WATU WAWILI WAFA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI MACHIMBO YA SALASALA, DAR

Watu wawili wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba kokoto katika eneo la Kunduchi Mtongani, lililopo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo liliibua vilio na simanzi kwa wakazi wa eneo hilo  na mmoja wao kupoteza fahamu, baada ya kutolewa kwa miili ya watu hao ambayo ilikuwa imeharibika vibaya kwa kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 11:00 jioni.

Kwa mujibu wa ndugu na mashuhuda wa tukio hilo, waliofariki dunia ni Shabani Kasilu na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Muddy.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakati zoezi la ufukuaji likiendelea, baadhi ya mashuhuda hao walisema tukio la watu hao kufukiwa na kifusi lilitokea juzi saa 11:00 jioni.

“Taarifa za watu hawa kufukiwa na kifusi nilizipata jana (juzi) muda wa saa kumi na moja kutoka kwa mmoja wa walionusurika katika ajali hiyo na ndipo nilipoamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi,” alisema Malaso Stephano.

Aliongeza: “Hata hivyo, mpaka sasa sijawaona ndugu zangu wengine wawili ambao nilikuwa nikiishi nao ambao ni Shabani na Muddy, ni wachimbaji wa kokoto ambao tunahofia kwamba watakuwa wamefukiwa na kifusi hicho.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kunduchi, Richard Rusisye, alisema matukio kama hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kwamba wananchi wamekuwa wakikiuka maagizo ya kuacha kuchimba kokoto katika eneo hilo licha ya kwamba wamepigwa marufuku na serikali.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela,  alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari jeshi hilo limetoa rai kuacha mara moja vitendo vya uchimbaji wa kokoto sehemu zilizokatazwa.

“Tukio hilo limetokea kweli na watu wawili ndio waliofariki dunia, lakini tumetoa rai waache mara moja biashara hiyo haramu na nimemuagiza Mkuu wa Polisi Kawe afanye doria kwa kushirikiana na serikali ya mtaa, Manispaa na mamlaka nyingine ili watakaokamatwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Kamanda Kenyela aliongeza: “Pia tumeomba wananchi kutoa taarifa pindi watakapowaona watu wanafanya biashara katika eneo hilo.”

Uchimbaji wa kokoto katika eneo la Kunduchi ulipigwa marufuku Januari, mwaka jana na Wizara ya Ujenzi ikieleza kwamba vitendo vya uchimbaji wa kokoto katika eneo la hifadhi ya barabara ni uvunjaji mkubwa wa sheria.

Uchimbaji huo ulizuiliwa kwa kuzingatia Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, ambayo inapiga marufuku kwa mtu yeyote kufanya ujenzi, uchimbaji, utupaji taka ama uharibifu wa aina yoyote katika eneo la barabara na hifadhi yake ambalo kwa ujumla linajumuisha upana wa mita 30 kila upande toka katikati ya barabara.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA