JK KUPANGUA BARAZA LA MAWAZIRI

PANGA pangua ya Baraza la Mawaziri imewadia. Imeelezwa kwamba Rais Jakaya Kikwete anajipanga kufanya mabadiliko makubwa katika baraza lake, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.

Taarifa za Rais Kikwete kutaka kufanya mabadiliko hayo, zilizagaa mjini Dodoma wakati alipowasili kutoka mjini Mwanza alikokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Baadhi ya mawaziri ambao hawakupenda majina yao yatajwe, waliliambia gazeti hili kwamba Rais Kikwete anatarajia kufanya mabadiliko makubwa ya baraza lake mara baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, (NEC), kilichomalizika mjini Dodoma juzi.

Vyanzo vyetu vya habari vilisema mabadiliko hayo ambayo yatakuwa ya kwanza tangu Rais Kikwete alipochaguliwa kwa mara ya pili kumalizia awamu ya mwisho ya uongozi wake, yametokana na sababu kubwa tatu.

Mosi, yanatokana na baadhi ya mawaziri kuugua kwa muda mrefu na hivyo kulazimika kuwapa nafasi ya kupumzika, huku wakiendelea kujiuguza.

Mawaziri wanaougua na huenda wakaachwa ili kupumzisha afya zao ni pamoja na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye kuugua kwake kumeibua tuhuma nzito kwamba huenda kiongozi huyo amelishwa sumu.

Hivi sasa umeanzishwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ambazo kwa mara ya kwanza ziliibuliwa hadharani na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kati, Samuel Sitta.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, naye huenda akakumbwa na mabadiliko hayo kwani licha ya kurejea nchini na kuanza kuingia ofisini, afya yake imezidi kuzorota.

Sababu ya pili ya mabadiliko hayo inaelezwa kuwa inatokana na utekelezaji wa maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyokuwa inachunguza mgogoro wa serikali na madaktari.

Katika mapendekezo yake, kamati hiyo inayoongozwa na Magareth Sitta ilipendekeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, na Naibu wake, Dk Lucy Nkya, wawajibishwe kwa madai ya kuhusika na uzembe uliosababisha mgomo huo ambao umeleta athari kubwa nchini.

Wengine waliopaswa kuwajibishwa kutokana na mgomo huo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu, Dk. Deo Mtasiwa.

Tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza kuwasimamishwa kazi Nyoni na Dk. Mtasiwa ili kupitisha uchunguzi dhidi yao.

Sababu ya tatu, inaelezwa kuwa ni uzembe wa baadhi ya mawaziri, huku panga pangua hiyo, ikitarajiwa kuwakumba pia mawaziri ambao kwa muda mrefu wizara zao zimekuwa zikituhumiwa kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa katika mabadiliko hayo yanayotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa, Rais Kikwete ameingiza sura mpya, kuwabadilishia baadhi yao wizara, huku wengine wakitupwa nje kusubiri wapangiwa kazi zingine.

Shinikizo la Rais kutaka afanye mabadiliko katika baraza lake, limekuwa likitolewa na watu wa kada mbalimbali nchini, wakiwemo wabunge wa CCM.

Alipokuwa akizungumza na wabunge wa CCM mjini Dodoma, baadhi ya wabunge walimtaka Rais Kikwete kufumua Baraza lake la Mawaziri kwani baadhi yao wamechoka na hawana ubunifu tena. Chanzo; gazeti la Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*