JK AENDA UINGEREZA LEO

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick jana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam leo, muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda Uingereza kikazi. (PICHA YA IKULU)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kesho kutwa, Jumatano, Februari 23, 2012, ataungana na viongozi wa nchi, serikali na mashirika ya kimataifa zaidi ya 40 kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Hali ya Somalia unaofanyika mjini London, Uingereza.
Rais Kikwete alialikwa binafsi kuhudhuria Mkutano huo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana David Cameroun wakati viongozi hao wawili walipokutana kwenye Mkutano wa Uchumi wa World Economic Forum (WEF) wa mwaka huu uliofanyika mwishoni mwa Januari mwaka huu, mjini Davos, Uswisi.
Rais Kikwete ambaye uzoefu wake kuhusu tatizo la Somalia utakuwa muhimu sana katika mkutano huo, ameondoka nchini leo, Jumanne, Februari 21, 2012, kwenda London kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo ambao unalenga kufikia maafikiano kuhusu namna mpya ya kimataifa ya kutatua tatizo la Somalia – A new International Approach to Somalia.
Viongozi wa nchi, serikali na mashirika ya kimataifa wanatarajia kujadili jinsi jumuia ya kimataifa inavyoweza kuongeza jitihada zake katika kukabiliana na vyanzo na matokeo ya matatizo ya Somalia ambayo sasa yamesambaa na kuathiri nchi nyingine za jirani na hata za mbali ikiwamo Tanzania.
Kwenye mkutano huo, Tanzania itaelezea uzoefu wake katika kukabiliana na uharamia wa Kisomalia ambao katika miaka miwili iliyopita umesababisha matukio 29 ya kiharamia katika Bahari ya Hindi.
Hali hiyo imesababisha kupanda kwa gharama za usafiri wa meli za mizigo na bidhaa zikiwamo zile za mafuta na kupanda kwa bima ya meli hizo. Matokeo ya kupanda kwa gharama hizo ni kupanda kwa bei za bidhaa zinazoingia nchini kupitia Bahari ya Hindi na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei nchini.
Katika miaka minne iliyopita, uharamia huo umesambaa kutoka kwenye pwani ya Somalia yenyewe hadi kwenye Ghuba ya Eden kwa upande wa kaskazini na hadi karibu na pwani ya Msumbiji kwa upande wa kusini.
Ajenda ya Mkutano huo ina mambo makubwa saba ambayo ni Usalama Ndani ya Somalia yenyewe kwa maana jinsi ya kuimarisha Jeshi la Umoja wa Afrika linalolinda amani katika Somalia, Kuimarishwa kwa Mchakato wa Kisiasa kwa maana ya kujadili aina gani ya utawala itakayochukua nafasi ya Serikali ya Muda na Taasisi zake wakati zitakapomaliza muda wake Agosti mwaka 2012, na Uimarishaji wa Utulivu wa Ndani kwa maana ya kuangalia jinsi gani jumuia ya kimataifa inavyoweza kuimarisha Serikali za Majimbo ya nchi hiyo kutokana na Serikali Kuu kuendelea kuwa dhaifu pamoja na kusaidiwa mno kimataifa.
Mambo mengine ya ajenda hiyo ni Kupambana na Uharami kwa maana ya jinsi ya kuvunjilia mbali na kuvuruga kabisa mfumo wa kibiashara wa uharamia, Kusaidia Wananchi wa Somalia kwa maana ya jinsi ya kukabiliana na zahama ya kibinadamu inayowakabili wananchi wa Somalia, Kupambana na Ugaidi kwa maana ya kupata namna nzuri ya kuyashinda makundi ya kigaida ya Al-Shaabab na Salafi Jihad, na Ushirikiano wa Kimataifa kwa maana ya kuongeza jitihada za kimataifa kushirikiana kumaliza tatizo la Somalia.
Somalia imekuwa haina Serikali tokea Januari mwaka 1991, miaka 21 iliyopita wakati utawala wa Rais Siadi Barre ulipoondolewa madarakani.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Februari, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI