Kupaza: Sina mpango wa kuhama Twanga

Na Mwandishi Wetu

MWANAMUZIKI nguli wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Saleh Kupaza 'Mwana Tanga' amesema kuwa hana mpango wa kuihama bendi hiyo.

Kupaza ambaye ni Kiongozi Msaidizi wa Twanga Pepeta akimsaidia Luiza Mbutu, amesema kamwe hawezi kurubuniwa akaiacha Twanga Pepeta na kuhamia bendi yoyote nchini.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Kupaza alikanusha uvumi kwamba ana mpango wa kufuata nyayo za mwenzake, Charles Gabriel 'Chaz Baba', aliyetua Mashujaa Musica kwa dau la sh. milioni 10 na gari aina ya Noah.

"Nimekuwa nikisikia uvumi kwamba mimi na wenzangu, Miraji Shakashia 'Shakazulu' na James Kibosho tunatakiwa Mashujaa... lakini hakuhakikishia miongoni mwetu hakuna mwenye mpango huo.

"Nipo Twanga Pepeta kwa ajili ya kulinda heshima ya bendi nikishirikiana na wenzangu... hao wanaosema Twanga itakufa wanajidanganya, tumejipanga vizuri sana," alisema Kupaza ambaye ni mtunzi hodari na mwenye sauti ya kipekee isiyoigika kirahisi.

Mbali ya Kupaza kuhusishwa na mipango ya kudaiwa kusakwa na Mashujaa, pia kuna minong'ono kuwa anawaniwa na bendi ya TOT Plus iliyo chini ya Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, huku kila moja ikimtaka kwa dau kati ya sh. milioni 15 na sh. milioni 20.

Hata hivyo, Kupaza alisema yeye bado ana mkataba aliosaini wa miaka mitatu na Twanga Pepeta, na kwamba anauheshimu, na hata isingekuwa hivyo, hana fikra za kuhama, kwa vile anatambua umuhimu wake katika bendi hiyo inayotambulika kama 'Kisima cha Burudani'.

Kupaza alisema kwa kushirikiana na wenzake kama Mwinjuma Muumin, Hamis Kayumbu 'Amigolas', Luiza Mbutu, Ramadhan Athuman 'Dogo Rama', Venance Mgori, Jumanne Said, Haji Ramadhan (mshindi wa BSS 2011), Janeth Isinika, Khadija Mnoga 'Kimobitel', Grayson Semsekwa, Msafiri Said 'Diouf' na wengine, wataendelea kuipeperusha vyema bendera ya Twanga.

Alisema pia wakiwepo wapiga vyombo, Shakazulu, Jojoo Jumanne, Godfrey Kanuti, Selemani Shaibu, Victor Nkambi, Hassan Kado, MCD, wanenguaji Asha Said 'Sharapova', Maria Soloma, Betty Johnson 'Baby Tall', Mary Khamis na wengineo, wataendelea kutamba.

Twanga Pepeta hivi sasa inatamba na albamu yake ya 11 ya Dunia Daraja yenye nyimbo za Kauli, Kiapo cha Mapenzi, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Dunia Daraja na Penzi la Shemeji.

Albamu zilizopita za bendi hiyo ni Kisa cha Mpemba (1999), Jirani (2000), Fainali Uzeeni (2001), Chuki Binafsi (2002), Ukubwa Jiwe (2003), Mtu Pesa (2004), Safari 2005 (2005), Password (2006), Mtaa wa Kwanza (2007) na Mwana Dar es Salaam (2009).

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA