76 Mbaroni Wakihusishwa na Vurugu Zanzibar


Na Mwantanga Ame

JESHI la Polisi limeshusha timu mpya ya wapelelezi kwa ajili ya kuwasaka watu wanaodaiwa kuhusika kuanzisha vurumai iliyodumu kwa siku mbili katika mji wa Zanzibar.

Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi, imekuja baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, (JUMIKI) kuanzisha vurugu ili kutaka kujua hatma ya kiongozi wao aliyekuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi hilo katika kituo cha Mwembe Madema.

Kutokana na hali hiyo tayari Jeshi la Polisi, limeshawakamata watu 76 ambapo kati ya hao 73 wameshafikishwa Mahakamani hadi mchana wa jana na watatu wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kukamilishiwa upelelezi.


Vurugu hizo zilisababisha kuzuka kwa vitendo vya uchomaji wa moto katika makanisa nyumba ya mlinzi kanisa la Welezo, Nyumba ya Mlinzi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Baa ya Mbawala, Mzushi na uporaji wa vitu mbali mbali.

Huku jumuiya ya UAMSHO ikihusishwa kuwa chanzo cha matukio hayo, wakuu wa Jumuiya hiyo wamekanusha matukio na kudai kufanya vitendo vilivyofanywa ni kwenda kinyume na misingi ya dini ya kiislamu ambayo inakataza kufanyika kwa hujuma.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Said Mwema, akizungumza na viongozi wa Makanisa ya Zanzibar na Tanzania bara katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) la Kariakoo, wilaya ya Mjini Unguja, alisema tayari Jeshi la Polisi limeshaongeza wapelelezi kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo.

IGP Mwema, alisema wameamua kuongeza wachunguzi kwa lengo la kubaini wahusika wa matukio ya uchomaji wa makanisa na vurugu nyengine kutokana na kuonekana vitendo hivyo ni venye kushabihiana na mambo muelekeo mwengine.

Alisema walichokibaini katika tukio la mwishoni mwa wiki baadhi ya watu wameamua kutumia mwanya huo kuendeleza vurugu hizo kwa kuanzisha maslahi yao binafsi kwa vile wanaofanya hujuma hizo huondoka na mali katika maeneo wanayoyashambulia.

“Tumeongeza timu ya wapelelezi kutoka Makao Makuu ya upelelezi wapo hapa Zanzibari ili kuweza kubaini wahusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria, tujenge imani watafanya kazi vizuri ila tunaomba muwape msaada”, Alisema IGP Mwema.

Alisema Jeshi hilo la Polisi litahakikisha linawatia mikononi wahalifu wote na litawakamata popote walipo na kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zao.

Alisema katika utekelezaji wa mpango hivi sasa kwa makusudi Jeshi la Polisi limeamua kuyapa ulinzi makanisa yote baada ya kuorodheshwa ikiwa ni hatua ya kudhibiti vitendo hivyo.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, akitoa maelezo ya serikali, alisema imesikitishwa na vitendo vilivyotokea na kuwataka waumini wa kikiristo kutochukua visasi kulipiza vurugu hizo.

Waziri Aboud, alisema katika kulifanyia kazi suala hilo kuanzia sasa serikali inapiga marufuku kufanyika kwa mihadhara ya dini, maandamano ambayo itakuwa haina kibali ha serikali na itakuwa tayari kuwashusha majukwaani wataokadi kutii amri hiyo.

Alisema nia ya serikali ni kuona inajenga uchumi ulioimara kutokana na hivi sasa kumekuwa na matatizo mbali mbali ya kukosema ajira kwa vijana wengi na huduma za kijamii jambo ambalo utatuzi wake utapatikana ikiwa nchi itabakia katika amani.

Alisema haoni sababu ya matukio hayo kuanza kutokea kwa mambo hayo wakati miaka ya nyuma Waislamu na Wakristo wa Zanzibar walikuwa kitu kimoja katika mambo mbali mbali ya shughuli za kijamii.

Aboud, alisema kinachojitokeza sasa kinaonekana kuna jambo lililojifichwa kwenye ncha ya baadhi ya makundi ambayo yanawapa shaka za kisiasa na kidini kwa kutumia watu ambao wanaukali wa maisha.

“Haiwezekani mtu tunasema Sheikh anaeaminika kisha aende kubeba kreti ya bia akimbie nalo serikali itapambana nao naomba nitoe salamu za pole kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein jambo hili linatusikitisha serikali nzima”, alisema Aboud.

Aidha, Waziri Aboud, alivitaka vikundi vya dini kuchagua kazi moja ya kuifanya na sio kuchangaya siasa na dini kwani serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiwaacha kufanya hivyo kwa kutanua demokrasia lakini imeonekana baadhi ya watu hawako tayari kufanya hivyo kwa amani.

Waziri Aboud, alikiri kwa serikali kufanya kosa kuacha kuyafanyia kazi masuala hayo wakati yakianza kujitokeza lakini kuanzia sasa itahakikisha inayadhibiti yasitokee tena.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Abdalla Mwinyi Khamis, akitoa maelezo yake alisema serikali ya Mkoa itahakikisha inarudisha hali ya amani kwani vurugu zilizojitokeza hazikuwa ni wazo wala nia ama msimamo wa Mkoa huo.

Nae Mjumbe kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Nauman Juma Jongo, alisema wameshangazwa na mambo yaliotokea kwani bado yanawapa wasi wasi kama yalishabihiana moja kwa moja na mambo ya dini kwani yalihusisha hadi uvunjaji wa maskani za vyama vya siasa na uchomaji wa bendera.

“Kuna watu wamekunywa bia na kuiba vitu huu sio uislamu, Ofisi ya Mufti inalaani kitendo hicho lazima tukae kuliangalia vyombo vya usalama lifanyieni kazi kwa niaba ya waislamu tunawapa pole jamani”, alisema Sheikh huyo.


Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Jimbo la Zanzibar Dickson P. Kagaga, aliwataka waumini wa kikristo kutulia na wasiwaze kulipa kisasi kwani wanaamini kilichotokea hakitokani na mawazo ya Mzee Abeid Amani Karume.

Hata hivyo, askofu huyo aliiomba serikali kuona inafanya kazi ya ziada kwa kuyapa ulinzi wa kutosha makanisa yao ili vitendo hivyo visiweze kujirejea jambo ambalo litaweza kuwatia hasira waumini wa dini hiyo.

Akisoma taarifa ya jumla ya matukio hayo katibu Mkuu wa Makanisa ya Pentecost Tanzania, Askofu David Andulile, alisema ni vyema kwa viongozi wa serikali kuona wanachukua tahadhari kwa kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake kwa wataobainika kufanya vitendo hivyo ili kuweza kujenga imani kwa waumini wao.

Nae Askofu wa Kanisa la Angikana Zanzibar, Michael Hafidh, akitoa maelezo yake aliiomba serikali kufikiria kuirejesha Kamati ya Amani ili kuweza kushughulikia matatizo ya aina hiyo.

Nae Askofu wa Kanisa la Roman Catholic Zanzibar, Agostino Shayo, alisema kurudishwa kwa kamati ya Amani ni jambo la msingi kwa hivi sasa kwani haiwezekani nchi kukosa kuwa na chombo hicho kwani hapo awali kiliweza kufanya vizuri.

IGP, Mwema bado yupo kisiwani Zanzibar, kulifanyia kazi suala hilo ambapo leo wanatarajiwa kukutana na viongozi wengine wa dini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI