EDWARD LOWASSA AMWAGA MILIONI 10 HARAMBEE YA KKKT 


 Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (kulia), akimkabidhi, Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji George Fute, sh. milioni 10, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha la Wezesha Upendo Fm Redio, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kuboresha na kuongeza usikivu wa redio hiyo lililofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam jana. Fedha hizo zilitolewa na Lowassa na marafiki zake. Zilikusanywa sh. milioni 125 katika harambee ya jana. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)
 
 Na Dotto Mwaibale
 

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM) amechangisha jumla ya sh. milioni 125 katika harambee ya kuchangia na kuiwezesha studio za Redio Upendo kununua vifaa vya kuiboresha.
Harambee hiyo ilifanyika Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Diamond Jubilee na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mawasiliano, wachungaji kutoka makanisa mbalimbali, wanasiasa na waimbaji wa vikundi tofauti kwa lengo la kutoa burudani.
Kabla ya kuanza kuchangisha, Lowassa alitoa mchango wake wa sh. milioni 10 na kusema kuwa mchango huo ametoa yeye na wenzake.
Alisema ameguswa kuchangia uendelezaji wa kituo hicho cha redio kwa kuwa huduma inayotolewa ni muhimu katika maisha ya kawaida ya binadamu kimwili na kiroho.
Lowassa alisema kuwa upo mpango mkakati wa kuanzisha televisheni itakayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambalo ndilo linalomiliki Redio Upendo na kuongeza kuwa uwezo wa kuanzisha kituo hicho upo na utaanzishwa pamoja na gazeti jipya.
Alisema kinachosubiriwa ni mchakato wa uanzishwaji wa kituo hicho kwani penye nia pana njia na utekelezaji wa mpango huo unaendelea.
Jumla ya fedha zilizopatikana katika mchakato wa uchangiaji wa Wezesha Upendo Redio Fm ni sh. milioni 125, kwani sh. milioni 80 zilitokana na uchangiaji wa kadi na sh. milioni 45 zilizopatikana kwa watu kuchangia ukumbini.
Mkurugenzi wa Redio Upendo katika kutoa salamu zake kwa watu waliojitokeza kwenye tamasha hilo, Agatha Lema alisema kuwa wananchi wanaunga mkono jitihada za kituo hicho katika kukiboresha na kuwaomba waendelee kutoa ushauri na kukiombea ili kizidi kuwahudumia.
Naye Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), George Fupe aliwasisitiza wananchi kuendeleza amani na upendo kama ilivyo jina la kituo hicho kwani ndiyo kiungo cha jamii.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Theolojia, Misheni na Uinjilisti, Chegei Sendoro aliwataka Watanzania kuombea visiwa vya Zanzibar viwe na amani kutokana na vurugu zilizojitokeza juzi na jana vya waandamanaji wa Jumuia ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) kufanya maandamano na kuchoma kanisa moja la Anglikana.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI