Pasaka yawavuta Kilahiro, Kissava, Nkone, Glorious

* Mashabiki wahimizwa kumiminika Uwanja wa Taifa

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 mwaka huu, limepangwa kusheheni waimbaji kochokocho wa nyimbo za injili.

Mbali ya kurindima Uwanja wa Taifa, Aprili 8 mwaka huu, tamasha hilo pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama anasema kuwa tamasha la Pasaka mwaka huu litapambwa na waimbaji nguli wa nyimbo za kumsifu Mungu wakiwamo wa hapa nchini na kutoka nje ya nchi kama Kenya, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Uganda na Rwanda ambao wanafanyiwa taratibu za kupata vibali.

Msamba ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, inayoandaa tamasha hilo, anasema tamasha hilo la Sikukuu ya Pasaka litasindikizwa na wasanii kochokocho wa muziki wa injili.

Miongoni mwa wasanii hao ni kundi la muziki wa Injili la Glorious Celebration Spirit of Praise 'Gospel Live' linalotamba na albamu ya Niguse.

Glorious hivi sasa wanatamba na albamu ya Niguse yenye nyimbo za Unaweza Yesu, Ee Roho, Juu ya Mataifa, Mawazo, Ameni Haleluya, Nafsi Yangu, Nakupenda Yesu, Usilie na Niguse uliobeba jina la albamu.

Msama anasema mbali na Glorious, waimbaji wengine galacha wa nyimbo za injili waliothibitisha kushiriki mpaka sasa ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone na Atosha Kissava kutoka Mkoa wa Iringa.

Anasema Nkone amepania amepania kukonga nyoyo za mashabiki atakapopanda jukwaani katika tamasha hilo, na ameahidi kufanya mambo makubwa kama yale aliyofanya katika matamasha yaliyopita.

Kulingana na maelezo ya Msama, ni kuwa msanii huyo amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na kwamba amepania kwa kiasi kikubwa kupagawisha mashabiki.

Msama anawaomba mashabiki wamiminike kwa wingi kuona mambo mazuri aliyowaandalia huku Nkone akibainisha kuwa kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwake.

Mwaka juzi Upendo alizindua albamu yake iliyokuwa na nyimbo kama Zipo Faida uliobeba jina la albamu, Unitetee, Nakushukuru, Sitarudi Nyuma, Uinuliwe, Iyomana alioimba kwa lugha ya kwao (Muha) kwa maana ya Huyo Mungu, Haleluya Usifiwe, Usinipite Bwana, Hata Sasa, Inakuwaje Huokoki, Moyo Wangu na Yesu Wangu.

Kabla ya uzinduzi wake, msanii huyo alipata kukaririwa akisema kuwa kutokana na kuzaliwa katika familia ya kichungaji na kushiriki katika uimbaji tangu akiwa na umri wa miaka 10, Mungu alianza kuwa katika fani hiyo na kutoa albamu yake ya kwanza mwaka 2005.

Anasema alikuwa akiongoza kwaya tangu akiwa Sunday School na baadaye kwaya ya vijana na kipaji chake kilianza kujionesha wazi kutokana na kukubalika kila alipokuwa akiimba.

Anasema mbali na kuwa mwanamuziki wa kujitegemea sasa, amewahi kuimba katika kwaya ya KWGC ya Kigoma na Dovya Gospel Singers ya Dar es Salaam.

"Zipo Faida Kukaa na Mungu ni albamu yangu ya tatu, nilianza na Mungu Baba na Hapa Nilipo za mwaka 2005 na 2007... Albamu yangu ya Zipo Faida Kukaa imebeba zaidi ujumbe wa Mungu kwa watu tofauti na albamu zangu mbili za awali ambazo nimekuwa nikijieleza zaidi mimi binafsi.

"Lakini sijafanya hivyo kwa makosa bali kutokana na mwongozo wa Mungu mwenyewe.. Kawaida nimekuwa nikitengeneza albamu zangu kwa mwongozo wa Mungu, huwa naomba mwongozo wa kitu cha kuimba.

"Mungu alisema na mimi juu ya kutengeneza albamu yenye nyimbo za ujumbe kwa jamii kwamba zipo faida kukaa na Mungu na kumsubiri kwani yeye hachelewi wala hawahi, bali hutenda kwa wakati wake kwa wote ambao wapo tayari kuvumilia," alipata kukaririwa mwimbaji huyo.

Kwa upande wake, Msama anakumbushia matamasha yaliyopita na kutolea mfano wa namna msanii Rose Muhando alivyong'ara kwa kuimba nyimbo mbalimbali na Solomon Mukubwa ambao ni moto wa kuotea mbali.

Msama anasema wamewaandalia mashabiki wa muziki wa injili mambo mazuri yatakayowaburudisha na kuridhika. Anatamba kuwa tamasha hilo litafana kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wa muziki wa injili watakaowapa mashabiki vionjo mbalimbali.

"Kuna orodha ya waimbaji wa nyimbo za injili wengi ambao tumefanya nao mazungumzo na wengine bado tunaendelea, lakini tutatangaza mmoja baada ya mwingine tunapokamilisha mazungumzo.

"Waimbaji wote maarufu wa muziki wa Injili watakuwepo, kwani tumejipanga vizuri mno kuhakiksha kwamba tamasha hili litakuwa gumzo kila mahali.

"Mwaka jana hatukuandaa tamasha la Krismasi, hivyo nguvu zote tumezielekeza katika tamasha hili la Pasaka," anasema Msama.

Msama anasema kwamba kwa kuwa tamasha hilo lipo kwa ajili ya watu, anakaribisha maoni kutoka kila sehemu ya Tanzania.

"Tutaheshimu maoni ya wapenzi wa tamasha hili kutoka sehemu mbalimbali na kila watakalotushauri tukiona linafaa tutalifanyia kazi... lengo kubwa ni kuboresha tamasha letu," anasema.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.