Hamad Rashid awabana CUF Mahakama Kuu Dar

MBUNGE  wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake 10 sasa wameiomba Mahakama Kuu Dar es Salaam iiamuru Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi(CUF) wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri ya mahakama hiyo.

Ukiacha wadhamini hao, jana Hamad Rashid  na wenzake, waliomba mahakama iamuru pia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad wajieleze kwanini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri hiyo.

Pia wanaiomba mahakama hiyo ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la  chama hicho wa kuwavua uanachama hapo Januari 4, 2012, kwa madai kwamba walikiuka katiba ya CUF.

Kabla ya uamuzi huo wa kuwavua uanachama, Januari 3, 2012, Hamad Rashid na wenzake waliwasilisha ombi  Mahakama Kuu Dar es Salaama chini ya hati ya dharura wakiomba mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho uliokuwa ukitarajiwa kufanyika Zanziba, uzuiwe kuwajadili.
Kupitia kwa mawakili wao, kampuni ya uwakili ya GF Law Chambers Advocates  walidai baraza hilo lina nia ya ama kuwasimamisha au kuwavua uanachama na kwamba uamuzi huo ungeathiri haki zao za kikatiba.

Waliendelea kudai kwamba, kuna kesi ya msingi ya madai namba 1 ya mwaka 2012  waliyoifungua mahakamani hapo wakihoji muundo wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho   na uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo.
Tayari Jaji Augustine Shangwa katika uamuzi wake wa Januari 4, 2012, aliamuru CUF kusitisha uamuzi wa ama kuwasimamisa au kuwavua uanachama walalamikaji hao.

Hamad Rashid jana alirejea amri hiyo ya mahakama kuu chini ya Jaji  na kueleza kwamba  CUF waliikaidi na badala yake kuendelea na kutekeleza azma yake ya kuwavua uanachama.


[Mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF, Hamadi Rashid Mohamed (mwenye kaundasuti) na wenzake wakitoka Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, jana, kuwasilisha kiapo cha mahakama kwa kulalamikia viongozi wa Cuf walikataa oda ya mahakama hiyo iliyozuia kufanyika kwa mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho Januari 4. Kushoto ni Shoka Khamis Juma, mmoja kati ya wanachama wanne wa Cuf walivuliwa uwanachama akiwemo na Hamadi. Picha na Said Powa]

Mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF, Hamadi Rashid Mohamed (mwenye kaundasuti) na wenzake wakitoka Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, jana, kuwasilisha kiapo cha mahakama kwa kulalamikia viongozi wa Cuf walikataa oda ya mahakama hiyo iliyozuia kufanyika kwa mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho Januari 4. Kushoto ni Shoka Khamis Juma, mmoja kati ya wanachama wanne wa Cuf walivuliwa uwanachama akiwemo na Hamadi. Picha na Said Powa
Katika hati ya kiapo cha Hamad iliyowasilishwa mahakamani hapo, alidai  kwamba baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, wakili wake akisaidina na mtumishi wa mahakama aliyemtaja kwa jina la Khatibu, waliwasilisha taarifa ya amri hiyo ya mahakama katika ofisi za chama hicho Buguruni saa 6:20 mchana.

Hata hivyo alidai kuwa Ofisa wa chama hicho aliyejulikana kwa jina la Mikidadi Nyandula alikataa kuipokea.
Alidai kwamba,  baadaye saa 6:50 wakili wake alimtumia uamuzi wa mahakama hiyo kwa njia ya baruapepe na kwamba yeye Hamad Rashid aliiwasilisha nakala ya uamuzi huo wa mahakama kwa Afisa Mkuu wa mlalamikiwa saa 8.15 mchama ili aiwasilishe kwa Katibu Mkuu.

Hamad Rashid alizidi kudai katika hati hiyo kwamba,  baada ya kuwasilisha uamuzi huo alitakiwa kufika mbele ya Baraza Kuu saa 8:25  na kutakiwa kujitetea na kwamba, ombi lake la muda wa kuandaa utetezi lilikataliwa.
Alisema pia  aliwaarifu wajumbe wa baraza hilo kwamba mahakama kuu ilikuwa imetoa uamuzi na amri ya kulizuia kuendelea na azma yake.

“Niliwaonesha wajumbe wa baraza hilo waliokuwepo katika mkutano huo nakala ya uamuzi huo,” alisisitiza Hamad Rashid katika kiapo chake hicho.

Alifafanua kwamba  hata hivyo, baraza hilo lilipuuza amri hiyo ya mahakama na kusisitiza kuwa ni lazima achague ama kujitetea mwenyewe au kutoka nje ya mkutano.

“Niliamua kutoka nje ya mkutano ili nisihusike katika kuidharau mahakama,”alifafanua Hamad  Rashid.
Aliendelea kudai kwamba walalamikaji wengine nao waliitwa mbele ya baraza hilo na kila mmoja aliliambia baraza hilo kuwa hawezi kuendelea kwa kuwa kuna amri ya mahakama, ambayo inazuia kuendele na mkutano huo.

“Hivyo, kila mlalamikaji aliwaonesha wajumbe wa baraza hilo nakala ya uamuzi wa mahakama na  lakini wajumbe wa baraza hilo walipuuza na kusisitiza kuwa ni lazima wajitete na walalamikaji waliamua kutoka nje ya mkutano,” alidai Rashid.
Alidai kwamba siku hiyo hiyo kabla ya uamuzi wa kuwafukuza, wakili wake  aliyemtaja kwa jina moja la Panya mnamo saa 9:05 mchana,  aliwasilisha nakala ya uamuzi huo wa mahakama ofisi ya  makao makuu ya chama hicho Zanzibar.

Aliongeza kuwa licha ya kuwasilisha taarifa hizo kwa wakati katika ofisi za chama hicho na kwa Katibu Mkuu na katika mkutano huo wa baraza kuu, baraza hilo liliendelea na azma yake ambayo hatima yake ilikuwa ni kuwafukuza uanachama wa chama hicho.
“Hatua ya  wa walalamikiwa kuendelea na mkakati wao wa kuwafukuza uanachama walalamikaji ulifanyika saa 9:55 jioni, wakati tayari kulikuwa na amri ya mahakama iliyokuwa imeshawasilishwa kwa walalamikiwa,” alizidi kudai.

Katika hati ya dharura iliyoambatanishwa kwenye maombi yao hayo, walalamikaji hao wanadai kuwa kwa kuzingatia uamuzi huo usio halali, walalamikaji wamewasilisha barua kumfukuza uanachama Rashid kwa Spika wa Bunge kwa ajili ya utekelezaji.
Wanadai kuwa ikiwa Bunge litatekeleza jukumu lake wapiga kura wa jimbo la  Wawi, ambao mbunge wao ni mlalamikaji wa kwanza wanaelekea kunyimwa haki yao ya uwakilishi bungeni.

Mbali na Hamad Rashid wengine waliofukuzwa uanachama CUF ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma na Juma Saanane, wote wakiwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho. (CHANZO CHA HABARI HII KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI)

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA