HABARI ZA SOKA KUTOKA TFF

Release No. 039
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 13, 2012
LIGI KUU VODACOM YAINGIA RAUNDI YA 21
Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 21 kesho (Machi 14 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo mabingwa watetezi Yanga watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuikabili African Lyon.
Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni ni sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 15,000.
Mechi nyingine ya kesho itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ambapo Simba watakuwa wageni wa timu ya Polisi Dodoma.
Yanga itarejea tena uwanjani Machi 17 mwaka huu kwa pambano dhidi ya wenyeji Villa Squad litakalofanyika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati siku hiyo hiyo Coastal Union itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Machi 18 mwaka huu kutakuwa na mechi tatu ambapo Simba itakuwa ugenini Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar, Toto African itaikaribisha Polisi Dodoma jijini Mwanza wakati Azam na Ruvu Shooting Stars zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Chamazi.
TEMEKE UTD, SMALL KIDS KUSHUSHANA MACHI 31
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Dar es Salaam jana (Machi 12 mwaka huu) imeamua timu za daraja la kwanza za Temeke United na Small Kids zicheze mechi Machi 31 mwaka huu mjini Dodoma ili kupata moja itakayoshuka daraja.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Ligi Daraja la Kwanza timu tatu zitashuka daraja, moja kutoka katika kila kundi. Kwa vile AFC ya Arusha na Manyoni ya Singida kutoka kundi C tayari zimeshashuka, Kamati ya Ligi imeamua Temeke United na Small Kids zilizoshika nafasi ya mwisho katika makundi yao ya A na B zicheze mechi hiyo ili kupata moja itakayokamilisha idadi ya timu tatu za kushuka daraja.
Baada ya kumalizika hatua ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza, timu tisa zimefanikiwa kucheza hatua ya fainali ya Tisa Bora na nyingine tano za Burkina Faso ya Morogoro, Morani ya Manyara, Polisi ya Iringa, Majimaji ya Songea na Green Warriors (94KJ) zimefanikiwa kubaki Ligi Daraja la Kwanza.
KITUO FAINALI LIGI DARAJA LA KWANZA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea kupokea maombi ya uenyeji wa kituo cha Fainali za Ligi Daraja la Kwanza iliyopangwa kuanza Machi 31 mwaka huu ikishirikisha timu tisa.
Mikoa kadhaa imeshawasilisha maombi ya uenyeji lakini hakuna ambao umekamilisha masharti ya kulipa sh. milioni 25 TFF ikiwa ni gharama za uendeshaji wa fainali hizo.
Baadhi ya mikoa ambayo imeshatuma maombi ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo ni Mbeya, Morogoro, Mwanza, Ruvuma na Tabora. Kamati ya Ligi itatangaza kituo cha fainali hizo baada ya Machi 15 mwaka huu ambayo ni siku ya mwisho kupokea maombi na kutimiza masharti yaliyowekwa.
Timu zilizofuzu kucheza hatua ya fainali kutoka kundi A ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga na Transit Camp ya Dar es Salaam. Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma na Tanzania Prisons ya Mbeya wakati kundi C ni Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro na Rhino Rangers ya Tabora.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI