Wafurahia tamasha la Pasaka Uwanja wa Taifa

Mwandishi Wetu

WADAU wa muziki wa Injili wa Dar es Salaam, wameipongeza Kampuni ya Msama Promotions kwa kuamua tamasha la Pasaka kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa badala ya Diamond Jubilee.

Maoni hayo yametolewa na baadhi ya wadau wa muziki wa Injili waishio Dar es Salaam baada ya kutangazwa kuwa tamasha la Pasaka litafanyika Aprili 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa.

"Nikiwa Mkristo mwenye kupenda kusikia ujumbe wa neno la Mungu pia kwa njia ya uimbaji, nimefurahi sana kusikia tamasha la Pasaka litafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam," alisema Jimmy Bukuku wa Mbagala.

Bukuku anayeabudu Kanisa la Pentekoste Church of Holiness Mission (PCHM) la Tandika, alisema kwa namna fulani tamasha hilo litawakuza watu kiroho.

Alisema, mbali ya kuburudisha na kufariji, ujumbe wa neno la Mungu ambao hupatikana kupitia nyimbo, huweza kuwabadili wengi.

Bukuku alisema kutokana na ujumbe wa neno la Mungu kumgusa kila mwanadamu, ndio maana muziki wa Injili umekuwa ukiwagusa wengi bila kujali ni Mkristo au Muislamu.

Alisema kwa upande wake analiombea tamasha hilo ili lifanikiwe kwa sababu limekuwa likiwabadili na kuwajenga wengi kiroho.

Alisema analisubiri kwa shauku tamasha hilo la Pasaka akiamini litakuwa lenye upako kama yaliyowahi kufanyika chini ya Msama Promotions.

Mdau mwingine aliyegusia tamasha hilo, ni Furaha Masinga wa Kanisa la Mchungaji David Mwasota ambaye kwa upande wake, alisema litasaidia wengi kuimarika kiroho.

"Tamasha linapofanyika chini ya maandalizi mazuri ikiwemo kuwashirikisha waimbaji wa ndani na nje ya nchi, huwa na msisimko mkubwa, hivyo naamini hili lijalo litakuwa la ubora wa kimataifa," alisema Masinga, mkazi wa Tabata.

Mwingine aliyepokea kwa furaha hadi kupongeza hatua ya Msama Promotions kuandaa tamasha la Pasaka ni Anna Ferdinand wa Yombo, Kigilagila.

"Mara ya mwisho kwangu kuhudhuria tamasha la Msama Promotions, ni lile la Pasaka ya mwaka 2011, ukumbi ulijaa zaidi mpaka baadhi ya watu wakakosa nafasi, hivyo ninamuomba Mungu anijalie uzima hapo Aprili 8, naamini wengi watapata nafasi kwa vile Uwanja wa Taifa ni mkubwa na nafasi itakuwa ya kutosha," alisema Anna huku akiungwa mkono na wifi yake, Violeth Meshack.

Violeth aliyemaliza kidato cha nnne mwaka jana katika Sekondari ya Tirav, alisema tamasha la mwisho kwake kuhudhuria Diamond, ilikuwa la Pasaka ya mwaka jana, hivyo anamuomba Mungu amjalie uzima na afya.

Mpaka sasa, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama amesema tamasha hilo linazidi kupanuliwa wigo mwaka huu kwa vile litashirikisha wasanii nguli, na tayari waliothibitisha ni waimbaji Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava.

Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu.

Msama alisema lengo la kuwajumuisha wasanii hao ni kutaka kulifanya tamasha hilo kuwa tofauti na miaka mingine, na litakuwa na kiingilio cha chini zaidi (kitatangazwa baadaye), ili kila mmoja ahudhurie na kupata baraka kutoka kwa waimbaji hao wanaomsifu Mungu.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.