Kwa upotoshaji huu, Ismail Jussa aombe radhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka

LEO gazeti la Mwananchi tumechapisha habari zinazomnukuu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akishangazwa na kauli iliyotolewa katika Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa Mji Mkongwe kwa tiketi ya CUF, Ismail Jussa kwamba andiko lililowakilishwa katika Umoja wa Mataifa (UN) na waziri huyo kuomba eneo la ziada nje ya maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi Baharini (EEZ) halikufanywa kwa niaba ya Serikali ya Muungano kwa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) haikushirikishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri Tibaijuka alisema andiko hilo liliwasilishwa Januari 18 mwaka huu kama ombi la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kuongeza kuwa, SMZ ilishirikishwa kikamilifu tangu mchakato wa kuandaa mradi huo ulipoanza mwaka 2007.

Waziri alitoa kauli hiyo baada ya mwakilishi huyo kuwasilisha hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi mwanzoni mwa wiki, akilitaka Baraza kutolitambua andiko hilo lililowasilishwa UN na kuliomba liiagize SMZ kutojihusisha na mpango huo kwa namna yoyote kwa madai kwamba ni mpango wa kuhujumu eneo la bahari la Zanzibar. Mwakilishi huyo alikwenda mbele zaidi na kumtaka Waziri wa Ardhi, Ali Juma Shamhuna ajiuzulu, vinginevyo awajibishwe na Rais, huku akiungwa mkono na wajumbe waliosimama kuchangia hoja hiyo.

Tunampongeza Waziri Tibaijuka kwa uamuzi wake wa kukutana na waandishi wa habari jana na kuchukua muda mrefu kutoa ufafanuzi wa suala hilo ambalo tunadhani lingeweza kusababisha msuguano usiokuwa wa lazima kati ya pande mbili hizi za Muungano wetu. Tunasema hivyo kwa sababu tuhuma alizotoa mwakilishi huyo ni nzito mno pengine kuliko yeye anavyofahamu. Ndiyo maana tuhuma kama hizo zinapotolewa, serikali makini popote duniani hulazimika kuzijibu kwa ufasaha pasipo kuzibeza au kutoa majibu ya mkato kwa nia ya kuzificha chini ya zulia.

Hivyo ndivyo Waziri Tibaijuka alivyofanya na tunakubaliana naye kabisa aliposema alilazimika kutoa ufafanuzi wa kina kwa sababu pande hizo mbili za Muungano hazipaswi kugombea fito wakati nyumba inayojengwa ni ya wote. Moja ya sababu zinazotufanya turidhishwe na ufafanuzi wake ni pale alipotoa ushahidi wa namna Zanzibar ilivyohusishwa kikamilifu kupitia SMZ katika ngazi zote tangu 2007, kiasi cha kuibua mashaka kama kweli mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe alipeleka hoja hiyo barazani kwa nia njema au alidhamiria kuwachafua viongozi wa pande hizo mbili za Muungano kwa kupeleka hoja iliyojengwa kwa misingi ya maneno ya mitaani?

Ufafanuzi wa Waziri Tibaijuka umetufumbua macho na sasa tumeelewa kwamba mchakato huo mkubwa na muhimu uliendeshwa na kamati mbalimbali zilizoundwa tangu mwaka 2007, ikiwamo kamati ya makatibu wakuu iliyoongozwa na Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji, Nishati, Ujenzi na Makazi Zanzibar, Mwalimu Mwalimu na kwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji Ramani, Haji Adam Haji ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi. Sasa tumejua pia kwamba Pandu Makame kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Rais ndiye aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Utekelezaji.

Tumefarijika kusikia kutoka kwa waziri huyo kuwa, zoezi la kupima alama za sehemu ya bahari inayoombwa lililofanyika Januari mwaka jana, masheha wa Kiuyu, Maziwa Ng’ombe, Kojani na Vitongoji walioko katika Kisiwa cha Pemba walishirikishwa, huku wenzao wa Makunduchi katika kisiwa cha Unguja pia wakishirikishwa. Hata wakati wa kuwakilisha andiko hilo huko UN ujumbe wa nchi yetu uliwahusisha viongozi wa pande mbili za Muungano, akiwamo Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Ayoub Mohamed Mahamoud.

Sisi wa Mwananchi tunajivunia rekodi yetu ya muda mrefu ya kutetea haki za wananchi wa Zanzibar pale tunapoona zinakiukwa. Lakini tumefadhaishwa na tuhuma hizo zilizotolewa dhidi ya SMZ na Serikali ya Muungano na mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe. Tunamshauri apate ujasiri na kuomba radhi kwa Baraza la Wawakilishi, SMZ na Serikali ya Muungano kwa upotoshaji mkubwa alioufanya. Chanzo,Mwananchi

Comments

Anonymous said…
Ndugu watanzania wenye nia njema na nchi nawasalimu kwa Jina la Mwenyezi Mungu. Napenda kutoa wazo kuhusu kauli na mwenendo mzima wa huyu binadamu mwenzetu Mh Jussa. Nashindwa kukiri kutamka kwamba ndg Jussa ni Mtanzania mwenzetu maana sijawahi kutana na Mtanzania mwenye ujasiri wa kauli kama za huyu bwana. Kauli zilizojaa husuda,unafiki,fitina,ushamba wa kuelewa mambo ya Kitaifa na kukosa uzalendo wa nchi ya aliyozaliwa. Kauli zake zimejaa kejeli na wivu mwingi kwa viongozi wake na serikali zetu tukufu. Nimekuwa namfuatilia huyu jamaa kila ajengapo hoja mwishowe analenga kuharibu kila mfumo ulioko mahali pake bila kuitoa wazo mbadala namna ya kuboresha mifumo au mipango husika. Amejaa hila na wivu tena usio na heshima hata utu wa Mtanzania amabo ni adimu sana hapa duniani.

Mie wazo langu ni: WATANZANIA tuchukue uamuzi wa kupuuza fikara hizi hatari za bwana Jussa lakini pia tuelimishane maana kuna baadhi yetu wanaweza wasijue hujuma za huyu mwivu wa maendeleo ya Tanzania.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Zanzibar

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA