CCM,CHADEMA WALIZANA

Mbunge wa Jimbo la Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga, akiwapungia wanachama wa CCM, waliokuwepo Mahakama Kuu kusikiliza matokeo ya kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo hilo, Fred Mpendazoe, baada ya Mahakama Kuu, kuuthibitisha uhalali wa ubunge wa Mbunge huyo, Dar es Salaam  jana. Aliyekumbatiana naye ni mkewe.



VYAMA viwili vilivyo mahasimu wakubwa wa kisiasa hapa nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana kila kimoja kilipata pigo baada ya matumaini yao ya kupata ushindi katika kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge kukwama.
Jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni huzuni na simanzi kwa aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CHADEMA, Fred Mpendazoe, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi lake, hivyo kumpa ushindi mgombea wa CCM, Dk. Makongoro Mahanga.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Profesa Ibrahim Juma alisema mlalamikaji alishindwa kuthibitisha moja ya tuhuma nzito za madai kuwa Mahanga alikimbia na sanduku la kura, na kwamba zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani, kwani inamaanisha kuwa Tume ya Uchaguzi hawakuwa makini na kazi yao.
Jaji huyo alisema Mpendazoe alishindwa kuleta mashahidi ambao ni wakuu wa vituo vya polisi kuja kuthibitisha kukamatwa kwa Mahanga na masanduku hayo.
Akisoma hukumu yake yenye kurasa 79, jaji huyo aliitaja hoja ya kwanza iliyohusu madai ya kukiukwa kwa utaratibu wa uchaguzi na matokeo ya baadhi ya vituo kuwa hayakusainiwa na msimamizi wa uchaguzi, alisema malalamiko hayo kama yangekuwepo yangepaswa kupelekwa na wasimamizi wa uchaguzi wa vituo na si kwakwe.
“Mahakama hii imeona hoja hiyo ya mgogoro wa kura haikupaswa kupelekwa mahakamani kwani kwa mujibu wa kifungu cha 79 cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka mlalamikaji apeleke malalamiko hayo kwa msimamizi wa kituo cha uchaguzi ili ayatolee uamuzi na kama akuridhika na uamuzi huo mlalamikaji atalazimika kupeleka lalamiko hilo kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo na kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa hakuna ushahidi unaoonyesha malalamiko hayo yaliwahi kufikishwa na walalamikaji kwa kufuata taratibu hizo na kwa maana hiyo mahakama hiyo inaitupilia mbali hoja hiyo,” alisema Jaji Ibrahim.
Katika hoja ya pili ya kulalamikiwa zoezi zima uchaguzi, jaji huyo alisema kwa kuwa mlalamikaji alishindwa kuleta ushahidi mahususi, hivyo mahakama imetupilia mbali hoja hiyo na imeridhika kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikidhi matakwa yote ya sheria na kanuni.
Hoja ya tatu ilikuwa ni je, kura za vituo 120 vya Kata ya Kiwalani na 129 vya Kata ya Vingunguti ambazo ilidaiwa kuwa hazikujumuishwa katika matokeo ya jumla yaliyompa ushindi Mahanga, mlalamikaji katika hati yake ya madai aliiambia mahakama kuwa angewasilisha mkanda wa video kuthibitisha hoja hiyo, lakini hakufanya hivyo, licha ya kuombwa kufanya hivyo.
“Kutokana na ushahidi wa mashahidi wa Mpendazoe kuhusu hoja hiyo mahakama imeona kuna matokeo ya ngazi ya kata za Kiwalani na Vingunguti fomu zilipotea. Pia inaonekana matokeo hayo hayakutangazwa kwa ngazi ya Jimbo la Segerea. Pili, mahakama imeona majumuisho ya kura ngazi ya kata ni kwa ajili ya kukusanywa tu na ngazi ya jimbo ni kwaajili ya kujumuishwa na kisha kutangazwa.
“Kisheria mahakama hii imejiuliza ni wakati gani majumuisho ya kura hufanyika, katika ngazi gani na wakati gani? Kifungu cha 81 cha Sheria ya Uchaguzi kinampa mamlaka msimamizi wa uchaguzi kumtangaza mshindi na kifungu cha 79(a), 80 na 81 vya sheria hiyo vinatamka bayana kuwa matokeo ya uchaguzi yatajazwa katika fomu Na. 21 B na kwamba matokeo hayo yatapita hatua nne:
“Mosi, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika kupokea matokeo kutoka katika vituo, atavihakiki na msimamizi wa uchaguzi ndiye atakayehakiki matokeo na aidha yeye mwenyewe au msaidizi. Pili, ni pale msimamizi wa uchaguzi anatoa uhalali kama kuna migogoro ya kura halali. Tatu, msimamizi atatangaza matokeo ya uchaguzi kwa sauti. Nne, msimamizi huyo atajaza fomu hiyo ili aweze kumtangaza mshindi kwa sauti. Na utaratibu huu unatumika kwa ngazi ya jimbo.
Aidha, jaji huyo alisema msimamizi wa uchaguzi wa majimbo ya Segerea, Ilala na Ukonga katika ushahidi wake alileta ushahidi wa kuthibitisha hatua hizo zilifuatwa na kwamba majumuisho ya kura yalifanyika kwa ngazi ya jimbo na kutangazwa katika Ukumbi wa Arnautoglu baada ya kuwaalika wagombea na wafuasi wa vyama vyote lakini CHADEMA na Mpendazoe walikataa kuhudhuria na mgombea huyo na wafuasi wake sita walimtaka Fuime asimamishe utangazaji wa matokeo hayo.
Alisema kwa sababu mawakala na mgombea wa CHADEMA waligoma kuingia kwenye chumba cha kuhesabia kura ni wazi kabisa si Mpendazoe wala huyo wakala wake wanaweza kuleta ushahidi ambao ungethibitisha kura za vituo vyote hazikujumuishwa, kwasababu walikiri kuwa hawakuwepo kwenye chumba cha kujumulishia kura za ubunge.
Kuhusu hoja ya tano ambayo Mpendazoe alishindwa kuleta ushahidi ni juu ya madai kuwa Imelda Kafanabo, ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Kata ya Tabata kuwa alikamatwa na polisi pale Arnaotoglu akiwa na matokeo yaliyoghushiwa.
Kuhusu hoja ya sita ya kijana kukamatwa Arnaotoglu akiwa na mhuri wa NEC, jaji huyo alisema hoja hiyo ni dhahifu kwa sababu mlalamikaji hakuleta ushahidi na kama ni kweli, je, mhuri huo uliathiri vipi matokeo ya Jimbo la Segerea?
Kuhusu masanduku kuwa wazi, jaji huyo alisema hata kama yangekuwa wazi yasingeathiri kura zilizokuwa ndani yake na kwamba mlalamikaji ameshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha hayo masanduku yalitoka kata zipi na namba za masanduku hayo.
Kuhusu hoja ya nane, ambayo mlalamikaji alidai mawakala wake, wa CUF na SAU waligoma kusaini fomu za uchaguzi kwa sababu matokeo ya kura za kata za Vingunguti, Buguruni na Kiwalani hayakujumuishwa, jaji alisema mlalamikaji alishindwa kuwaleta wagombea ubunge wa CUF na SAU mahakamani kuja kuthibitisha dai hilo na kuongeza katika ushahidi wa Mwakatobe na Mpendazoe walioutoa mahakamani walikiri kuwa hawakuwepo kwenye chumba cha kuhesabia kura.
Katika hoja ya 10 na 11 ambayo mlalamikaji anadai kushinda kwa kura 56,962 na kufuatiwa na Dk. Mahanga aliyepata kura 44,904, Mpendazoe alipohojiwa na mawakili wa utetezi alidai kuwa alipata idadi hiyo ya kura za ushindi kwa makadirio na kwamba matokeo hayo alipewa na mawakala wake ambao waliandika idadi hizo za kura katika kipande cha karatasi ambacho amekisahau kwenye gari lake.
“Kanuni ya 13(1) inayoongoza kesi za uchaguzi zinamtaka mgombea kuwasilisha dai la aina hiyo dhidi ya aliyeshinda ndani ya siku sita kabla ya kupangwa kwa tarehe ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa na atapaswa apeleke orodha ya matokeo hayo anayodai kushinda kwa Msajili wa Mahakama Kuu ambayo anakusudia kuyatumia katika kesi yake, jambo ambalo Mpendazoe hakulifanya.
“Kwa sababu zote za kisheria nilizozitaja hapo juu mahakama hii inatupilia mbali madai 11 ya Mpendazoe yaliyotaka nibatilishe ubunge wa Mahanga kwa sababu ameshindwa kuleta ushahidi ambao ungeutisha ushahidi wa upande wa wadaiwa. Kwa maana hiyo mahakama hii inasema Dk. Mahanga ndiye mbunge wa Jimbo la Segerea kwa sababu hakuna sheria yoyote iliyokiukwa wakati wa zoezi la uchaguzi wa jimbo hilo,” alisema Jaji Juma.
Dk. Siame CCM asalimu amri
Katika Mahakama Kuu ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Mbunge wa Jimbo la Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA), ilimtangaza kuwa mbunge halali wa jimbo hilo, baada ya kufuta shauri la kesi ya rufaa iliyopelekwa na aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Lucas Siame.
Siame aliyekuwa amekata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Julai mosi, mwaka jana dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliompa ushindi mbunge huyo wa CHADEMA, alilazimika kuomba Mahakama Kuu kuondoa shauri hilo.
Mbele ya majaji watatu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo chini ya Mwenyekiti wao, Jaji Januari Msofe, ambao ni Jaji William Mandia na Jaji Mbarouk S. Mbarouk, wakili wa mlalamikaji Victor Mkumbe, aliwasilisha ombi la kutaka kuondoa shauri hilo mahakamani hapo jana.
Akiwasilisha ombi hilo, Wakili Mkumbe alisema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya mlalamikaji kuonesha nia ya kutotaka kuendelea na kesi hiyo huku akitumia kanuni ya 102, kifungu cha kwanza cha kanuni za Mahakama ya Rufaa.
Hata hivyo Jaji Msofe alikikataa kifungu hicho akisema kuwa kina upungufu mwingi, hivyo kisingeweza kutumika katika ombi hilo badala yake akatumia kanuni ya 4(2)(a) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa.
Katika kesi hiyo serikali iliwakilishwa na mawakili wawili; Mwanasheria Mkuu Mwandamizi, Obadia Kamea na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Rosemary Shio, ambao waliridhia kuondolewa kwa rufani hiyo baada ya kuhojiwa na Jaji Msofe.
Jaji Msofe alimhoji wakili wa mlalamikiwa Benjamin Mwakagamba kama angekuwa na la kusema baada ya kusikia ombi la mlalamikaji, ambapo alikubaliana na ombi hilo lakini akiitaka mahakama kumwamuru mlalamikaji kumlipa gharama alizotumia.
“Waheshimiwa majaji tumetumia gharama zetu katika kuendesha kesi hii lakini pia leo tulikuwa tumejiandaa kwa ajili ya kusikiliza, kwa kuwa mlalamikaji kaamua kuondoa kesi mwenyewe, tunaomba kulipwa gharama zetu tulizotumia,” alisema Mwakagamba.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Mandia alisema kuwa Mahakama ya Rufaa imekubali ombi hilo na hivyo shauri hilo limeondolewa.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 4(2)(a) Mahakama inaliondoa shauri hili kutokana na pande zote kuridhia na inamwamuru mlalamikaji kulipa gharama zote alizotumia mlalamikiwa,” alisema Jaji Mandia.
Akizungumza na Tanzania Daima nje ya mahakama hiyo, Silinde alisema kuwa anaipongeza Mahakama ya Rufaa kwa kufikia uamuzi huo na kutenda haki kwa kuwa katika kesi ya awali alimshinda mlalamikaji na aliamini kuwa angemshinda pia.
“Niseme tu kwamba mpinzani wangu ameshituka na kujua kuwa nitamshinda na gharama za kunilipa zitaongezeka ndiyo maana amechukua maamuzi ya kuondoa kesi hii, amefanya jambo la busara sana nampongeza,” alisema Silinde.
Kwa upande wake wakili Mwakagamba aliyekuwa anamtetea Silinde alisema kuwa wataandaa utaratibu wa kuweza kudai fidia ya gharama walizozitumia.
Mwenyekiti wa Jimbo la Mbozi Magharibi (CHADEMA), Joseph Mwachembe, maarufu kama ‘China’ aliwashukuru watu waliojitokeza kusikiliza kesi hiyo na kusema sasa ni utekelezaji wa ahadi alizozitoa mbunge huyo kwa wananchi wake wakati wa kampeni.Chanzo;Tanzania Daima

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.