kutoka nje ya kikao na kuanza kupingana na maamuzi yake,"alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Akinukuu kifungu katika Katiba ya chama chake kinachoeleza maadili ya viongozi, Mbowe alisema, "Kiongozi anatakiwa kutii na kutimiza maagizo anayopewa na viongozi wa ngazi ya juu au vikao halali na kama hakubaliani na maagizo hayo aeleze hivyo kwa kupitia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye kanuni."
Kauli ya ZittoKwa upande wake, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, aliliambia gazeti hili jana kuwa mbunge kupingana na sera ya chama chake, ni kutokiamini chama hicho.
"Maana yake hakiamini chama, hivyo hafai kuendelea kuwa mwanachama na mbunge wa chama hicho,"alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Aliendelea, "Hapa kuna mambo mawili; masuala ya kisera na masuala ya utaratibu. Mbunge anayepingana na taratibu adhabu yake ni kumwita na kumpa onyo, lakini mbunge anayepingana na sera, huyo hakiamini chama na dhabu yake ni kufukuzwa."
Kwa mujibu wa Zitto, suala la kupinga posho kwa Chadema ni sera kwa kuwa limo kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
"Hili (suala la posho), lipo kisera. Kwenye Ilani yetu ya uchaguzi tulisema, tutapunguza mishahara ya wabunge na posho zao. Sasa kama mbunge anachaguliwa kwa sera hiyo halafu anaipinga haradhani, huyo hakiamini chama na chama hakipaswi kumwamini."
Aliendelea,"Sasa, adhabu ya juu kabisa ya mbunge asiyekiamini chama, ni kufukuzwa. Huu ni usaliti. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mwenyekiti wa chama ameshalitolea tamko suala hilo halafu mbunge anakuja kumpinga hadharani maana yake nini,?" alihoji.
Tundu Lissu je?Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kitendo cha Shibuda kupingana na sera ya chama chake, "ni uasi usiovumilika".
"Sasa nikiwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni nadhani ninahitaji kukaa naye. Nitamwita anieleze kulikoni. Aseme kulikoni ameamua kukiasi chama na upinzani kwa ujumla?"
Aliendelea, "Lakini kwa bahati mbaya sana, adhabu kubwa inayoweza kutolewa na kambi ya upinzani ni kumtenga na kambi. Lakini kwa mtu kama Shibuda ambaye tayari anaijua adhabu hiyo na kuitafuta kwa makusudi, inaonekana haitamtosha."
"Kwa sababu hiyo basi, kambi ya upinzani itaenda mbali zaidi baada ya kumtenga. Tutakiandikia chama barua kukijulisha usaliti huo wa mbunge wake halafu chenyewe kina taratibu zake za kinidhamu."
Kauli ya ShibudaJuzi alipokuwa akichangia Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2011/2012, Shibuda alitoa mpya pale alipopingana na misimamo wa Chadema kuhusu malipo ya posho kwa wabunge na watumishi wengine wa umma.
Akitumia lugha yake ya mashairi, Shibuda aliliambia Bunge kuwa utata uligubika posho za wabunge na watumishi wengine wa umma, unatokana na tafsiri potofu ya neno hilo ambalo asili yake ni Ujira wa Mwia.
"Ujira wa Mwia (sasa posho) yalikuwa malipo anayopewa mtu kwa kazi anayoifanya ili kumwongezea hamasa ya kuendelea kuifanya kazi hiyo. Kwa bahati mbaya sasa neno hilo linaitwa posho na ndiyo sababu linaleta mjadala bungeni,"alisema Shibuda huko akishangiliwa na wabunge wa CCM.
Kwa mujibu Shibuda, kama maana ya posho ni Ujira wa Mwia kama ilivyokuwa ikitumika na wakoloni, haina sababu kuifuta kwa kuwa ndiyo hamasa kwa wabunge na watumishi wengine wa umma kuendelea kufanya kazi yao.
Shibuda alilitahadharisha Bunge kuwa mjadala wa posho umetokana na Bunge kuwa na aina mbili ya wabunge; wabunge maslahi jamii na wabunge maslahi binafsi.
"Wabunge maslahi binafsi hawashiriki misiba, hawatembelei hospitali wakasaidia dawa, hawaendi kwenye sherehe na hawana msaada wowote kwa jamii. Sasa aina hiyo ya wabunge hatutegemei kwa nini watake posho,"alisema
Aliendelea,"tabia ya choyo ndiyo inayowasumbua wabunge hao. Lakini pia tujue kwamba kuna wabunge wafanyabiashara na wabunge maslahi, mbunge maskini hawezi kuacha kuchukua posho, sasa ni vema tukatambua tofauti hizo ili tumalize mjadala huo."
Shibuda alipendekeza posho ziendelee kutolewa tena kwa haraka zaidi na nyongeza kubwa badala ya kuendelea kuvutana kuhusu uhalali wake nje na ndani ya Bunge.
"Mheshimiwa Spika, posho haitoshi, inafaa kuongezwa hadi Sh500,000. Mimi nasema na kazi ya kutafsiri ninachosema inategemea busara ya mtu, lakini posho ziongezwe ili zisaidie wabunge maskini, shughuli mbalimbali za kijamii."
Wakati Shibuda akiwa anaeleza hayo, Mbowe, alionekana akitikisa kichwa kwenye kiti chake.
Msimamo wakeLakini Shibuda alilimbia gazeti hili jana atashangaa kama atatuhumiwa kwa maoni yake binafsi aliyoyatoa bungeni juzi juu ya kutaka wabunge waendelee kulipwa posho za vikao vya Bunge.
"Nitashangaa kama nitaitwa na kiongozi yoyote wa kambi yetu ya upinzani au Chadema kwa tuhuma za kutoa maoni yangu huru niliyoyatoa bungeni jana (juzi), hata nilipokuwa CCM nilipenda kusahihisha palipokuwa na makosa".
"Sitarajii Chadema kuna viongozi wanaweza kudidimiza demokrasia na uhuru wa kutoa maoni, wakati chama kinafanya maandamano kutoa maoni huru kwa Watanzania. Kama mimi sitakiwi kutoa maoni huru basi hakuna maana ya kuandamana kutoa maoni kwa Watanzania".
"Tusitafute hila na visa kwa maslahi binafsi, tutambue kwamba mbunge anapozungumza bungeni anasema kwa maana pana kwa watu wenye mitazamo tofauti kwa lengo la kuleta fikra endelevu".
Alisema kwamba hana habari kama wabunge wote wa Chadema walikutana na kukubaliana kuikataa posho ya vikao vya Bunge.
Shibuda akifafanua zaidi suala hilo la posho japo kwenye Ilani ya Uchaguzi wa 2010 ya chama chake ilitaka kupunguza posho hizo za vikao pamoja na mshahara wa mbunge, alisema, "Ilani ya Uchaguzi ni mpango kazi wa kuendeleza programu ya chama kilichopo madarakani, kwa hiyo hivi sasa hapa bungeni bila kujali itikadi zetu wabunge tunaunganishwa na programu ya kuendeleza nchi, utawala bora na uongozi wa kuongoza fikra za Watanzania".

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.