MJUE KIZZA BESIGYE WA UGANDA

Kizza Besigye alikuwa daktari binafsi wa Rais Yoweri Museveni. Lakini sasa Bw Besigye anamuita kiongozi huyo wa Uganda "dikteta".

Kizza

Kizza Besigye

Bw Besigye analalamika kuwa wafuasi wake wananyanyaswa na kuambiwa hawatapatiwa misaada na serikali, ingawa hakukamatwa wakati wa uchaguzi, na aliweza kufanya kampeni zake.

Baada ya kurejea Uganda, kabla ya uchaguzi wa mwaka 2006, alikamatwa na kushitakiwa kwa uhaini na ubakaji.

Dokta Besigye, 54, ana mke na mtoto mmoja wa kiume.

Alizaliwa katika wilaya ya magharibi ya Rukingiri, akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto sita. Baba yao alikuwa ni polisi.

Besigye

Besigye

Wazazi wake wote walifariki wakati akisome shule ya sekondari.

Mwaka 1975, alikwenda jijini Kampala na kusomea udaktari, katika kilichokuwa chuo maarufu katika eneo hilo, chuo kikuu cha Makerere.

Idi Amin, alikuwa rais wa Uganda katika kipindi hicho, na wanajeshi wake walisababisha hali ya wasiwasi na mashaka katika maeneo mengi ya nchi ikiwa ni pamoja na chuo kikuu.

Kumzaba kibao

Bw Besigye, hakukimbia hali hiyo. Siku moja, akiwa na miaka 18, mjini Kampala katika hoteli moja kupata chakula cha jioni, alipoinuka kwenda chooni, alisimama kuzungumza na mwanafunzi mwenzake.

Ghafla, mtu mmoja wa miraba mitatu alimyanyua na kumzaba kibao usoni kilichompeleka sakafuni.

Anasema safari yake ya chooni iliishia hapo, hakwenda kula tena. Aliinuka na kukimbia kuokoa maisha yake.

Kufuatia kuondolewa madarakani kwa Idi Amin, Dk Besigye, alikuwa mmoja wa wanachama wa Vuguvugu lililoongozwa na Yoweri Museveni.

Msituni

Vuguvugu hilo halikuwa na mafanikio makubwa katika uchaguzi wa mwaka 1980, ambao ulishuhudia kurejea madarakani kwa Milton Obote - uchaguzi ambao unadhaniwa ulitawaliwa na wizi wa kura.

Dk Besigye aliliambia gazeti la East African kuwa hakujiunga mara moja na Museveni alipoingia msituni.

Lakini alikamatwa na kushhikiliwa kwa miezi miwili katika hoteli ya Nile mwaka 1981, akituhumiwa kushirikiana na waasi, na hivyo kuteswa.

Dk Besigye alikimbilia Nairobi na mwaka 1982 alijiunga na Bw Museveni msituni na kuwa daktari wake binafsi.

Vita

Ingawa aghalabu akishiriki katika vita mstari wa mbele, Dk Besigye alikuwa akipelekwa katika vikosi vilivyokuwa vikipambana, ambapo aliwatibu majeruhi.

Wakati Bw Museveni alipoingia madarakani, Dk Besigye, akiwa na umri wa miaka 29, aliteuliwa kuwa waziri wa nchi wa masuala ya ndani na pia kamisaa wa taifa wa siasa.

Uteuzi huu uliwashitusha baadhi ya watu waliokuwa pamoja na Dk Besigye msituni, kwa sababu hakuwa amehusishwa katika masuala ya kisiasa wakati wa vita.

Baadhi wanaamini kupanda haraka kwa Dk Besigye kulionekana kama tishio kwa rais na matokeo yake alipewa majukumu madogo katika miaka ya 1990.

Mgombea urais

Dk Besigye alipanda na kufikia cheo cha kanali jeshini, lakini hakustaafu kazi ya jeshi hadi muda mfupi kabla ya uchaguzi wa 2001 - ambapo alikuwa ameandika taarifa inayotuhumu chama kinachotawala cha National Resistance Movement, kwa ukosefu wa demokrasia, ufisadi na kutokuwa na uwazi.

Miezi michache kabla ya uchaguzi, alijitokeza kama mgombea urais.

Baada ya kushindwa uchaguzi aliopambana na Bw Museveni, alikwenda mahakamani kupinga matokeo kwa misingi kuwa serikali ilitumia nguvu, vitisho na ghasia.

Kesi yake ilitupiliwa mbali na yeye kukimbia nchi.

Uasi

Aliporejea mwaka 2005 alisema: "Niliondoka ili kuendelea kuwa hai kisiasa, badala ya kuwa kifungoni au kaburini kama nilivyotishiwa."

Serikali inasema Dk Besigye anahusiana na kundi la waasi, na tuhuma hizo ndio zilisababisha mashitaka.

Alikanusha kuhusika na kundi lolote la uasi, ingawa alisema hatosita kuingia msituni ili kuingoa serikali, iwapo katiba itapuuzwa na itahitaji kutumika tena.

Wakosoaji wake wanasema ana kiu ya madaraka, lakini wengine wanamsifu kwa kuwa thabiti na msimamo wake.

Dk Besigye mwenyewe anasema lengo lake ni "kushirikiana na mamilioni ya wananchi wa Uganda kuleta demokrasia na Uganda yenye amani".

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA