Diwani CCM atishia kumuua mbunge



• Polisi wamdaka na watoto wake

na Mwandishi wetu, Iringa
SIKU moja baada ya kundi la vijana wanaoaminika kuwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwacharanga mapanga wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, sasa ametishiwa kuuawa.

Habari zinasema kuwa Diwani wa Kata ya Nduli, Idd Rashid Chonanga, jana asubuhi alimvamia Mchungaji Msigwa ofisini kwake na kumtaka ajue kuwa siku zake zinahesabika, hata kama juzi alinusurika, lakini atahakikisha ameuawa kwa njia zozote zile, hali iliyomfanya mbunge huyo kukimbilia polisi kuomba msaada.

Diwani huyo, ndiye anayetuhumiwa kusimamia kikamilifu tukio la kucharangwa mapanga kwa wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati wa mkutano wa mbunge huyo uliofanyika katika uwanja wa kata ya Nduli na kuwajeruhi vibaya.

Katika mkutano huo ambao ulifanywa na mbunge huyo, mwenyekiti, katibu, wajumbe sita wa CCM wa kata ya Nduli na wanachama wengine takriban 90 walihamia CHADEMA, huku ikidaiwa kuwa wengine zaidi ya 150 wangelikihama chama tawala wiki hii.

Akizungumza akiwa polisi, Mchungaji Msigwa alisema kuwa kauli ya diwani huyo imemtisha kwa kuwa anajua ina baraka za viongozi wake wa ngazi ya juu.

Mchungaji Msigwa alilitaka Jeshi la Polisi lisifanye mzaha katika jambo hilo, kwa kile alichodai kuwa ni jambo la hatari na lenye lengo mahsusi la kuwatisha viongozi wa vyama vya upinzani na wananchi baada ya kuona kuwa CCM inazidi kupoteza maelfu ya wanachama wake kila kukicha.

Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, alisema hadi muda huo alikuwa hajapokea taarifa hizo, lakini akaahidi kulishughulikia jambo hilo kikamilifu, ili kulinda amani na usalama wa kiongozi huyo na raia wengine.

Hata hivyo, Tanzania Daima imethibitishiwa kukamatwa kwa diwani huyo na vijana wa CCM waliohusika kuwakata mapanga watu watatu waliokuwa katika mkutano wa mbunge huyo juzi.

Mmoja wa maafisa wa polisi alidai kuwa miongoni mwa vijana waliokamatwa, wawili ni watoto wa diwani huyo na kwamba watu wengine wanne, akiwemo mfanyakazi wa diwani huyo, bado wanasakwa na jeshi hilo kwa kuhusina na tukio la juzi.

Akizungumzia kutishwa kwa maisha kwa mbunge Msigwa, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM kata ya Nduli, Ayub Mwenda, alisema tangu jana amekuwa akipokea vitisho na kudai kuwa hali hiyo haitakisadia chama tawala, badala yake kinasababisha kichukiwe na hata na wale waliokuwa wakikipenda.

“Wananchi wengi wamechukizwa sana na tukio la juzi, na wakisikia tena na hili alilofanya huyu diwani leo, ndio itakuwa imezidi kujipalia mkaa. Hii ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi, na kila mtu anayo haki ya kujiunga na chama chochote, sasa inashangaza kuona inakuwa nongwa kwao,” alisema Mwenda alipohojiwa na gazeti hili.

Wakati huohuo, mmoja wa watu waliojeruhiwa vibaya katika shambulizi la mapanga juzi, Osca Sanga bado amelazwa katika hospitali ya mkoa, wakati wengine wawili waliruhusiwa jana.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, George Kabona, amesema Sanga anaendelea na matibabu, ingawa alikiri kuwa hali yake bado haijawa ya kuridhisha.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI