WAFUASI WA GADDAFI WAUTEKA MJI LIBYA

WAFUASI wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi wameuteka Mji wa Ban Walid nchini Libya.
Mji huo ulioko umbali wa kilomita 170 kutoka mji mkuu Tripoli na ambao ulikuwa mmoja wa miji ya mwisho kabisa kutekwa na wapinzani wa Gaddafi, wakati wa mapinduzi sasa unamilikiwa na wafuasi hao.Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kutuma wanajeshi wake 12,000 ambao lengo lao likidaiwa kuwa kwenda kudhibiti visima vya mafuta na bandari nchini humo.

Maandamano ya wananchi huku yakiwa yanaendelea katika baadhi ya miji nchini humo, pamoja na utekwaji wa mji huo, vurugu mbalimbali zikiendelea kushika kasi nchini humo.Huku hali ikizidi kuwa tete nchini humo, ambapo Serikali ya mpito nchini humo, imeshindwa kupitisha sheria mpya ya uchaguzi kama ilivyopanga kufanyika wiki hii.

Abdur Razzaq al Iradi mjumbe mwandamizi wa Baraza la Mpito la Libya alisema kuwa, kazi ya kutunga sheria ya uchaguzi Libya imeahirishwa kwa wiki moja nyingine.

Hata hivyo, Fauzi Abdul Aal, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya amekanusha habari za wafuasi wa Gaddafi kuhusika katika matukio ya Mji wa Bani Walid na kusema kuwa, kilichotokea mjini humo ni ugomvi baina ya makundi hasimu na hakuna mfuasi yeyote wa Gaddafi au bendera ya kijani iliyoonekana ikipeperushwa hewani.

Wakati huohuo, zaidi ya wanachuo 4,000 wamefanya maandamano mjini Benghazi wakitaka wanachuo wenzao waachiwe huru, baada ya kutiwa mbaroni kufuatia kushiriki kwenye maandamano ya kupinga Baraza la Mpito la Libya (NTC).Hivi karibuni wananchi wa Benghazi walivamia ofisi za NTC mjini humo, wakilalamikia kutofikiwa malengo ya mapinduzi yao.

Kutokana na vurugu hizo za juzi mjini Benghazi, zilisababisha naibu kiongozi wa Serikali ya Mpito ya Libya ajiuzulu.

Abdel Hafiz Ghoga aliiambia Al Jazeera kwamba, anajiuzulu kwa sababu ya maslahi ya taifa. Waandamanaji zaidi ya 100 walivamia makao makuu ya Serikali ya Mpito mjini Benghazi juzi.

Ghoga ambaye pia ni msemaji wa Serikali amelengwa, katika madai ya kutaka Serikali ya Mpito kuwa na uwazi zaidi. Baada ya majuma mawili ya maandamano mjini Benghazi, Serikali ya Mpito, inatarajia kujiuzulu kwa naibu huyo, kutapunguza chagizo. Ghoga ndiye aliyelengwa.

Baadhi ya waandamanaji wanamshutumu kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na Serikali iliyopita ya Gaddafi. Habari zinasema kuwa, waandamanaji hao wanamwelezea kiongozi huyo kuwa na nyuso kadhaa. Hata hivyo, waandamanaji hao, wanataka Serikali ya Libya iwe na uwazi zaidi jinsi inavyotengeneza sheria mpya na jinsi inavyotumia fedha za taifa. Waandamanaji wengi wamepoteza jamaa, marafiki, au viungo katika vita vya miezi 9 dhidi ya Kanali Gaddafi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA