ZITTO ATAKA KUGOMBEA URAIS 2015

Sitta awashangaa CCM wanamhofia kwa nafasi hiyo
Fidelis Butahe
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Zitto Kabwe ameibuka na kusema kuwa anataka kuwa rais wa Tanzania mwaka 2015.Wakati Zitto akitoa kauli hiyo nzito, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta naye amesema anashangazwa na watu wanaoweweseka wanaposikia kuwa mwanasiasa huyo anayeongoza vita dhidi ya ufisadi ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, anataka kuwania urais.

Kauli hiyo ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni huenda ikaibua mjadala mzito ndani ya chama chake, ukiacha zile mbio za vigogo wa CCM wanaotajwa kuutaka urais 2015.

Katika taarifa yake aliyoituma jana kwa gazeti la Mwananchi Jumapili, Zitto alisema; “ Kwanza niseme wazi kabisa kuwa Urais ninautaka, nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi.” Alitamba anao uwezo kwa kuwa ni mzalendo, mwenye utashi wa kuleta mabadiliko stahiki kulingana na nchi inavyoongozwa. Katika taarifa hiyo ameeleza kuwa kwa sasa nchi imesahau maendeleo ya watu badala yake imejikita katika maendeleo ya vitu.

“Ninajua kuwa hivi sasa viongozi wetu wengi wanaangalia zaidi mitindo badala ya mambo ya msingi,” Zitto amesema taarifa na kuongeza: “Ninajua kuwa maendeleo vijijini yamesahaulika, ninajua nchi yetu inahitaji uongozi wa kufanya mabadiliko makubwa badala ya mabadiliko ya juujuu.”
Alieleza kuwa mabadiliko makubwa yanahitaji maamuzi magumu yatakayoudhi wengi hasa vigogo wa nchi za Magharibi huku akitoa mfano kuwa ni pamoja na kuzuia nchi kuuza malighafi pekee. Alisisitiza kuwa rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo ya nchi na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi.

“Rasilimali kama madini, mafuta, gesi asilia, ardhi na nyinginezo ni lazima zifaidishe wananchi wa nchi yetu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Sababu za kutaka Urais Katika taarifa hiyo Zitto alieleza kuwa kwa sasa nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto muhimu na kwamba yeye anaweza kuwaongoza Watanzania kukabiliana na changamoto hizo. “Sio kazi rahisi, lakini ni kazi ambayo lazima Mtanzania mmoja aifanye, mimi nataka kuifanya, nina uwezo wa kuifanya,” alitamba katika taarifa hiyo.

Alieleza kuwa hata kama anaitaka kazi hiyo, ni lazima Watanzania walio wengi waamue, pia ni lazima Chadema kiseme wazi kuwa yeye ndio anastahili kuifanya kazi hiyo na kwamba kuitaka tu nafasi hiyo hakutoshi bila ridhaa hizo. “Kama wananchi watasema huyu Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama hawataki kabisa tuache iwe hivyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Umri wa kugombea urais Katika taarifa hiyo, Zitto alieleza kuwa mjadala wa umri wa kugombea urais umekuwa mkali na kwamba baadhi ya watu kwa sababu zao binafsi, wameamua kuuita ni mjadala wake na Mbunge wa Bumbuli January Makamba ambao unaowabagua wazee.
Alisema kuwa mjadala huo aliouita wa ‘kupandikiza chuki na sumu za kibaguzi’ ni wa kitabaka, unaonyesha kuwa Zitto na January sio tabaka stahili la vijana walio wengi. Huku akionyesha kujibu makala katika moja ya magazeti(sio ya Mwananchi Communications Limited) ambayo haikupinga umri bali hoja ya wanaoujadili urais na vyama wanavyotoka kutowapika vilivyo vijana kuwa viongozi, Zitto alieleza kuwa hali hiyo inaonyesha ubaguzi wa wazi.

“Ingawa sisi sio waanzilishi wa hoja hii lakini ni hoja ya kibaguzi. Nawashangaa wasomi wa siku hizi kwa kujadili watu badala ya hoja,” ilieleza taarifa hiyo. Chadema kukuza vijana Alieleza kuwa Chadema kinalea na kukuza vijana kuwa viongozi na kwamba yeye alijiunga na chama hicho akiwa na umri wa miaka 16 huku akipewa majukumu mbalimbali.
Alisema kuwa wakati akisoma Chuo Kikuu Dar es Salaam(UDSM), Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Hai, alimuomba kushiriki kikamilifu kukijenga chama hicho kutokana na kukimbiwa na wanachama isipokuwa wale waliokuwa wakitokea Kigoma, Kilimanjaro, Shinyanga, Karatu na Ukerewe.

“Mwaka 2001 muongo mmoja uliopita ni mimi na Mbowe ndio tuliofanya mabadiliko yote yanayoonekana Chadema. Tumeingiza watu wapya na tumeandika Katiba upya, tulichambua mambo mengi na Mbowe kuijenga Chadema,” alieleza katika taarifa hiyo.

Alieleza kuwa mwaka 2005 Mbowe aligombea urais na kwamba walijua kuwa watashindwa ila walitaka kukijenga chama hicho na walipata wabunge na kuongeza kuwa mwaka 2010, Chadema kilishiriki uchaguzi mkuu kama chama imara kinachokwenda kuchukua dola. Huo ndio ukawa mwanzo wa kuibuka kwa wabunge John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), wabunge ambao alieleza kuwa awali walionyesha wasiwasi mkubwa kujiingiza katika siasa.
“Baadhi ya watu wazima waliingia Chadema kwa sababu ya vijana, nani anasema hatulei vijana kuwa viongozi wazuri, nani haoni hazina ya viongozi vijana hivi sasa ndani ya Bunge kutoka vyama vyote. Kuna namna bora ya kulea viongozi zaidi ya kuwapa majukumu?” Alihoji katika taarifa hiyo.

Hoja ijadiliwe Katika taarifa hiyo Zitto alifafanua kuwa hoja ya umri wa kugombea urais iwe na mahali pakuanzia na inapaswa kujadiliwa bila kuangalia majina ya wanaotetea hoja hiyo. Suala hilo lijadiliwe kwa faida na hasara zake na kufafanua kuwa hakuna anayejua kuwa yeye atakuwa hai mwaka 2015 na kwamba isiandikwe katiba yenye kupanua wigo wa kutoa haki ya kugombea urais kwa sababu yake.
Samuel Sitta

Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika Tamasha Vyombo vya Habari lililofanyika jana kwenye Ukumbi Msasanki Beach, Dar es Salaam, Sitta alieleza kuwa anashangazwa na watu wanaoweweseka wakisikia anataka kuwania urais mwaka 2015.

"Nashangaa watu wanapata kiwewe kusikia nataka kuwania urais, kuwania urais ni haki ya kila Mtanzania na Watanzania ndiyo watakaoamua nani ni mzuri na atawafaa," alisema Sitta na kushangiliwa na waliohudhuria tamasha hilo.

"2015 tunataka kuwa na mwelekeo mzuri, nikiwa na maana mambo ya hongo, ubadhirifu hatutaki yawe na nafasi, alisema Sitta na kuongeza:

"Kuna hadithi moja, siku moja trafiki mmoja alikamata gari pale Mwenge (Dar es Salaam) akaomba, leseni, akaangalia kadi ya gari sasa yule mama alikuwa na mtoto wake ana miaka kama minane, akamwambia mama yake, mpe kitu kidogo...hivi imefikia hatua hata mtoto wa miaka minane anajua rushwa."

Alisema rushwa imesababisha nchi kuingia mikataba ya uongo, kuna mikataba mingi ya uongo na ndio maana leo hii nchi imefika hapa ilipo.

"Hii imesababisha matatizo hadi ya umeme, tungeweza kuuza umeme wetu nje, lakini leo haiwezekani, nasema haya kama mzee wenu na kiongozi wenu.

"Sasa, nawaasa waandishi, msikubali kuwa mawakala wa viongozi waongo, msikubali uongo na kama tungeendelea kule uongo, nchi ingeharibika...hatuwezi kusonga mbele kwa uongo na vyombo vyenu visitumike kusambaza mambo ya uongo," Sitta alishauri.
Alisema watu wanatumia fedha nyingi kusaka urais na hata wengine kutumia ndumba kwa kwenda Mlingotini, Bagamoyo, kwa nia ya kutaka uongozi na matokeo yake kama watu hao watashinda lengo la kwanza linakuwa kurudisha fedha walizotumia.

Alivipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kufichua maovu ndani ya jamii na kuwataka viongozi wawe wastahimilivu wanapoandikwa maovu yao.Aliwaasa viongozi wenzake kutanguliza uzalendo kwa nchi na kuwataka wachape kazi kwa maslahi ya taifa vinginevyo watarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA