TWIGA STARS KUAGWA LEO

TIMU ya Taifa ya wanawake ya Twiga Stars inatarajiwa kuagwa na Naibu Waziri wa Maendeleo, jinsia na watoto Ummy Ally Mwalimu leo mchana kabla ya kukwea pipa jioni kwa ajili ya safari yao ya kuelekea mjini Windhoek, Namibia ambapo Jumamosi itacheza dhidi ya Namibia katika mechi ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake.

Timu hiyo ambayo ilipiga kambi Mkoani Pwani itaondoka leo usiku na ndege ya Shirika la Precision air hadi Afrika kusini kabla ya kuchukua usafiri mwingine kuelekea nchini humo.

Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Boniface Wambura aliwashukuru wadhamini kwa kujitokeza kusaidia timu hiyo huku akitoawito kwa makampuni na watu binafsi kuendelea kuisaidia timu hiyo kwani bado wana deni kubwa.

Wambura alisema bado timu hiyo haijapata fedha za posho hivyo wamewaahidi wachezaji kuwapa posho zao watakaporejea na kuendelea kusisitiza wadhamini kuendelea kujitokeza kuisaidia timu hiyo.

"Timu itaagwa kesho (leo) na Naibu Waziri Mwalimu, kabla ya jioni kuondoka kwenda Namibia,ni matumaini yetu maandalizi yao kama ripoti ya kocha inavyosema wamejiandaa vyema kukabiliana na michuano hiyo na kuahidi kutuwakilisha vyema,"alisema Wambura.

Kwa upande wa Nahodha wa timu ya Taifa ya wanawake 'Twiga Stars', Sophia Mwasikili aliwatoa hofu Watanzania na kuwaahidi kwenda kupambana kuhakikisha wanaiwakilisha vyema nchi yao katika michuano hiyo.

Mwasikili aliiambia Mwananchi jana kwa njia ya simu kuwa maandalizi duni si sababu ya wao kuvunjika moyo bali wanayachukulia kama changamoto ya kutaka waendelee kuheshimika kwa kuitangaza soka ya wanawake kimataifa.

"Nina imani kubwa na kikosi chetu, tuliweza kuliwakilisha Taifa katika mashindano mengi ya miaka ya nyuma na kufanya vizuri, timu inakabiliwa na ukata wa fedha na kama mnavyoona tumeendelea kujifua kwa kucheza na timu za vijana, lakini kwetu hii ni kama changamoto ya kuzidi kufanya vizuri na tunawaahidi Watanzania wategemee mazuri zaidi,"alisema Mwasikili.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA