IGP, MWANASHERIA MKUU WAPEWA SIKU 7 NA MAHAKAMA

MAHAKAMA Kuu imewapa siku saba Mkuu wa Polisi nchini (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ,kuwasilisha majibu ya madai yaliyofunguliwa mahakamani hapo kuhusiana na kukamatwa kwa mwanasiasa maarufu wa Burundi, Lexis Sinduhije.Mhakama hiyo ilitoa muda huo baada ya wakili wa wadaiwa hao, Wakili Mkuu wa Serikali, Obadia Kameya akisaidiana na wakili Edwin Kakolaki kudai kuwa walichelewa kupata hati ya kuitwa mahakamani kwa wadaiwa hao.

Juzi, Jaji Lawrence Kaduri alitoa amri ya IGP na AG kufika mahakamani ili kujieleza kutokana na kumkamata na kumshikilia kwa siku 14 Sinduhije, ambnaye ni Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Burundi cha Movement for Solidarity and Development.Jaji Kaduri alitoa amri hiyo kufuatia maombi yaliyowasilishwa na wakili wa Sinduhije, Hubert Nyange.

Katika maombi hayo namba 7 ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa chini ya hati ya kiapo cha dharura, Nyange anadai kuwa kitendo cha Sinduhije kukamatwa na kushikiliwa ni kinyume cha utawala wa sheria na ukiukaji wa haki za binadamu.Lakini, jana Wakili Kameya kwa niaba ya wadaiwa aliomba mahakama kuwapa muda wa kujibu madai hayo kwa sababu walichelewa kupata hati ya wito wa kufika mahakamani, hivyo hawakuweza kuandaa hati ya kiapo kinzani (counter affidavit).

“Mheshimiwa jaji, tulipata hati ya wito wa kufika mahakamani jana mchana, hivyo hatukuweza kuandaa hati ya kiapo kinzani. Kwa hiyo tunaomba muda wa siku saba ili tuweze kuwasilisha hati hiyo ya kiapo kinzani,” aliomba wakili Kameya.Jaji Kaduri alikubaliana na ombi hilo baada ya Wakili Nyange kudai kuwa hana pingamizi na maombi hayo ya wadaiwa.

Hivyo, Jaji Kaduri aliamuru wadaiwa hao wawasilishe mahakamani hati hiyo ya kiapo kinzani Januari 31 na kuutaka upande wa muombaji kuwasilisha majibu ya hati ya kiapo kinzani hiyo (rejoinder) na kwamba, maombi hayo yatasikilizwa Februari 6, mwaka huu.Hata hivyo, Sinduhije alisafirishwa juzi asubuhi kwenda Kampala, Uganda kwa Shirika la Ndege la Precision.

Wakati Sinduhije akisafirishwa kwenda Kampala wakili wake, Nyange alidai kuwa hakuwa na taarifa hadi alipopigiwa simu na mtu mwingine, kabla ya yeye mwenyewe kumpigia simu Mkuu wa Kitengo cha Interpool, Gustav Babile, ambaye alimthibitishia.

Polisi walimrejesha Sinduhije Kampala kwa kuwa wakati akiingia nchini hati yake ya kusafiria ilionyesha kuwa ametokea huko, lakini kabla ya kuigia Kampala alikuwa ametokea Ufaransa ambako amekuwa akiishi kwa muda tangu kumalizika uchaguzi mkuu Burundi mwishoni mwaka 2010.Sinduhije alikamatwa Januari 11, mwaka huu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu mbalimbali nchini Burundi.

Januari 13, mwaka huu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini hakuweza kusomewa mashtaka na badala yake alirudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi ambako alikuwa akishikiliwa bila kupelekwa mahakamani hadi jana. HABARI KWA HISANI YA GAETI LA MWANANCHI

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA