KILICHOWAPONZA MAWAZIRI 6 WALIOACHWA

Rais Jakaya Kikwete jana alisuka upya baraza lake la mawaziri kwa kuwatosa mawaziri sita kati ya mawaziri wanane waliokuwa wametajwa kwa kashfa mbalimbali katika ripoti ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG). Mawaziri hao ambao sasa wameondolewa kwenye baraza hilo ni pamoja na Ezekiel Maige wa Mali Asilia na Utalii, William Ngeleja wa Nishati na Madini, Omar Nundu wa Uchukuzi, Cyril Chami wa Viwanda na Biashara, Hadji Mponda wa Afya na Ustawi wa Jamii na Mustafa Mkulo wa Fedha.
Mawaziri walionusurika katika sakata hilo ni wawili ambao ni George Mkuchika na Jumanne Maghembe ambao hata hivyo wamehamishwa kwenye wizara zao za awali; Tamisemi na Kilimo. Zifuatazo ni baadhi ya tuhuma zilizokuwa zimeibuliwa na CAG kwenye wizara za mawaziri hao waliositishiwa utumishi jana.

Mustafa Mkulo Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ndiye aliyekuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu. Mkulo alituhumiwa kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwamo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL).

Ukaguzi wa CAG ulibaini kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa kiwanja hicho Na.10 kilichopo kando ya barabara ya Nyerere bila kuishirikisha bodi ya CHC. Vile vile, CAG alibaini kuwapo kwa sintofahamu katika hati ya madai ya Sh2.4 bilioni kutoka katika kampuni ya DRTC kama gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya kuingilia kwenye Kiwanja Na.192 kando ya barabara ya Nyerere.

Upungufu pia ulionekana kwenye uuzwaji wa jengo la Kampuni ya Tanzania Motors (TMC) lililopo kiwanja Na.24 kilichopo katika eneo la viwanda la Chang’ombe kwa kampuni ya Maungu Seed. Ngeleja Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alikabiliwa na kashfa baada ya CAG kubaini kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa mwaka mmoja wa fedha linafanya manunuzi yenye thamani ya Sh300 bilioni hadi Sh600 bilioni. Kwa mwaka wa fedha 2009/10, Tanesco ilitumia Sh1.8 bilioni ukilinganisha na Sh65 milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati mojawapo katika kituo cha bwawa la Mtera na kuingia mikataba isiyo na tija kwa taifa.

Ezekiel Maige Waziri huyu wa Maliasili na Utalii ripoti ya CAG ilieleza kuwa ofisi yake ilipoteza Sh874,853,564 baada ya kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa kiwango cha chini cha mrahaba kwa mauzo ya misitu. Katika kipindi cha ukaguzi wa hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa) ilibainika kuwa Shirika liliingia katika mkataba na kampuni ya CATS Tanzania LTD unaohusiana na matengenezo ya kawaida, ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine katika mkataba wa jumla ya dola milioni moja za Marekani.

Alishutumiwa kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, ugawaji ambao inadaiwa ulitawaliwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza majina ya waliopata vitalu bila kuonyesha ni vitalu vipi walivyopewa. Pia, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilieleza kuwa kampuni 16 zilipewa vitalu hivyo hazikuomba na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la kwanza na la pili.

Mbali na tuhuma hizo, Maige hivi karibuni alidaiwa kununua nyumba kwa Dola za Marekani 700,000 iliyopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa nyumba hiyo ameinunua kwa Dola 410,000, sawa na zaidi ya (Sh600 milioni).

Dk Haji Mponda Kilichomkabili Waziri Mponda ni kashfa ya Bohari ya dawa (MSD) ambapo ukaguzi maalum wa MSD uliofanyika ulibaini kuwapo tofauti ya Sh658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokelewa na kuripotiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda MSD, ambapo ushahidi wa kupokelewa haukutolewa. Pia kulikuwa na kiasi cha Sh100 milioni kilichopelekwa na MSD kutoka Wizara ya Afya na kikatumiwa na MSD bila kuwapo na mchanganuo wa matumizi.

Ukaguzi maalum ulibaini pia kuwapo kiasi cha Sh4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh4.344 bilioni tu ndicho kilichopokelewa na MSD ikiacha Sh196 milioni bila kuwapo na ushahidi wa kupokelewa na MSD kutoka Wizara ya Afya. Ilibainika pia kuwa, baadhi ya vifaa vinavyotolewa na MSD vimekuwa havina viwango vinavyostahili kwa mfano vifaa vya kupima shinikizo la damu na machela za kubebea wagonjwa zilizotolewa kwa mganga mmoja wa wilaya (DMO), viliharibika kabla ya muda uliokusudiwa.

Mwaka 2009/10 Wizara ya Afya ilitumia fedha za matumizi ya jumla ya Sh1.10 bilioni kwa ajili maonyesho ya Nane nane, fedha ambazo hazikuwamo kwenye bajeti iliyopitishwa na bunge. Omari Nundu Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu anakabiliwa na kashfa ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.

CAG katika ukaguzi wake alibaini Shirika la Ndege Tanzania limekuwa likijiendesha bila Bodi ya Wakurugenzi kwa muda mrefu jambo ambalo limesababisha kudorora kwa shughuli za shirika hilo. Sakata jingine ni la mkataba kati ya ATCL na Shirika la Ndege la Afrika Kusini uliovunjika kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji.

Baada ya kuvunjika kwa mkataba huo Septemba 2006, ATCL ilisaini mkataba mwingine wa makubaliano na Kampuni ya China Sonangol International Holdings Limited. Kampuni hii ilileta ndege mbili chakavu ambazo zilikuwa zikitumiwa na shirika jingine kinyume na makubaliano. Sakata jingine ni usimamizi mbaya wa mkataba wa ujenzi katika mamlaka ya bandari Tanzania (TPA).

TPA iliingia katika mkataba na kampuni ya AF MULT-Con LTD kujenga nyumba ya makazi ya msimamizi mkuu wa Bandari ya Tanga kwa gharama ya Sh500 milioni. Hivi karibuni katika utetezi wake Waziri Nundu alisema naibu wake, (Athuman Mfutakamba) amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa kwenda nje.

Waziri Nundu pia alishangazwa na shinikizo la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake, Peter Serukamba kuingia na kushinikiza CCCC ipewe kazi hiyo huku akihoji kuna nini? Hata hivyo, naibu wake, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu safari zake hizo za nje kugharamiwa na CCCC na baadaye kuandika ripoti akishinikiza ipewe kazi ya kujenga gati hizo, alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo, lakini akasema alifuata taratibu zote za kiserikali.

Chami Kilichomuondoa Chami ni kashfa iliyoigubika wizara hiyo kwa kwa kudaiwa kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege anadaiwa kusimamia ofisi hewa za ukaguzi wa magari mjini Singapore na Hongkong na kuitia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa upande wake Dk Chami alisema hadi Bunge linamalizika mjini Dodoma hivi karibuni, alikuwa hajaiona ripoti ya kamati ndogo ya Bunge iliyomchunguza Ekelege ambayo ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili mkurugenzi huyo ili kuchukua hatua.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*