SACP MPINGA ALONGA NA WANAHABARI KUHUSU MIKAKATI MIPYA YA KUPUNGUZA MATUKIO YA AJALI NCHINI

Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP, Mohammed Mpinga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu mikakati mbalimbali waliyopanga kupunguza matukio ya ajali nchini. Kushoto ni Ofisa Mfawidhi wa  Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johansen Kahatano.
Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mohamed Mpinga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu mikakati mbalimbali waliyopanga kupunguza matukio ya ajali nchini. Kulia kwake ni Ofisa Mfawidhi wa  Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johansen Kahatano.
Ofisa Mfawidhi wa  Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johansen Kahatano akifafanua jambo mbele ya wanahabari
 Baadhi ya maofisa wa kikosi hicho wakisikiliza kwa makini wakati SACP, Mpinga akizungumza
                                             Wanahabari wakiwa kazini wakati wa mkutano huo 

                                                TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
 
                                                       NDUGU WAANDISHI WA HABARI,
                                                                  MABIBI NA MABWANA.

Awali ya yote napenda  kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana waandishi wa habari wote kwa kazi nzuri mnayofanya katika kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi juu ya sual zima la Usalama barabarani. Kama mjuavyo mwishoni mwa wiki ijayo tutakuwa na sikukuu za PASAKA na Kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Z anzibar hayati Abeid Karume.
 
Wakati wa siku zote hizi wengi watakuwa na pilikapilika za hapa na pale ikiwa ni pamoja na kufanya ibada, lakini wengine watakuwa katika kumbi za burudani na wengine kuziona kama siku za kufanya starehe kwa kunywa pombe na kulewa kupita kiasi.
 
Jeshi la Polisi hususani Kikosi cha usalama barabarani kinapenda kuwatahadharisha watumiaji wote wa barabara hasa madereva, kwamba askari wote wa kikosi hicho watakuwa kazini kuhakikisha kuwa hakuna hata Dereva mmoja atakayeendesha gari kwa uzembe ama kwa ulevi na kusababisha ajali za makusudi.
 
Jeshi la Polisi linawaonya vikali madereva na watumiaji wengine wa barabara wakiwemo waendesha bajaji, pikipiki, baiskeli, maguta na mikokoteni na wale waendao kwa miguu kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyopelekea ajali. Tunawataka pia Madereva wote wa mabasi yaendayo mikoani, ama kufanya safari kati ya mkoa mmoja na mwingine, kuacha kabisa kwenda mwendo wa kasi ili kuepusha ajali.
   
Tunawaomba abiria na wananchi wote kwa ujumla kulisaidia Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa pale wanapoona ukiukwaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani, kwani nia ya kila abiria ni kufika salama kule anakokwenda na wala sio kuishia njiani aidha kwa kujeruhiwa ama kufariki kutokana na ajali za barabarani.

Mwisho tutachukua hatua kali sana za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria za Usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kufungiwa au kunyang’anywa kabisa leseni yake.
MWELEKEO  WA  AJALI ,
Ajali za barabarani kwa miezi miwili Januari hadi Februari  mwaka huu zimepungua kwa 10% ukilinganisha na mwaka 2011 kwa muda uleule. Kwa mwaka huu kunaongezeko la 14% ya vifo na majeruhi  kumepungua kwa 6%  ukilinganisha na mwaka jana.

MLINGANYO WA AJALI ZA  BARABARANI  ( T) BARA  ZILIZO SABABISHA VIFO NA KUJERUHI KATI MIEZI JAN-FEB 2011 NA JAN-FEB  2012.

MWAKA    AJALI    VIFO    MAJERUHI     
2011 JAN-FEB    4080    530    3227     
2012 JAN-FEB    3688    603    3026     
 + / -    -10%    +14%    -6%    

MLINGANYO WA AJALI ZA PIKIPIKI TANZANIA BARA ZILIZOSABABISHA VIFO NA MAJERUHI KATI YA JAN-FEB 2011 NA  JAN-FEB 2012.

MWAKA    AJALI    VIFO    MAJERUHI     
2011 JAN-FEB    1043    134    806     
2012 JAN-FEB    813    159    815     
 + / -    -22%    +19%    +1%    

Takwimu hizi za ajali za pikipiki zimeonekana kuwa zimepungua kwa 22% lakini vifo  vimeongezeka kwa 19%. Katika mikoa 10 ambayo ina ajali nyingi za pikipiki ni Pamoja na Mkoa wa Dar Es salaam unaongoza  ikifuatiwa na Morogoro, Ruvuma, Arusha, Pwani Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Manyara na Mtwara.

IDADI YA AJALI ZA BARABARANI ZILIZOSABABISHA VIFO NA MAJERUHI KATI YA MWAKA 2010 NA MWAKA 2011.

MWAKA    AJALI    VIFO    MAJERUHI     
2010    24665    3582    20656     
2011    23986    3981    20802     
+ / -    -3%    +11%    +1%    

Ajali za barabarani mwaka 2011 zilipungua kwa 3% hiyo nikutokana na na mikakati ya Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani kuhakikisha kwamba ajali za barabarani zinapungua au kuisha kabisa. Mikakati mbalimbali ambayo ilitumika na inaendelea kutumika ambayo ni pamoja na kutoa elimu ya Usalama barabarani kwenye Radio,Tv, kufundisha watoto mashuleni.Elimu ya Usalama inatolewa kote nchini. Pia usimamizi wa sheria za Usalama barabarani tukishirikiana na wadau mbalimbali kama vile SUMATRA n.k.

MIKAKATI YA KUKABILIANA NA AJALI ZA BARABARANI.
Kikosi kimeanzisha programmu mbalimbali katika kuhakikisha kuwa ajali za barabarani zinapungua au kuisha kabisa. Programmu hizo ni pamoja na:

MUONGO WA UMOJA WA MATAIFA WA USALAMA BARABARANI (UN DECADE OF ACTION FOR ROAD SAFETY) 2011 – 2020.
Ajali za barabarani zimekuwa ni tatizo kubwa duniani. Inakadiriwa zaidi ya watu milioni moja na laki tatu (1.3 milion) hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani duniani kote hii ni sawa na vifo 3000 kila siku.  Asilimia 50 ya watu wanaokufa kwa ajali hizi ni watu ambao hawamo ndani ya magari bali wanajikuta wakipata madhara ya ajali hizi. Hawa ni watumiaji wa barabara walio hatarini kama watembea kwa miguu, wapanda baiskeli na pikipiki.
Bara la Afrika ndilo linaloongoza kwa idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani (asilimia 20 ya vifo) hali ya kuwa bara la hili lina asilimia 2 tu ya magari yote duniani. Ajali za barabarani zinashika nafasi ya nne kwa kusababisha vifo vya watu wenye umri wa miaka 5 hadi 44 barani Afrika (zinaua kuliko hata malaria).
Kutoka na tatizo hili la ajali za barabarani Umoja wa Mataifa umeliona hili ni tatizo linalohitaji kupatiwa tiba vinginevyo linaweza kuongezeka kama hatua thabiti hazitachukuliwa. Ndipo azimio la Umoja huo lilipitishwa la kupunguza vifo na majeruhi zinazotokana na ajali za barabarani duniani kwa asilimia hamsini (50%) ifikapo mwaka 2020 na uzinduzi wa azimio hili ulifanyika tarehe 11/05/2011.
Miongoni mwa mambo yaliyolengwa kusimamiwa kwa umakini wa hali ya juu ili kuhakikisha lengo la kupunguza ajali linafikiwa ni haya matano:
i.  Menejimenti ya usalama barabarani (Road Safety Management),
ii. Barabara salama (Safer roads and Mobility),
iii. Magari salama (Safer vehicles),
iv. Watumiaji salama wa barabara (Safer Road users),
v. Kuimarisha huduma baada ya ajali au uokoaji (post crash response),
Tanzania ambayo pia ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa nayo ipo katika mchakato wa utekelezaji wa azimio hilo la Umoja wa Mataifa la kupunguza ajali za barabarani.
SMARTER TRAFFIC PROGRAMME.
Smarter Traffic ni mpango unaoelenga kuboresha  mwenendo wa shughuli za usalama barabarani Tanzania. Ni utafiti uliofanywa na kampuni ya IBM-International Bussiness Machine toka Marekani. Katika utafiti huo ulibainisha maeneo saba ambayo yakifanyiwa kazi ipasavyo swala la ajali na kero za barabarani zinakwisha.
i)Elimu ya Usalama barabarani inahitajika kwa jamii yote Tanzania.
ii)Unahitajika usimamizi wa vyombo vya moto vikiwa barabarani.
iii)Kuwa na Kanuni za uagizaji wa vyombo vya moto vyenye usalama.
iv)Kushirikishwa kwa wadau mbalimbali kutaleta tija barabarani.
v)Kuwa na barabara salama zinazokidhi watumiaji wote wa barabra.
vi)Kuwa na vifaa vya mawasiliano kwa Jeshi la polisi na idara husika.
vii)Kusimamia sheria na kanuni zilizopo.
Kikosi kimeanza kuyafanyia kazi baadhi mambo hayo.

JUNIOR PATROL PROGRAMME,
Mpango wa kujivusha  watoto wa shule barabarani (Junior Patrol). Huu ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na watafiti wa SMARTER TRAFFIC Japo kuwa mpango huu ulianza kabla ya Utafiti huu, Kwa kuzingatia kwamba programme ya smater traffic inakwenda sambamba na mipango mingine iliyokuwepo kabla, mpango wa kujivusha watoto ulianza kwa shule 12 za msingi zilizopo mkoani Dar es Salaam zimeongezeka na kufikia shule 22 nchi nzima. Mikoa mingine ambayo imeanza kutekeleza mpango wa Junior Patrol ni Arusha, Morogoro, Kagera  Mbeya Tabora na  Shinyanga.

TRAFFIC WARDEN PROGRAMME.
Huu ni mpango wa kuwatumia wananchi katika kusimamia sheria za usalama barabarani. Lengo kubwa la kuanzisha mpango huu ni kuhamasisha wananchi washiriki katika kusimamia sheria za usalama barabarani na kuhamasisha mtazamo chanya kwa wananchi dhidi ya kikosi cha usalama barabarani ili kupunguza ajali za barabarani. Mfano kwa sasa kuna askari 40 wa manispaa ya Ilala tumewapa mafunzo ya Usalama barabarani ambao watasaidia kutatua kero na makosa yanayofanywa na madereva.


CHANGAMOTO ZA USALAMA BARABARANI.
Uelewa mdogo kwa wapanda pikipiki ikiwa pamoja kutumia vyombo hivyo bila kupata leseni ya Udereva.
Kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha katika kudhibiti makosa ya barabarani.
Utoaji na kupokea rushwa  bado tatizo hilo lipo kwa kiasi hivyo linahitaji ushirikiano kwa watu wote hasa kuwachukulia hatua wanaoshawishi kutoa rushwa na wale wanaopokea.
Madereva wa magari baadhi ni wavunjifu wa sheria na kanuni za barabarani.
Madereva wa daladala kutokufuata njia walizopangiwa hasa muda waalfajiri na Usiku.
MAFANIKIO YA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI.
Kupungua kwa ajali kwa 3%  ikilinganishwa na mwaka 2010.
Kikosi Cha Usalama Barabarani kupata ushirikiana na VETA na vyuo vya Udereva mikoa yote kuendelea kuwahamasisha wapanda pikipiki kupata mafunzo kwa gharama nafuu na baada ya mafunzo wanapata cheti cha kuhitimu ndipo wanaomba leseni. Kupitia mafunzo hayo watafahamu umuhimu wa kuvaa helmet na kufuata sheria/kanuni za usalama barabarani.
Ushirikiano wa Kikosi Cha Usalama Barabarani na SUMATRA katika kukabiliana na madereva wanao katisha route au kuiba route ambayo hupekea kero kwa wananchi.
Ushirikiano wa vyombo vya habari na kikosi chetu nchini kote kutupa vipindi vya Radio, Televisheni, kutoa elimu ya Usalama barabarani kwa umma.
Pia kuwa na ushirikiano mzuri na shule  kutupa vipindi vya kufundisha shule za Msingi na Sekondari.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.
IMETOLEWA NA:           MOHAMMED .R. MPINGA – SACP.
              KAMANDA  WA POLISI
             KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (T).


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU