RICHMOND KUTIKISA BUNGE MBUNGE WA UBUNGO,JOHN MNYIKA

Mbunge wa Ubungo,John Mnyika
 NI HOJA BINAFSI ILIYOWASILISHWA NA JOHN MNYIKA WA UBUNGO

SAKATA la Richmond linatarajiwa kurudi upya bungeni baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika kuwasilisha hoja binafsi kuhusu utekelezaji wa Maazimio 13 yaliyobaki ya Bunge, juu ya mkataba baina ya Tanesco na kampuni hiyo ya kufua umeme wa dharura.Mnyika alisema jana katika taarifa yake kuwa lengo la hoja yake hiyo ni kutaka uamuzi wa Bunge la Tisa Mkutano wa 18 Februari, 2010 kufunga mjadala huo ubadilishwe ili hoja hiyo irudi upya bungeni.
“Niliwasilisha hoja hiyo Ofisi za Bunge Januari 25, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, Kanuni 54, (4) na 55 (1),” alisema Mnyika katika taarifa yake hiyo na kuongeza:
“Ikipokewa na kujadiliwa, hoja hiyo itaongeza msukumo wa utekelezaji wa maazimio ya Bunge na hivyo kuchangia katika mapitio ya mikataba yenye kuongeza bei ya umeme na kuweka mfumo wa kulihusisha Bunge katika maandalizi ya mikataba yenye maslahi kwa taifa.”
Februari 2010, Bunge lilifunga mjadala huo baada ya Serikali kutoa taarifa ya tatu ya utekelezaji wa mapendekezo yake. Taarifa hiyo ilitanguliwa na nyingine mbili zilizowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Agosti 28, 2008 na Februari 11, 2009.
Moja ya taarifa hizo ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, umefanyika hadi Februari 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwahayajakamilika.
Baadhi ya maazimio ambayo utekelezaji wake haujakamilika ni Azimio Na. 3, ambalo liliagiza Mkataba kati ya Tanesco na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na mingine kati ya Tanesco na IPTL, Songas, Aggreko na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema kama mikataba ya madini ilivyopitiwa upya na Serikali.

“Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji Tanesco zingepungua na hivyo bei ya umeme isingepandishwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa,” alisema Mnyika.

Maazimio mengine ambayo utekelezaji wake haujakamilika ni pamoja na lile lililotaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah awajibishwe kutokana na taasisi yake kushindwa kuona upungufu katika mchakato ulioipatia zabuni Richmond.

Azimio jingine ni lile lililotaka kuwajibishwa kwa watumishi wa umma akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, ambaye hata hivyo, hakuchukuliwa hatua yoyote hadi alipostaafu na kutowajibishwa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.

Katika sakata hilo, Serikali pia haijatekeleza azimio la kuwajibishwa kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi badala yake ilieleza kuwa uchunguzi ulikuwa unaendelea dhidi yake. 

“Hoja binafsi itakapojadiliwa bungeni itawezesha Bunge na wananchi kwa ujumla kupata taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo 13,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwa Mnyika kuwasilisha hoja hiyo bungeni. Aprili 13, 2011 aliiwasilisha... “Hata hivyo, niliijibu Ofisi ya Bunge kupatiwa taarifa ya utekelezaji uliofanywa na Serikali baada ya Februari, 2010 bila kupatiwa majibu hivyo nimeiwasilisha tena ili hoja husika ijadiliwe.”

“Kwa muktadha huo, hoja binafsi husika itawezesha mjadala kuhusu uamuzi husika kufunguliwa na kutoa fursa kwa jambo hilo kufikiriwa tena ili kuwezesha hatua kamili kuchukuliwa juu ya maazimio 23 ya Bunge yaliyopitishwa Februari 15, 2008 katika Mkutano wa 10 wa Bunge la Tisa.”
Mnyika alihoji Serikali kutochukua hatua zozote hadi sasa wakati ililieleza Bunge kwamba vyombo vya dola vimekamilisha uchunguzi wake wa ndani ya nchi kuhusu suala hilo.
“Hata hivyo, zoezi lililoendelea toka Februari, 2010 ni kufanya uchunguzi wa nje ya nchi kwa kushirikiana na vyombo vya dola vya kimataifa ambapo, mmoja umemalizika bila hatua zozote kuchukuliwa kwa wahusika katika kashfa ambayo maazimio ya Bunge yalipitishwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita hali ambayo inaweza kusababisha hata mashahidi na ushahidi kupotea,” alisema.
Mnyika pia alihoji sababu za kutoanza kutekelezwa ipasavyo kwa azimio la 13, lililotaka Serikali izihusishe Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara ili kuondokana na utaratibu uliopitwa na wakati kwamba mikataba ya kibiashara ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe.
Soma zaidi http://mwananchi.co.tz

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI