MSAMA ATOA MSAADA WA SH. MIL.2, SARUJI MIFUKO 50 UKARABATI WA KANISA LA KATOLIKI

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama (kulia), akimkabidhi Paroko wa Kanisa la Katoliki Parokia Takatifu ya Mashahidi wa Uganda, Sigfridus Rwechungura msaada wa sh. mil.2 za kusaidia ukarabati wa kanisa hilo lililopo, Magomeni, Dar es Salaam. Katika hafla hiyo iliyofanyika kanisani hapo leo, Msama aliahidi kutoa msaada mwingine wa mifuko 50 ya saruji. Anayeshuhudia katikati ni Padri wa Kanisa hilo, Dismas Kimboi.

Na Mwandishi Wetu  
KAMPUNI ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha la Pasaka, imetoa msaada wa fedha taslimu sh. milioni 2 na mifuko 50 ya saruji kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni. Akikabidhi msaada huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema hatua hiyo ni sehemu ya kutekeleza majukumu ya dhamira ya kampuni hiyo kama ilivyokusudiwa. Msaada huo ulipokewa na Padri Sigfrid Rwechungura wa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni, alisema anaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo. "Hatuna budi kuishukuru Kampuni ya Msama Promotions kwa msaada huu na pia tunatoa mwito kwa wengine wenye uwezo wajitokeze kusaidia kuinua kazi ya Mungu," alisema Padri Rwechungura. Padri Rwechungura alitoa mwito kwa wadau mbalimbali bila kujali itikadi zao za dini, kujitokeza kwa wingi kuhudhuria matamasha ya Pasaka mwaka huu. Tamasha hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8 mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu. Tayari kundi la muziki wa Injili la Glorious Celebration Spirit of Praise 'Gospel Live' linalotamba na albamu ya Niguse, limethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka. Mbali na Glorious, waimbaji wengine waliothibitisha kushiriki mpaka sasa ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava. Msama aliyeanzisha tamasha hilo mwaka 2000, alisema limelenga kuwasaidia Watanzania milioni 1 mwaka huu kwa kuwapatia misaada anuwai. Walengwa katika misaada hiyo ni wasiojiweza, walemavu, wajane na watoto yatima ambao wanasaidiwa fedha za ada na matumizi mbalimbali ya shule. Mwaka jana walisaidiwa wanawake wajane 25 fedha za mitaji ya biashara sh. 150,000 kila mmoja na ilitoa sh. milioni 3 kwa waathirika wa milipuko ya mabomu iliyotokea kwenye kambi ya jeshi Gongo la Mboto, Dar es Salaam. Msama alisema wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo jukumu la Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete la kupambana na ukosefu wa ajira, kwa kuwasaidia watoto yatima.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI