JK ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA WILAYA YA LINDI, MAREHEMU CHIWILE


Marehemu Paul Chiwile
                                              TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Ludovick Mwananzila kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Marehemu Paul Chiwile kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 23 Machi, 2012 Mkoani Lindi alikokuwa amekwenda kikazi kutekeleza majukumu muhimu ya kitaifa.

Marehemu Paul Chiwile alikwenda Mjini Lindi kuhudhuria Kkao cha Kamati ya Sherehe za NaneNane, Kikao cha Siku ya UKIMWI Duniani ambayo mwaka huu kitaifa itafanyika mkoani Lindi, Kikao cha Maandalizi ya Maonyesho ya SIDO ambayo Kikanda yanafanyika Mkoani Lindi, na Kikao kuhusu Wiki ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi ambayo pia kitaifa inafanyika Mkoani humo.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Paul Chiwile ambaye enzi za uhai wake nilimfahamu kama kiongozi hodari, shupavu na msaidizi muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika nchi yetu hususan katika Wilaya ya Liwale alikokuwa akiwatumikia wananchi”, amesema Rais Kikwete katika katika salamu zake. Amesema kifo chake kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale huku Taifa na hususan Wilaya ya Liwale ikiachwa na pengo kubwa la kiuongozi.

Kutokana na kifo cha Marehemu Chiwile, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkuu wa Lindi kunfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa kwa familia ya Marehemu kwa kuondokewa na mpendwa wao na mhimili madhubuti wa familia.  Ameihakikishia familia hiyo kuwa yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.   Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahala pema peponi roho ya Marehemu Paul Chiwile, na awape wanafamilia moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo.

Rais Kikwete vilevile ametoa pole nyingi kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kumpoteza kiongozi muhimu aliyejitoa vilivyo kuwatumikia.  Amewataka hali kadhalika wawe watulivu na wavumilivu licha ya kumpoteza kiongozi wao kwani kazi ya Mungu haina makosa.

Mwisho.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Machi, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI