LEO KAZI YANGA VS KIKWAJUNI MAPINDUZI CUP

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abed Karume akipiga kiki ya penalti kama ishara ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amani muda kabla ya kuanza mechi kati ya Yanga na Mafunzo.

Doris Maliyaga, Zanzibar
BAADA ya kujeruhiwa na kipigo cha bao 1-0 toka Mafunzo ya Zanzibar katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi mjini hapa, Mabingwa wa Bara, Yanga leo wanashuka dimbani kwa lengo la 'kutibu' kipigo hicho pale itakaposaka pointi tatu dhidi ya Kikwajuni kwenye Uwanja wa Aman.

Azam FC baada ya mwanzo mzuri katika michuano hiyo inayoshirikisha timu za Bara na Visiwani, nao leo wanashuka dimbani kujaribu kukoleza kasi yao ya ushindi mnono watakapocheza na Mafunzo ya mjini hapa.
Katika mechi za leo, Azam itaanza na Mafunzo saa 10 jioni na kisha saa mbili usiku itakuwa zamu ya Yanga dhidi ya Kikwajuni.

Mechi ya Yanga ni muhimu kushinda ili kufufua matumaini yao na kwani kinyume chake itakuwa imejiweka kwenye wakati mgumu wa kusonga mbele.Yanga ilitua Zanzibar juzi ikiwa na chipukizi wengi na mastaa tisa tu, kabla ya baadaye kuwasili kwa ndege kwa nyota Jerry Tegete na Omega Seme sambamba na kocha wao, Kostadin Papic.

Papic alisema juzi mara baada ya kufungwa na Mafunzo kuwa, kikosi chake kilicheza vibaya na kupoteza mchezo huo kwa vile hakikuwa na maandalizi mazuri kulinganisha na wapinzani wao.Hata hivyo Papic, amesema mechi ya leo ni muhimu kwao na wachezaji wanafahamu wanapaswa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri.

"Ni lazima tushinde leo kabla ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Azam," alisema Papic. Azam iliifunga Yanga mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi wiki moja iliyopita.
Papic alisema: "Tumefanya marekebisho sehemu ya ushambuliaji na beki. Maeneo haya ndiyo tatizo kubwa kwetu kwa sasa."

"Leo tutacheza mchezo wa kushambulia, nafanya mpango wa kuongeza washambuliaji wengine (Hamis Kiiza au Pius Kisambale) mmoja wao anapaswa kuja kuongeza nguvu," alisema zaidi.''

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Masoud Hattai alisema hakuna timu inayokatazwa kuongeza wachezaji ila ni lazima wawe wale waliosajiliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa timu za vijana na wakubwa.
Kwa upande wao Kikwajuni, watalazimika kushinda mechi ya leo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele hasa ukizingatia kuwa walipoteza mechi ya kwanza mbele ya Azam.

Katika mechi nyingine, Azam itakuwa ikisaka ushindi wa pili na kama hilo litatimia, basi watajihakikishia nafasi ya kusonga mbele.

Mechi hiyo inatarajia kuwa na upinzani mkali kutokana na Mafunzo kuonyesha kandanda safi siku walipocheza na Yanga.

Kocha wa Azam, Stewart Hall amesema kuwa: "Mechi itakuwa ngumu, lakini nina imani na kikosi changu, kitafanya vizuri."

Mchuano hiyo itaendelea tena kesho kwa mechi kati ya Jamhuri na KMKM itakayoanza saa 10:00 jioni na kisha Simba dhidi ya Miembeni itakayochezwa ushiku.

Wakati huo huo, Miembeni United, jana iliichapa KMKM bao 1-0 katika mechi iliyochezwa jioni kwenye Uwanja wa Aman. Bao la United lilifungwa dakika ya 36 na mchezaji Iss Othman.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA