WANASIASA WANAOJITAPA KUIGEUZA ARUMERU TUNISIA KUKIONA: POLISI

Kamishna Msaidizi wa Polisi Isaya Mngullu

* Yasema imejiandaa kisawasawa  kusambaratisha vyanzo vyote vya vurugu vitakavyojitokeza


* Watakaozianzisha kuwa wa kwanza kushukiwa

USA RIVER
Zikiwa zimebakia siku tatu ufanyike uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki,  Jeshi la Polisi limewaonya wanasiasa wanaojitapa kuwa jimbo hilo litageuka Tunisia kwa umwagaji damu, na kusema kwamba jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kukabiliana na yeyote atakayejaribu kuvuruga amani tangu sasa hadi mwisho wa uchaguzi.


Limesema limeshasikia kauli za baadhi ya wanasiasa wakijitapa na kuwashawishi kwenye mikutano ya kampeni kwamba vyama vyao visipopata ushindi Arumeru Mashariki patachimbika na kuwa kama Tunisia, kauli ambayo limesema ni ya hatari sana kwa wapenda amani na utulivu.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Operesheni Jimbo la Arumeru Mashariki, Kamishna Msaidizi wa Polisi Isaya Mngullu alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kila hatua moja kunakuwa na doria imara zikiwemo za askari waliovaa kiraia.


Akitoa taarifa ya hali ya hali ya ulinzi na usalama katika kipindi cha kampeni zinazoendelea, Mngullu alisema jumla ya matukio 36 ya uhalifu wa kisiasa yameripotiwa na kuendelea kuchukuliwa hatua mbalimbali. 


Mngull alisema  miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kwafikisha mahakani kwa hatua zaidi za kisheria na kuyataja matuki hayo kuwa ni ya kujeruhi, matumizi ya lugha za matusi, kuchana picha za wagombea, kushambulia mwili, kuchana bendera, kutishia kuua, kuchoma moto bendera, wizi wa bendera na kuharibu mali na kwamba matukio hayo yapo kwa idadi mbalimbali.

“Mpaka sasa kesi nne namba USR/IR718.2012 CC No. 227/2012 kuharibu mali, USR/IR/721/2012 CC No. 228/2012 shambulio, USR/IR/780/2012 CC No. 241/2012 shambulio ,USR/IR/749/2012 CC No. 230/2012 shambulio zimepelekwa mahakamani" alisema Mngullu na kuongeza.

“Kesi mbili USR/IR/687/2012  shambulio la kudhuru mwili na USR/IR/694/2012  shambulio  la kudhuru mwili zimepelekwa ofisi ya mwanasheria kwa hatua za utendaji na zilizobakia zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.".


Mbali na taarifa hiyo jeshi hilo pia limebainisha kwamba linaendelea kufanyia kazi matamko yaliyotolewa na baadhi ya vyama vya siasa vinavyoshiriki kufanya kampeni kwa kutumia lugha za matusi, kudhalilishana, uchochezi na vitisho kwa vyombo vya dola kuwa ushindi usipopatikana  Arumeru patachimbika na kuwa mfano wa Tunisia.

Mngullu alisena Jeshi la polisi limestushwa sana na kauli hizo kutolewa na wanasiasa wawapo majukwaani huku Asasi za kiraia zinazopigania haki za binadamu na utawala bora hususani wanaharakati wakiwa wamekaa kimya na kushindwa kujitokeza na kukemea vitendo hivyo badala yake kusubiri kutoa matamko ya kulaumu polisi pale linapoingilia kati na kuchukua hatua za kurudisha hali ya utulivu na amani kutokana na vitendo vya uvunjifu amani vinavyosababishwa na kuchochewa na viongozi.


Mbali na kuonyesha kusikitishwa, jeshi hilo limekemea na kuvitaka vyama vya siasa vinavyojifanya maandamano na misafara batili mara baada ya kumaliza mikutanio yao ya kampeni kuacha mara moja kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuvunja sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

Mngullu alisema, zipo taarifa kwamba moja ya vyama ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa kufanya maandamano ni CHADEMA na kutoa mfano kwamba  baada ya mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Jumatatu mjini Usa River, walionekana wakiongoza misarafa ya wanedesha pikipiki kuzunguka mitaani wakiandamana na malori yao Fuso ya chama hicho jambo ambalo lingeweza  kuhatarisha amani.


Kamishna Msaidizi Mngulu aliwataka wanasiasa wanaohamasisha wafuasi wao, wakereketwa na wanachama kulinda kura za mgombea wao kuacha mara moja kitendo hicho kwani kila Chama kimeweza kutoa wakala ambaye kimemuamini kwa kazi hiyo. 


“Wanachama hawana sababu ya kuhamasishana kulinda kura kwani kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 80 (2) (G) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 ya Mwaka 2010 inabainisha wazi kuwa kila Chama kitakuwa na wakala wake wa kuhakiki na kulinda kura za mgombea ndani ya kila chumba cha kupigia kura,” alisema Kamishna Msaidizi Mngulu. 


Kamishna Msaidizi Mngulu alivitaka vyama vya siasa kujipanga baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, ambapo alikitaka Chama kitakachokuwa kimeshinda kuainisha mapema sehemu, muda na taratibu za kusherehekea ushindi wao bila kuathiri na kubughudhi shughuli au mali za watu wengine. 


Uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru Mashariki, utafanyika Aprili Mosi mwaka huu, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM Jeremiah Sumari mapema mwaka huu ambapo jumla ya vyama vinane vimeweka wagombea. Chanzo, Nkoromo Blog

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU