Arusha yazizima, kifo cha kada wa CHADEMA

UMATI mkubwa wa watu jana ulijitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo (38), aliyeuawa kwa kukatwa shingo na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumamosi.

Wingi huo wa watu ulisababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara za jiji la Arusha, ikiwemo barabara kuu ya Moshi- Arusha, huku baadhi ya shughuli zikisimama kwa muda ili kuruhusu watu wengi kumuaga mwanasiasa huyo maarufu.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Thobias Andengeye, waliongoza msafara wa magari yaliyokuwa yameongozana na gari lililobeba mwili wa marehemu Mbwambo kutoka katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru hadi nyumbani kwake marehemu eneo la Magadini, Usa River kisha kanisa la Wasabato Liganga ambako ilifanyika ibada na baadaye kuusindikiza katika Uwanja wa Ngaresero ambako hotuba na heshima za mwisho zilifanyika.

Vilio na maneno ya kuomboleza vilipasua anga la Uwanja wa Ngaresero wakati gari lililobeba jeneza lenye mwili wa marehemu lilipoingia taratibu, huku baadhi ya watu wakianguka na kuzimia.

Viongozi mbalimbali wa CHADEMA na serikali waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, wabunge Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Vicent Nyerere (Musoma Mjini) na Cecilia Paresso (Viti Maalumu).

Nalo jeshi la polisi liliwakilishwa na Naibu Kamishna wa Polisi Isaya Mngulu pamoja na kamanda wa polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye, na mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mercy Silla.

CHADEMA yaishukia polisi
Wakizungumza katika uwanja huo viongozi wote wa CHADEMA waliwataka wananchi kuwa watulivu huku wakilitaka jeshi la polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo ya kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Katibu wa CHADEMA mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, alisema umati mkubwa wa watu uliojitokeza kwenye viwanja hivyo unadhihirisha kuwa kifo cha Mbwambo hakikuwa cha kiholela bali cha kupigania haki; hivyo damu yake iliyomwagika itaendelea kulia kwa ajili ya kudai mabadiliko ndani ya taifa hili.
Alisema kuwa hata kama jeshi la polisi ambalo wanaamini litatimiza wajibu wake, kama halitawakamata waliohusika na mauaji hayo halitarudisha nyuma moyo na ari ya Watanzania katika harakati za kupigania ukombozi.

Lema alisema kuwa hata ikibidi wote kujeruhiwa, bado watazidi kusonga mbele mpaka mabadiliko ya kweli ya maisha ya wananchi yatakapopatikana hivyo kuwataka wananchi wa Arumeru kutohofu kitu.
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Lema, alisema kuwa waliofanya mauaji hayo kama walilenga kuwatisha na kuwaogopesha wananchi kujiunga na harakati za CHADEMA wameshindwa kwani ndiyo kwanza imeongeza vuguvugu la kudai haki.

Alisema kuwa polisi wakiamua kumpata muuaji ni kazi rahisi kwani wauaji walimpigia simu marehemu wakimuita kabla ya kumuua hivyo wanaweza kuwasiliana na kampuni ya simu wakapata taarifa muhimu za kuwatia mkononi wauaji hao.

Lema alisema kuwa marehemu aliwahi kuwaeleza yeye pamoja na Nyerere wakati wa kampeni za ubunge wa Arumeru Mashariki kuwa kuna watu wanamtishia kumuua kutokana na misimamo yake ya kisiasa lakini hawakutilia maanani wakidhani ni vitisho tu lakini anasikitika kuwa wamemuua.
Aliwataka wananchi wasilipe kisasi kwa yeyote kwani kazi ya kisasi ni ya Mungu wao wafunge na kuomba matokeo yataonekana.

Akizungumza kwa niaba ya familia, kaka wa marehemu, John Mbwambo, aliwashukuru wananchi walioungana nao katika msiba huo pamoja na CHADEMA kwa kugharamia msiba huo ambapo alikiomba chama hicho kisaidie kuwasomesha watoto watatu wa marehemu.

Naye mkuu wa wilaya ya Arumeru, Silla, ambaye alifika baada ya kuchelewa aliungana na viongozi wengine kuifariji familia ya marehemu na CHADEMA kwa kuondokewa na baba na kiongozi huku akiwataka wawe watulivu kipindi hiki jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wake.

Polisi watangaza dau
Kamanda Andengenye alisema kuwa Jeshi la Polisi litatoa zawadi nono ya sh milioni 10 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa waliohusika na mauaji hayo huku akiweka wazi kuwa wamekuwa wakifanikiwa katika masuala mengi pale wanapopata ushirikiano toka kwa raia wema.

Marehemu Mbwambo ameacha mjane, Eunice, na watoto watatu, Nazaeli (14), helen (10) na Magreth (6) ambapo anatazamiwa kuzikwa leo kijijini kwao, Mamba wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo mbunge wa Musoma Mjini, Nyerere, alitilia shaka ahadi ya Kamanda Andengenye akidai kuwa katika bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hakuna fungu lililotengwa kwa ajili ya kutoa zawadi kwa wananchi wanaotoa taarifa jambo alilosema kuwa atalifuatilia.

“Mimi ni mkweli sana, mtanisamehe pamoja na ahadi nzuri aliyotoa RPC, mimi sitafuatilia kwake nitapambana na waziri wake kujua kama fedha tunazotenga kwa ajili ya kulinda raia na mali zao zinatumika ipasavyo,” alisema Nyerere.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Nassari, alisema kuwa hafurahishwi na ahadi ya fedha iliyotolewa na jeshi la polisi kwa kile alichosema kuwa anaamini polisi wakiamua kufanya kazi yao wauaji hao wanaweza kupatikana.

Alitolea mfano wa jambazi aliyemuua askari mwishoni mwa mwaka jana na kukamatwa katika kipindi kifupi akitibiwa kwa mganga wa kienyeji, na kusema mazingira ya tukio hilo yalikuwa magumu kuliko hili la kuuawa kwa Mbwambo hivyo akalitaka litumie utaalamu wake kuhakikisha wauaji wanapatikana.

Baraza lalaani mauaji ya wanachama 

Jijini Dar es Salaam, Baraza Kuu la CHADEMA limelaani mauaji ya wanachama wake huku jeshi la polisi likishindwa kuchukua hatua zozote za maana.

“Baraza Kuu limelaani mauaji ya Mwenyekiti wa Kata ya Usa River yaliyotokea Aprili 28 mwaka huu na pia limeeleza kusikitishwa na jeshi la polisi kwa kushindwa kuchukua hatua za maana dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya wanachama wa CHADEMA ambayo yamekuwa yakitokea tangu uchaguzi mdogo wa Igunga,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema baraza hilo limeuagiza uongozi wa chama hicho kuanzisha mchakato wa kulishtaki jeshi la polisi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Aidha pamoja na hayo, alisema baraza hilo limeagiza chama kusukuma hoja ya kuwapo kwa uchunguzi huru dhidi ya matendo ya kidhalimu yanayofanywa na Jeshi la Polisi na kutolea mfano Arusha, Mwanza, Ruvuma Mbeya na Mtwara (Tandahimba).

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA