JAJI WARIOBA ATAKA WAIACHE TUME IFANYE KAZI

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue (kulia), akimkabidhi funguo za ofisi ya Tume ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam jana. Katikati ni Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani.

MWENYEKITI wa Tume ya mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewacharukia watu wanaoanza kuisakama tume yake na wenye mipango ya kutaka kuingilia utendaji kazi wa tume yake, wakae pembeni na kuwaacha huru.
Jaji Warioba alitoa onyo hilo jana wakati wakikabidhiwa rasmi jengo jipya la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, mkabala na Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, litakalotumiwa kwa kazi ya tume hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema taasisi zilizowapendekeza wajumbe waliofanikiwa kuteuliwa katika tume yake zisijaribu kuingilia kazi zao, wala kuwapa shinikizo wajumbe wake ili kulazimisha watende wanayotaka.
“Ninaomba kwa dhati kabisa wale waliopendekezwa watuache tufanye kazi. Tumepewa kazi na nchi, watuache tufanye bila presha yoyote. Na wale wanaosema tuna mtu wetu kule, hawana mtu wao, bali Watanzania wana watu wao hapa,” alisema Warioba.
Warioba alisema kwa kuwa jukumu la tume yake ni zito na nyeti, watajitahidi kufanya kazi kwa uwezo wao wote ili watekeleze yale waliyokabidhiwa na rais kwa niaba ya Watanzania wote.
Alisema watapanga ratiba kamilifu kuhakikisha wanakuwa na utaratibu utakaowawezesha kuwafikia wananchi wengi.
Alisema watatoa nafasi ya kutosha kwa kila mwananchi, wakitambua kuwa wana hoja zao kuhusu uzuri na upungufu wa katiba ya sasa, na wataomba mapendekezo ili iandikwe katiba itakayokidhi matakwa ya taifa.
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisema kuwa ushirikishaji wa wananchi katika ujenzi wa katiba ni jambo muhimu na la lazima katika kupata katiba inayokubalika na walio wengi.
“Wanazuoni wanatufundisha kuwa mamlaka ya taifa lolote yapo mikononi mwa wananchi wa taifa hilo na inapohitajika kujenga katiba basi ni lazima wananchi hao washirikishwe katika mchakato mzima kwa kutoa maoni na hatimaye kuihalalisha katiba ya taifa lao,” alisema.
Alisema kufanikiwa kwa mchakato huo kutategemea zaidi uelewa wa wananchi wa katiba yetu ya sasa ya mwaka 1977, kwani ni ukweli usiopingika kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu katiba ya nchi yao.
Alikiri kuwa kiwango kidogo cha uchapishaji na ukosefu wa utamaduni wa kusoma miongoni mwa wananchi ndiyo sababu ya uelewa mdogo wa wananchi kuhusu katiba.
Alisema serikali imewapatia mahali pazuri pa kufanyia kazi na vifaa vipya vya ofisi, pia inakamilisha ununuzi wa magari mapya kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.
Kombani alisema, serikali itaendelea kutenga fedha za kutosha katika bajeti ili tume iendeshe mchakato huo kwa ufanisi na uharaka kwa kadiri itakavyokuwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete amemwagiza wafanye kila liwezekanalo kuiwezesha tume ifanye kazi yake katika mazingira stahiki, kwa uhuru, utulivu, salama na amani.
Alisema katika kufanya maandalizi hayo serikali ilizingatia uhuru na utulivu wa kufanya kazi, ulinzi na usalama, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, mawasiliano, bajeti ya tume na usafiri wa wajumbe.
Pia vitendea kazi muhimu, umeme, watumishi na nyumba kwa wajumbe wote walio nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambazo zitakuwa na samani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI