BURIANI REGIA MTEMA WA CHADEMA

MBUNGE wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regia Estelatus  Mtema (32), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha, kupinduka eneo la Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani jana.

Ajali hiyo ilitokea saa 5:30 asubuhi karibu na Sekondari ya Ruvu, wakati mbunge huyo na watu wengine saba, wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Landcruiser wakitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema mbunge huyo alifariki baada ya gari hilo alilokuwa akiendesha mwenyewe, kuacha njia na kupinduka.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya Mtema kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla aliona gari lingine likija kasi mbele yake,  katika kujaribu kulikwepa, ndipo gari hilo lilipinduka.

"Wakati akiwa hajalipita gari hilo aliliona gari lingine likija mbele kwa kasi , katika kulikwepa wasigongane uso kwa uso, alitoa gari lake barabarani na kusababisha kupinduka,’’ alisema Mangu.


Alisema watu wengine saba  waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa, wawili kati yao  hali zao zilikuwa mbaya,  walipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, huku wengine watano, wakiwahishwa Hospitali Teule ya Tumbi Kibaha.

Aliwataja majeruhi waliolazwa Tumbi kuwa ni Lawrence Mtokambali (58), Benadetha Mtema (50), Peter Madesa (50) na Rogers Abdallah(18).

Chadema yatoa tamko
Chadema kilisema kuwa Mtema alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho na Waziri Kivuli wa Kazi na  alikuwa mchapa kazi hodari katika majukumu mbalimbali yakiwepo ya kijamii na kisiasa.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Chadema jana na kusainiwa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika ilieleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibroad Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu, Wakurugenzi wa chama hicho makao makuu na wabunge, wameshtushwa na kifo hicho na kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Chadema kimesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano kati familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kufuatia kifo hicho, mkutano wa Chadema uliokuwa umepangwa kufanyika jana Mjini Kibaha umehirishwa hadi itakapotangazwa wakati mwingine.

Elimu yake
Mtema alizaliwa Aprili 21, 1980. Alisoma elimu ya msingi kati ya mwaka 1989 na 1995. Alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani, Dar es Salaam mwaka 1996 hadi  1999 na kuhitimu kidato cha nne.
Aliendelea kidato cha tano 2002 na sita kati ya mwaka 2000 na 2002 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Machame, mkoani Kilimanjaro.

Mwaka 2003 hadi 2006 alisoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na kupata Shahada ya Maarifa ya nyumbani na Lishe. Baada ya kuhitimu shahada yake, marehemu Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na Chadema na kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya chama hicho.

Baadaye aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya chama hicho, nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum.

JK amtumia rambirambi Mbowe
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufuatia kifo cha mbunge huyo.

Katika salamu hizo, Rais ameelezea kusikitishwa kwake na taarifa za kifo cha mbunge huyo na kueleza kwamba, marehemu Mtema  amepoteza maisha akiwa kijana na kwamba pigo hilo si kwa Chadema pekee bali kwa taifa zima.

“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi habari za kifo cha Mheshimiwa Mtema katika ajali ya gari. Siyo kwamba ajali hii imechukua maisha ya kijana bali imelinyang’anya taifa mbunge hodari, na kwa hakika, kifo chake siyo tu ni pigo kwa chama chako bali ni pigo kwa sote na kwa taifa letu kwa jumla.

"Nakutumia wewe binafsi, chama chako na wanachama wake salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo na msiba huu mkubwa," alisema Rais Kikwete kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

[Gari la Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Regia Mtema alilopata nalo ajali iliyosababisha kifo chake jana, eneo la Ruvu, mkoani Pwani likiwa limeegeshwa katika Kituo cha Polisi cha Mlandinzi, mkoani humo. ]

Gari la Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Regia Mtema alilopata nalo ajali iliyosababisha kifo chake jana, eneo la Ruvu, mkoani Pwani likiwa limeegeshwa katika Kituo cha Polisi cha Mlandinzi, mkoani humo.
Aliongeza: “Napenda ujue kuwa niko nanyi katika msiba huu. Napenda vilevile uniwasilishie salamu zangu za rambirambi za dhati kabisa kwa wana-familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mheshimiwa Mtema.

Taarifa hiyo imemwomba Mbowe kufikisha salamu za Rais Kikwete kwa familia ya mbunge huyo na kuijulisha kuwa amepokea habari hizo kwa huzuni kubwa. "Wajulishe kuwa nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, awajalie uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu kwa sababu yote ni mapenzi yake.

Wananchi wamlilia

Katika kuonyesha kuguswa na kifo hicho mamia ya watu wanaotumia mtandao wa kijamii maarufu kwa jina la ‘Facebook’  walielezea kusikitishwa na kifo hicho huku wakitoa maoni mbalimbali.

Miongoni mwa maelezo yao ni juu ya maneno aliyowahi kuyazungumza mbunge huyo kijana, ukiwamo ujumbe alioandika katika mtandao huo akiwataka wananchi wamweleze kero zao ili azifikishe katika mkutano ujao wa Bunge.

Ujumbe huo aliouandika Januari 10 mwaka huu na kuungwa mkono na watu 159 ulisomeka hivi;

“Wapenzi, habari zenu kama una kero yoyote unayoona inafaa ikasemewe bungeni au nje ya Bunge na Wabunge na Viongozi wa Chadema basi tupia hapa kero yako. Angalizo; isiwe kero binafsi..., karibuni sana pamoja tunaweza”.

Mtema anakuwa mbunge wa pili wa chama hicho kufariki dunia kwa ajali ya gari, Julai 27, 2008 Mbunge mwingine wa chama hicho Jimbo la  Tarime, Chacha Wangwe alikufa katika ajali ya gari

eneo la Pandambili mkoani Dodoma.

Taarifa ya Chadema ilieleza kwamba mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa  nyumbani kwa baba yake, Tabata Dar es Salaam .

Gari la Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Regia Mtema alilopata nalo ajali iliyosababisha kifo chake jana, eneo la Ruvu, mkoani Pwani likiwa limeegeshwa katika Kituo cha Polisi cha Mlandinzi, mkoani humo.    


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA