TFF YAIOKOA YANGA

KATIBU Mkuu Shirikisho la Soka nchini TFF, Angetile Osiah jana aliokoa jahazi baada ya kuamua kukatisha mjadala kuhusu suala la kuchelewa kulipwa kwa mishahara ya wachezaji wa Yanga.
Tukio hilo lilitokea wakati wa mkutano wa wanahabari na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilipokuwa ikikabidhi vifaa kwa klabu za Simba na Yanga ndipo lilipozuka suala la kwa nini wadhamini hao huchelewesha mishahara ya wachezaji wa timu hizo.
Kabla ya makatibu wa timu hizo mbili, Evodius Mtawala wa Simba na Celestine Mwesigwa wa Yanga hawajatoa ufafanuzi wa kuchelewesha mishahara kwa wachezaji wao,  Katibu mkuu wa TFF, Osiah akaingilia kati na kutaka mjadala huo usiendelee.
"Hii ni press ya kutoa vifaa, msiharibu kwa kuuliza maswali ambayo mnaweza kuuliza kwa wakati wenu mkiwa huko," alisema Osiah kitendo ambacho kilionekana kuwaudhi waandishi wa habari ambao walidai kuwa suala hilo linahusu wadhamini ambao ni TBL pamoja na klabu hizo ila haliwahusu TFF.

Awali Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema kuwa wao wamekuwa wakitoa mishahara mapema ila wanashangazwa na utaratibu unaofanywa na klabu hizo kwa kuwacheleweshea mishahara wachezaji wao.
"Sisi tulipoingia kudhamini hizi klabu mbili lengo letu lilikuwa kuwaondolea ukata, hata hivyo hatuwezi kumaliza matatizo yao yote ndio maana tukaamua kuangalia yale maeneo ya msingi ambayo ni mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi waajiriwa,"alisema Kavishe.
"Hata siku moja Simba na Yanga hawaji kwetu kupanga foleni kusubiri waandikiwe cheki zao, tunaingiza fedha za malipo yao kwenye akaunti zao moja kwa moja kila tarehe 28, hayo masuala ya kulipana Simba wana utaratibu wao na Yanga nadhani wana utaratibu wao,  sisi tunachoangalia ni ripoti yetu wanayotuletea,"alisema Kavishe.
Yanga imeingia kwenye mtikisiko wa uchumi, huku ripoti ikionyesha kuwa klabu hiyo inahitaji kiasi cha shilingi 1.2 bilioni kila mwaka ili kutimiza mahitaji muhimu.
Miezi michache iliyopita Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alikaririwa akisema wanahitaji fedha hizo, ambapo kiasi cha shilingi 600 milioni ni kwa ajili ya usajili, shilingi 50 milioni ni mishahara ya wachezaji, benchi la ufundi, watumishi wa utawala na gharama za umeme na maji wakati mfuko wa Yanga pekee unaingiza shilingi 212.4 milioni kupitia mkataba wa udhamini.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa aliwahi kukaririwa akisema,"fedha inayotolewa TBL ni 25 milioni, mishahara ya wachezaji pekee ni shilingi 50 milioni, tunatafuta vyanzo vingine vya mapato ili kuondokana na hii hali."
Wakati huo huo, TBL jana imekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi 70 milioni kwa timu za Simba na Yanga tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi unaoanza kesho kwa Yanga kumenyana na Moro United wakati Simba itacheza na Coastal Union Januari 25.
Vifaa vilivyotolewa na TBL ni gloves pisi sita kwa kila timu, vilinda ugoko jozi 30, mipira ya mazoezi na mechi 30, stop watch pisi tano, kitambaa cha nahodha pisi tano, viatu vya mazoezi jozi 40 na vikoti vya mazoezi jozi 60.
Vingine ni vizuia vifundo vya mguu (10), viatu vya mechi jozi 35,  suti jozi 40, jezi  za benchi la ufundi jozi 20, jezi  za mazoezi jozi 60, jezi za mechi za ndani jozi mbili na jezi za mechi za kimataifa jozi mbili na Casual Wear jozi 20.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA