WAZIRI MWINYI,KOVA NA LUNDENGA WAMESOMA AZANIA SEC.SHULE ILIYOKUWA INAOONGOZA KITAALUMA

MWAKA 1934 Serikali ya kikoloni ilijenga shule maalumu kwa ajili ya wanafunzi wenye asili ya Kiasia. Baada ya kukamilika, shule hiyo iliitwa Government Indian Primary School Mtendeni.

Mwaka 1939, shule hiyo iliyokuwa eneo la Mtendeni katikati ya mji wa Dar es Salaam, ilibadilishwa jina na  kuwa Government Indian Secondary School Mtendeni ambapo sasa watoto wa kiume pekee ndio waliokuwa wakisoma badala ya mchanganyiko kama ilivyokuwa awali.

Mwaka 1952 shule hiyo ikahamishwa kutoka Mtendeni hadi eneo ilipo sasa Shule ya Sekondari ya Azania. Ikaitwa Government Boy School, huku  ikiendelea kusomesha watoto wa Kiasia.

Hii ndiyo hadithi ya chimbuko la shule marufu ya Sekondari ya Azania, jina lililoasisiwa mwaka 1952 baada ya shule hiyo kuanza kusomesha watoto wa Kiafrika.

Hata hivyo, wakati jina hili linaanza kutumika historia inaonyesha bado asilimia kubwa ya wanafunzi wake walikuwa watoto wa Kiasia kwa zaidi ya asilimia 90.
Azania ya sasa

Kama ilivyo kwa shule karibu zote zilizojengwa tangu enzi za ukoloni, Shule ya Sekondari ya Azania  kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali  ikiwamo uchakavu wa majengo.

Mkuu wa Shule hiyo, Bernald Ngoziye, anasema kinachosikitisha zaidi kuhusu majengo hayo ni kuwa baadhi hayajapakwa japo rangi tangu yajengwe miaka zaidi ya 55 iliyopita.

“Majengo mengi yanavuja sana.  Kuongezeka kuvuja kwa majengo haya, kulitokana na kuyaezeka  tena. Majengo yote kwa jumla yanahitaji ukarabati mkubwa,” anaeleza.

Aidha, anasema  miundombinu mbalimbali shuleni hapo ikiwamo ile ya maji taka, imekufa kabisa.
“Mimi nilisoma katika shule hii na nilimaliza kidato cha nne mwaka 1986.  Kama shule hii ingekuwa inazungumza, ingetulilia sana sisi watu tuliosoma hapa miaka ya zamani,’’ anasema na kuongeza:

“Ilikuwa kwenye hali nzuri sana, majengo yake safi. Miundombinu yote ilikuwa safi sana, lakini kwa sasa haitamaniki kabisa.”

Anasema pia  shule hiyo inahitaji kusukwa upya kwa mfumo wa nyaya za umeme katika majengo yake yote.
Changamoto nyingine kwa mujibu wa Ngoziye ni  uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia hususan vitabu na vifaa.

“Pia tuna upungufu wa walimu. Tunatumia walimu wa nje ambao siyo wa uhakika sana. Tungepata kama walimu sita wa Fizikia, Kemia na Baiolojia, kidogo hali ingekuwa afadhali,” anaeleza zaidi.

Anasema  kuwa, maji safi ni changamoto nyingine inayoikabili shule ambayo kwa sasa ina kisima kimoja pekee kinachotumiwa kwa shughuli za shule na wanafunzi ambao ni zaidi ya 2000.

Licha ya changamoto hizi, mwalimu Ngoziye anasema uongozi wa shule umekuwa mstari wa mbele kuwahimiza walimu kufanya kazi kwa moyo na ari zaidi.

Aidha, anasema shule imeandaa mkakati wa kuwasiliana na watu mbalimbali walisoma hapo kwa ajili ya kutafuta njia za kuisadia shule iepukane na kadhia inazozikabili.

Maendeleo ya taaluma

Kuhusu taaluma anasema hali siyo nzuri kwa kiasi fulani, kwani baadhi ya nyakati wamekuwa wakipokea wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika.

Aidha, tofauti na miaka ya nyuma shule hiyo ilipokuwa ikitamba katika matokeo ya mitihani ya taifa, anasema kwa sasa matokeo hayo yamekuwa yakishuka kila mwaka.

Kwa mfano, katika mtihani wa  kidato cha sita mwaka 2009 wanafunzi waliopata daraja kwanza walikuwa 34, daraja la pili 67, la tatu 105,  la nne 40 na sifuri 32.

Mwaka 2010,  daraja la kwanza walikuwa 13, la pili 71, la tatu 200, nne 60 sifuri 36. Mwaka 2011, daraja la kwanza walikuwa wanne, la pili 41, la tatu 152, la nne 58 na sifuri 69.

Kwa upande wa kidato cha nne, mwaka 2008 waliopata daraja la kwanza walikuwa 103, la pili 127, la tatu 110, la nne 121 na sifuri 22. Mwaka 2009, daraja la kwanza  ni 67, la pili 76, la tatu 137, la nne 203 na sifuri 94. Mwaka 2010  daraja la kwanza 56, la pili 62, la tatu 122, la nne 207 na sifuri 159.

Wanafunzi maarufu 
Kwa mujibu wa mwalimu Ngoziye, baadhi ya watu maarufu nchini waliopitia Azania ni pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu,   Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman  Kova, Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (Muhas), Profesa Kisali Pallangyo na mratibu wa shindano la Miss Tanzania,  Hashimu Lundenga.
Wengine ni...

Hata hivyo, mwalimu huyo anasema  ni Kamanda Kova peke yake aliyewahi kuitembelea shule hiyo  na kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo mipira kwa wanafunzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teophile Kisanji (Teku), Nikodemo Mbwambo aliyesoma hapo   kati ya mwaka 1964 na 1967, anasema Azania ya enzi zao ilijaa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, wanafunzi wachache darasani na walimu waliokuwa na ari ya kufanya kazi

“Sifa kubwa ya shule wakati ule ilikuwa ni kufanya vizuri kwenye mpira wa miguu pamoja na taaluma,” anaongeza kusema Mbwambo.

Na Fredy Azzah wa gazeti la Mwananchi

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*