Kutojiunga na CHF kunaleta picha mbaya Kagera-RC

Na Grace Michael, Kagera
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe amesema afya ni hazina kubwa kwa kila mwananchi ambayo inatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote hivyo akazitaka Halmashauri mkoani humo kushindana katika uandikishaji wa kaya zinazojiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Amesema kuwa kitendo cha kushindwa kujiunga na Mfuko huo kinaleta picha mbaya mkoani humo kutokana na ukweli kwamba wananchi wanazo fursa nyingi za kujiiingizia kipato.

Massawe aliyasema hayo jana mkoani hapa wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ulilenga kujadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto zinazoukabili Mfuko huo hatimaye huduma zake ziweze kuboreshwa.

"Afya ni hazina kubwa kwa kila mwananchi hivyo ni lazima suala hili tulione ni la muhimu na tulifanyie kazi, uchumi wa Mkoa huu ni mzuri tu...tusiwekeze afya zetu katika hali ya mashaka...wenzetu waheshimiwa madiwani, wabunge na viongozi wengine, hamasisheni wananchi kujiunga na Mfuko huu kwa kuwa unayo manufaa makubwa kwa afya zetu," alisema.

Aliongeza kuwa ni lazima Halmashauri zishindane katika uandishaji wa kaya kujiunga na Mfuko huu ili lengo la kuwa na afya bora kwa wote lionekane kwa vitendo.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa CHF ndani ya Halmashauri ni kuonesha kushindwa viongozi waliopo ndani ya Halmashauri husika, hivyo akaonya kuwa hali hiyo asingependa kuiona mkoani kwake.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wadau hao kutokuwa  wanaharakati katika kuchangia hoja mbalimbali kuhusiana na suala la Mfuko wa Afya ya Jamii hivyo akasisitiza kila mdau kuwa na mchango chanya ili kusaidia kuboresha huduma za Mfuko huo.

"Tusiwe kama wanaharakati ambao wanaangalia mambo kwa mtizamo hasi...lazima tuangalie kama kuna mahali pa kupongezwa Mfuko upongezwe na kama kuna eneo la kusahihiswa basi ifanyike hivyo ili kuutendea haki na uweze kudumu na kuhudumia wananchi wetu," alisema Massawe.

Aliongeza kuwa umuhimu wa suala la afya upo katika kila nchi na akasema kuwa katika nchi zingine kila mwananchi anatakiwa kuwa kwenye mfumo wa bima ili aweze kupata matibabu.

Aidha aliupongeza Mfuko kwa hatua ya kusogeza huduma kwa wanachama wake hasa kwa kusogeza ofisi katika ngazi ya Mkoa kwani hiyo ndiyo hatua nzuri na yenye kuoneshwa mafanikio.

"Natoa agizo kwa wakurugenzi wote kuhakikisha mnachangamkia fursa hii ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili huduma katika vituo vyetu ziwe bora zaidi," alisema.

Massawe alitumia fursa hiyo kuuomba Mfuko kuendelea na uwekezaji katika miradi ya maendeleo katika sekta ya afya ikiwemo uwekezaji au ujenzi wa vituo vya matibabu vya mfano.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Prof. Joseph Shija, alitoa wito kwa watoa huduma kutumia fursa zinazotolewa na Mfuko huo kwa uzalendo na uadilifu mkubwa ili badae wananchi wote waweze kunufaika na mfuko.

Akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba, aliwataka wadau hao kutoa michango yao bila woga kwa kuwa ndio njia nzuri ya kusaidia kuboresha huduma zake.

Baada ya mkutano huo wa wadau mkoani Kagera, timu nyingine ya Mfuko itaendesha mikutano katika Mikoa ya Tabora, Kilimanjaro na Tanga, lengo ni kuhakikisha wadau wanakutana na kujadili kwa pamoja ili kupata majibu ya uboreshaji wa huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*