Sekeleti wa Zambia kushiriki Pasaka

Na Mwandishi Wetu

MWIMBAJI wa muziki wa Injili kutoka Zambia, Ephraim Sekeleti Mutalange amethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ambaye ni Mkurugenzi wa Msama Promotions, waandaaji wa tamasha hilo, Sekeleti amekubali kushiriki.

Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za kumsifu Mungu atatua nchini akiwa na albamu zake za Acha Kulia na Mungu Mwenyewe.

Msama alizitaja baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo kuwa ni Uniongoze na Kidonge cha Yesu. Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu.

"Sekeleti ameomba mashabiki wajitokeze kwa wingi, hivyo ni nafasi nzuri kwa Watanzania kufika kumshuhudia mwimbaji huyo," alisema Msama.

Aliongeza kwamba Sekeleti atakuja nchini na waimbaji wake 10 na ataimba 'live' siku hiyo ambayo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Sekeleti ni mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili nchini Zambia, alizaliwa mwaka 1983 katika mji wa Kalulushi, Zambia. Alimaliza elimu yake ya sekondari katika Shule ya Kalulushi mwaka 2001.

Sekeleti ni mtoto wa pili kutoka mwisho kati ya watoto sita. Aliingia kwenye muziki wa injili tangu akiwa kinda huku alifundishwa kupiga kinanda na mmisionari.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu lina malengo ya kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane wasiojiweza.

Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.

Mbali na Sekeleti, wasanii wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Rebecca Malope, Rose Muhando, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Atosha Kissava na kundi la Glorious Celebration.

Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na albamu yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka na Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC.

Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI