SUDANI NAYO YATINGA ROBO FAINALI

Sudan ilipata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya miaka 42, ilipofanikiwa Jumatatu kuishinda Burkina Faso magoli 2-1 katika uwanja wa Bata na kufuzu kuingia robo fainali.

Sudan imekuwa miongoni mwa mataifa manane yatakayoshindana katika robo fainali, hasa kutokana na Ivory Coast kuishinda Angola magoli 2-0, katika mechi nyingine ya kundi B mjini Malabo.

Mshambulizi wa Sudan Mudather El Taib alifunga bao katika kipindi cha kwanza na vile vile katika kipindi cha pili, na kuiwezesha Sudan, mabingwa wa mwaka 1970, kuendelea kuwa na matumaini ya kupata ubingwa tena mwaka huu.

Bao la Burkina lilitiwa wavuni na Issiaka Ouedraogo.

Sudan sasa itakutana na Chipolopolo ya Zambia katika pambano la robo fainali, Jumamosi tarehe 4 Februari, katika uwanja wa Bata, nayo Ivory Coast itacheza na Equatorial Guinea.

Wachezaji wa Sudan, baada ya kushindwa na Ivory Coast 1-0 katika mechi yao ya kwanza, waliweza kujikakamua na angalau kupata pointi yao ya kwanza tangu mwaka 1976, walipotoka sare na Angola siku ya Alhamisi wiki iliyopita.

Kufuatia Angola kushindwa kwa mara ya kwanza katika mashindano ya mwaka huu, timu hiyo sasa imezikosa robo fainali, baada ya ushindi wa Sudan.

Angola ilijisahau katika kulinda ngome yake, na Emmanuel Eboue aliitumia nafasi hiyo kwa kumshambulia kipa akiwa karibu sana, na baadaye Wilfried Bony akautumbikiza mpira wavuni katika lango ambalo lilikuwa wazi kabisa.

Mechi za mwisho za kundi C zinachezwa Jumanne, wakati Gabon itakapocheza na Tunisia, na wengi wakisubiri kujua ni nani ataongoza katika kundi hilo, baada ya mechi hiyo ya Franceville.

Na mjini Libreville, Morocco na Niger watakutana, na kila nchi bila shaka itafanya juhudi kubwa kujipatia pointi zake za kwanza katika mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA