Beatrice Mathew 'Nabisha': *Nyota wa Bongo Fleva aliyeibuliwa na kanisa






Na Hamisi Magendela

KADRI siku zinavyosonga ndipo na wasanii wa muziki wa kizazi kipya nao wanavyozidi kuongezeka.

Ambapo ukifuatilia walipotokea watakueleza kuwa awali walikuwa wanaimba kwaya kanisani. Baadhi yao hasa wale wanaofanya vizuri katika tasnia hiyo kimsingi wameandaliwa vizuri ikiwamo kutumia vyombo.

Beatrice Mathew 'Nabisha' mkali kutoka Nyumba ya Vipaji (THT), ni miongini mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao walikuwa waimbaji kanisani kabla ya kujikita katika muziki wa Bongo Fleva.

Anasema alikuwa mwimbaji wa Kwaya ya Mtakatifu Cecilia ya Kanisa Katoliki Parokia ya Kongwa Jimbo la Dodoma.

Nabisha ambaye alijiunga na THT mwaka 2008, anasema alivutika kwenda kwenye nyumba hiyo kwa lengo la kuinua kipaji chake ambacho kilianza kuonekana tangu akiwa mdogo.

Nyota huyo ambaye anavutiwa na Lady Jay Dee 'Komandoo Jide' anasema baada ya kufika THT alipokelewa vizuri na Rebeca Young ambaye alikuwa mmoja kati ya viongozi wa nyumba hiyo na kumpeleka kwenye bendi ya kituo hicho kujaribiwa.

Anafafanua kuwa baada ya kufanyiwa usahili aliweza kufanya vizuri katika majaribio hayo na kujiunga rasmi na hivyo kuanza mazoezi ambayo yalianza kumpa mwangaza wa kufanya vizuri zaidi katika muziki wa kizazi kipya.

Msanii huyo anasema baada ya kukaa katika nyumba hiyo ya vipaji kwa muda wa miaka miwili alianza kupata uwezo wa kutunga nyimbo kadhaa, na kwamba wimbo wake kwanza uliitwa Mapenzi ya Kweli ambao hadi sasa unaendelea kusumbua kwenye vituo mbalimbali vya televisheni na redio.

Anasema baada ya kutoa wimbo huo na kuteka mashabiki, wengi walianza kumpa moyo kuwa anaweza kitu ambacho kilimfanya aongeze juhudi ya kufikiria utunzi wa nyimbo ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja.

Pia anasema wimbo wake huo wa Mapenzi ya Kweli ameuimba kiasili zaidi hali ambayo inamfanya awe tofauti na wasanii wengine wanaoingia katika tasnia hiyo kwa mara ya kwanza.

Nyota huyo chipukizi katika muziki wa Bongo Fleva anaweka bayana kuwa baada ya kuachia kibao hicho na kufanya vizuri alijipanga na kuachia kingine kinachoitwa Kidole Gumba ambacho nacho anasema kuwa kilifanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio na luninga.

" Nashukuru nyimbo zangu kunitambulisha vizuri na wadau kwa kunipokea vizuri na wadau kuanza kunitambua kuwa ni sehemu ya wanamuziki chipukizi wanaosumbua kwenye anga la muziki wa kizazi kipya," anasema Nabisha.

Msanii huyo ambaye amehitimu kidato cha nne mwaka 2004, katika Shule ya Sekondari Kongwa iliyopo mkoani Dodoma, anasema kwa sasa yuko mbioni kuipua albamu yake ya kwanza inayoitwa Dunia Duara.

Amesema ameamua kuipa albamu yake hiyo ijayo dunia duara kutokana na mzunguko wa maisha ulivyo, ambapo kuna changamoto kochokocho (nyingi) ambazo zinahitaji subira, uvumilivu na akili zaidi kuweza kupambana nazo.

Nabisha anasema katika albamu yake hiyo inatarajiwa kuwa na nyimbo nane ambazo kati ya hizo saba tayari zimekamilika ambazo zina mahadhi tofauti ambayo yataweza kukonga nyoyo kwa mashabiki katika nyanja zote.

Pia anasema licha ya kufanya kazi kubwa katika kuandaa albamu inasikitisha kuona wasanii wakiendelea kunyonywa bila sababu za msingi.

" Inasikitisha kuona msanii anatumia gharama kubwa katika kuandaa albamu ya muziki, lakini baada ya kuipeleka sokoni anaambulia kipato kiduchu tofauti na gharama na muda aliyoutumia aviendani kabisa," anasema.

Hivyo, anatoa mwito kwa wasanii kuendelea kutafuta nguvu za kushikamana ili kutatua kero hiyo na kuwataka kuwa na msimamo thabiti wa usimamizi wa uuzwaji wa kazi zao.

" Tukishikamana na kuwa kitu kimoja katika kutafuta haki zetu tutafanikiwa kwa maana mzigo huu si wa msanii mmoja mmoja ni wetu sote. Hivyo jamani wasanii tuungane kusaka haki zetu," anasisitiza nyota huyo.

Pia amewataka wasanii kuwa wabunifu katika kazi zao na si kuendelea kunakili midundo ya muziki wa Afrika Kusini ambayo kimsingi imepitwa na wakati.

Anasema ikiwa wasanii wa Tanzania hawatakuwa makini muziki wa bongo fleva uko hatarini kufutika katika ramani ya muziki kwa maana wengi wanaangalia wasanii wa nje na kuacha tamaduni zao.

" Binafsi nafikilia kuwa tofauti zaidi na wengine ambapo muziki wangu utakuwa wa Kiafrika zaidi ambao naamini utanisaidia kuwa mwanamuziki wa Kimataifa," anabainisha nyota huyo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA