Nani ni nani wa Kenya mbele ya ICC


Kwa mara ya kwanza washukiwa wakuu sita wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya wanafika mbele ya mahakama ya uhalifu wa kivita, ICC, iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, siku ya Alhamisi na Ijumaa. Wote wameshakanusha mashtaka hayo. Washukiwa hawa ni kina nani ?

UHURU KENYATTA

Uhuru

Uhuru Kenyatta

Ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

Kwa sasa ni Naibu waziri mkuu na pia Waziri wa Fedha.

Bw Kenyatta alizaliwa mwaka 1961. Aligombea kiti cha urais mwaka 2002 kwa tikiti ya chama cha KANU lakini akashindwa na Rais Mwai Kibaki baada ya vyama vya upinzani Kenya kuunga mkono mgombea mmoja.

Mahakama ya ICC inadai kwamba Uhuru alifadhili vijana wa kundi lililopigwa marufuku la Mungiki kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi, baada ya ghasia mkoani Rift Valley zilizowalenga wafuasi wa chama cha PNU.

WILLIAM RUTO

Ruto

William Ruto

Alisimamishwa wadhifa wa waziri wa elimu ya juu ili uchunguzi ufanyike kuhusu madai ya kuhusika na rushwa katika masuala ya ardhi.

Kwa sasa yeye bado ni mmoja wa manaibu viongozi wa chama cha Orange Democratic Party kinachoongozwa na Raila Odinga.

Mahakama ya ICC inadai Bw Ruto ndiye aliyepanga vitendo vya uhalifu dhidi ya wafuasi wa chama cha PNU mkoani Rift Valley. Ruto alizaliwa mwaka wa 1966 mkoani Rift Valley.

Baada ya Daniel Arap Moi kustaafu, Bw Ruto anaonekana ndiye aliyechukua uongozi wa jamii ya Kalenjin.

Ushirikiano baina yake na Bw Odinga ulivunjika baada ya serikali ya umoja wa kitaifa kuundwa.

Ingawa bado ni mmoja wa viongozi wa chama cha ODM, inatarajiwa ataunda chama kingine ili kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2012.

Kwa sasa anashirikiana na Uhuru Kenyatta katika kutafuta uungwaji mkono, ingawa Kenyatta naye ananuia kugombea urais.

Ruto alikuwa miongoni mwa wale waliopinga kuanzishwa kwa mahakama maalum nchini Kenya ya kuwashtaki washukiwa wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi wakitaka kesi zipelekwe ICC, jambo ambalo sasa analipinga.

Aliwahi kusafiri kwenda The Hague katika juhudi za kutaka kujisafisha.

FRANCIS MUTHAURA

Muthaura

Francis Muthaura


Bwana Muthaura ni mkuu wa utumishi wa umma na katibu wa Baraza la Mawaziri nchini Kenya.

Alizaliwa mwaka 1946 katika wilaya ya Meru mkoani mashariki.

Yeye ni mmoja wa washirika na washauri wa karibu sana wa Rais Kibaki.

Alikuwa katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kutumika kama balozi wa Kenya katika nchi mbali mbali kwenye serikali ya Daniel Arap Moi.

Muthaura alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kutoa Ushauri kuhusu Usalama wakati wa ghasia za nchini Kenya.

Kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC Luis Moreno Ocampo amekuwa akielezea wasi wasi wake kwamba kwa Bw Muthaura kuendelea kushikilia wadhifa huo kunaweza kuhitilafiana na uchunguzi wa washukiwa.

Lakini serikali ilisema mapema mwezi huu kwamba Muthaura bado ni mwenyekiti wa kamati hiyo lakini kwa sasa hahudhurii mikutano.

ICC inasema Muthaura aliagiza Polisi kutumia nguvu za kupindukia dhidi ya wafuasi wa ODM na kuwalinda makundi ya vijana wafuasi wa chama cha PNU.

HUSSEIN ALI

Ali

Hussein Ali


Bw Ali alikuwa mkuu wa jeshi la Polisi nchini Kenya wakati wa ghasia , na sasa ni mkuu wa shirika la Posta.

Ali ni kutoka jamii ya Wasomali, na alizaliwa mwaka 1956 katika mji wa Eldoret mkoani Rift Valley.

Ali alikuwa anatumikia Jeshi la Wanahewa la Kenya kabla ya Rais Kibaki kumteuwa kuwa mkuu wa Polisi mwaka wa 2004, wakati ambapo kulikuwa na matukio mengi ya ghasia na uhalifu mjini Nairobi na kote nchini Kenya.

Anakumbukwa kwa kukabiliana vilivyo na kundi lililopigwa marufuku la Mungiki.

Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi, Polisi walishtumiwa kwa kutumia nguvu za kupindukia.

Uchunguzi wa mashirika ya kutetea haki ulionyesha vifo vingi vya raia vilitokana na majeraha ya risasi kufuatia agizo la wakuu wa Polisi la kupiga risasi na kuuwa waliofanya ghasia.

Pia inadaiwa baadhi ya Polisi walishiriki katika ghasia hizo , wakichukua pande walizopendelea, na wengine wakakataa kufanya kazi.

Ali alikuwa wa kwanza kuwasili mjini The Hague siku ya Jumanne.

HENRY KOSGEY

Henry

Henry Kosgei


Bw Kosgey alikuwa Waziri wa Viwanda , lakini naye pia alilazimika kujiuzulu ili kuruhusu uchunguzi kufanyika kuhusu madai dhidi yake, ya kutumia vibaya madaraka.

Alizaliwa mwaka 1947 , na amekuwa katika siasa kwa muda wa miaka mingi.

Yeye bado ni Mwenyekiti wa chama cha ODM.

ICC inasema Ruto ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa vitendo vya uhalifu dhidi ya wafuasi wa chama cha PNU.

JOSHUA ARAP SANG

Joshua

Joshua Arap Sang


Sang ni mtangazaji na mwandishi wa habari katika redio ya jamii iitwayo KASS FM. KASS FM hutangaza kwa lugha ya Kalenjin.

Ana kipindi chake maalum cha asubuhi.

Mahakama ya ICC inasema kwamba wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi, Sang alikuwa miongoni mwa waliopanga uhalifu dhidi ya wafuasi wa chama cha PNU.

Sang alikuwa ametuma ombi kwa mahakama ya ICC la kutaka azungumze lugha ya Kalenjin atakapofika mbele ya mahakama hiyo, na akaomba serikali impe ulinzi, lakini maombi hayo yakakataliwa.


Hata hivyo mahakama ya ICC imekubali ombo lingine la Bw Sang la kumsaidia na gharama za kuhudhuria mahakamani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA