CCM,CHADEMA WAGEUZA MAHAKAMA UWANJA WA MAPAMBANO

HALI ya usalama katika viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya Arusha ilikuwa tete jana, baada ya waliodhaniwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), kuanzisha vurugu zilizohusisha pia makada wa Chama cha mapinduzi(CCM), wakati wa kuahirishwa kwa kesi inayohusu kupinga Ubunge wa Godbless Lema(Chadema).

Vurugu hizo zilizohusisha wafuasi wa vyama hivyo vyenye upinzani mkali mjini hapa, zilitokea Saa 6:45 mchana wakati shauri la kesi hiyo likiahirishwa na kupelekea wapinzani hao kutafutana nani si mwenzao na kugundua uwapo wa kada wa CCM aliyedaiwa kuwa na silaha miongoni mwa wafuasi wa Chadema .

Chanzo cha vurugu hizo zilianzia wakati wafuasi wa CCM wakiwa ndani ya mgahawa ulioko eneo la mahakama hiyo kujipatia chochote, wenzao wa Chadema waliamua kutoka nje ya geti la mahakama na ndipo wafuasi hao wa upinzani walipomgundua mtu mmoja miongoni mwao kuwa siyo mwenzao na kuanza kumhoji kabla ya kumpekua na kudai kumkuta na silaha hizo.

Kada huyo wa CCM aliyedaiwa kujipenyeza katikati ya wana Chadema akiwa na silaha alitambuliwa kwa jina la James Mallya ambaye ni dereva wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake wa CCM (UWT) mkoa wa Arusha na alilazimika kutimua mbio hadi ndani ya mgahawa walipokuwa wenzake kujinusuru na kichapo kutoka kwa wana Chadema.

Katibu wa Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, Abdalah Mpokwa alithibitisha kumtambua kijana huyo kuwa mwanachama na dereva wa UWT na kuongeza kuwa alikimbizwa hospitali na kuruhusiwa kutoka baada ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa dawa.“Namshukuru Mungu kijana yule anaendelea vema baada ya madaktari kuthibitisha kuwa hakupata madhara makubwa, amepewa dawa na kuruhusiwa,” alisema Mpokwa.

Katibu huyo wa UVCCM aliwataka viongozi na wafuasi wa Chadema kujenga utamaduni wa kuvumiliana kuhusu tofauti za kiitikadi zilizopo miongoni mwao kwani licha ya kutofautiana, wanaendelea kubakia kuwa watanzania na wana Arusha wenye lengo moja la kujiletea maendeleo.Kwa upande wake, Kada wa Chadema, Rashid Shubet alisisitiza kumkuta mwana CCM huyo akiwa na silaha hizo katikati ya wana Chadema bila kueleweka vema alikuwa na nia gani na kuwataka viongozi wa pande zote kudhibiti hisia za wanachama na wapenzi wa vyama vyao.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Tobias Andengenye hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo baada ya simu zake zote za mkononi kutopatikana na hata Akili Mpwapwa anayekaimu nafasi hiyo hakupatikana.
Katika hatua nyingine shauri la kupinga Ubunge wa Godbless Lema (Chadema), jimbo la Arusha linaendelea kuunguruma leo kwa mlalamikaji wa kwanza, Mussa Mkanga kuendelea kutoa ushahidi wake kuhusu hoja kumi zilizowafanya wafungue kesi hiyo ambazo zinabishaniwa na upande wa madai na utetezi.


Jaji Gabriel Rwakibarila anayesikiliza shauri hilo baada ya Jaji Aloyce Mujulizi kujitoa alitaja hoja zinazobishaniwa kuwa ni pamoja na iwapo walalamikaji hao wana haki kisheria kufungua kesi hiyo.Pande hizo pia zinabishana iwapo wadai wamefungua shauri hilo kwa niaba ya wapiga kura wote wa Arusha, wametumwa au iwapo wao ni mawakala wa aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CCM, Dk Batilda Burian.

Hoja zingine ni iwapo maneno kuwa Dk Burian hakustahili kuchaguliwa kuwa mbunge wa Arusha kwa sababu ni mwanamke aliyeolewa Zanzibar na hivyo anaenda huko mara baada ya uchaguzi na kwamba ni mwanamke asiye mwaminifu aliyezaa na kupata ujauzito nje ya ndoa yalitamkwa na Mbunge Lema katika mikutano yake ya kampeni mwaka 2010.

Katika uamuzi mdogo alioutoa kuhusu pingamizi la wakili wa wadai, Alute Mugwai aliomba shahidi huyo asihojiwe kuhusu barua ya malalamiko kwa Kamati ya Uchaguzi Jimbo la Arusha juu ya Lema kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi, Jaji Rwakibarila aliruhusu shahidi huyo kutoa ushahidi na kusahihi maelezo yake yanayodaiwa na wakili Kimomogoro kuwa yanapingana na kilichomo kwenye hati ya mashtaka.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.