Ndugu zangu,

Wakati mwingine kuna tunaojisahau,  kuwa umri wetu umetusadia, sio tu kusoma habari za bara letu hili la Afrika na kwingineko, bali, tukiwa shule za msingi tumepata kusikia na hata kusoma  habari  zilizoshtusha na kubaki katika historia. Ndio , tumeshuhudia vioja pia.

Na mara nyingi Afrika husikika  habari zenye kuhusiana na  hazina na kilichomo kwenye hazina.Na hiyo  ndio Afrika yetu; ” Ex Africa simper aliquid novi”. Maana yake: “Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika.  Alipata kutamka  Ptolemy, mwanafalsafa wa Kiyunani. 

Ndio, swali kubwa Afrika ni namna gani ya kufaidika na kilichomo kwenye hazina na si namna gani ya kuongeza kilichomo kwenye hazina. Afrika mtu au kikundi cha watu wanaweza kufanya lolote lile ilimradi walifikie sanduku la hazina.  Na mara nyingi mipango ya watu hao huishia hapo, huwa hawana mipango mingine kwa nchi iliyo mbele ya sanduku la hazina.

Naam, Afrika walio walio chini kabisa hawatakiwi  kujua kilichomo kwenye hazina bila hizini !
Na kuna viongozi Afrika wanapenda yote; madaraka na pesa.

Kuna kisa cha Rais aliyekatwa masikio katika kugombania na wenzake akina Prince Johnsson na Charles Taylor juu ya kilichomo kwenye hazina; ni Sajenti Samuel Doe wa Liberia.

Alfajiri ya  Aprili 12, 1980,  kikundi kidogo cha wanajeshi 17 kilijipenyeza ndani ya makazi ya Rais jijini Monrovia. Ikulu walimkuta Rais  William Tolberts bado amelala. Wakamwua. Aliyeongoza kikundi hicho alikuwa askari kijana na wa cheo cha chini; Sajenti Samuel Doe.

Na inasemwa, kuwa Doe alipoingia Ikulu na wenzake alidhani watakwenda kumlalamikia Rais juu ya mishahara midogo ya askari wa vyeo vya chini. Lakini, jinsi walivyoikuta Ikulu ikiwa nyepesi vile, ndivyo mipango ilipobadilika na kuamua kumwua Rais mwenyewe na kuchukua madaraka.

Naam, Samuel Doe alikuwa askari ambaye hata madarasa manne ya shule ya msingi hakuyamaliza. Alitoka kabila dogo la waishio misituni. Kabila la krahn. Ni  watu wa kabila kama lake, masikini na  ambao ndio waliotoka vijijini na kukimbilia jijini Monrovia kutafuta vibarua na pesa. Kwa wenye bahati,  kama Samuel Doe, walionekana mitaani na kuitwa kujiunga na Jeshi.

Vinginevyo, wengi wa vijana hawa hawakuwa na cha kufanya mijini. Hawakuwa na kazi. Na idadi yao iliongezeka. Na si Monrovia tu, ni katika miji mingine ya Afrika. Hali hiyo imeendelea hata leo hii. Na sasa hali ni mbaya zaidi.

Tangu siku ya kwanza, Afrika  kijana anayeingia mjini na kuishi bila kazi hugeuka kuwa  bayaye. Ndivyo walivyokuwa wakijulikana katika nchi ya Uganda. Na miji mingi ya Afrika ya sasa imefurika ma-bayaye. Ni jeshi la wasio na kazi- ni bomu linalosubiri wakati kulipuka.

Sajenti Samuel Doe naye alikuwa bayaye, ni kama ilivyokuwa kwa Idi Amin wa Uganda. Na kama ilivyokuwa kwa Idi Amin, Urais ulimdondokea tu Samuel Doe- kama vile mtu aliyeshinda bahati nasibu.

Ujio wa Samuel Doe uliwafaya WaLiberia waamini kuwepo kwa mabadiliko. Kuondokana na utawala wa kifisadi na kirasimu wa William Tolberts.

Samuel Doe akajitangaza kuwa Rais. Haraka sana akawatwanga risasi mawaziri wote wa Tollberts. Ni kwenye pwani ya bahari huku wananchi wakitazama kama mechi ya mpira.

Sajenti Samuel Doe akatawala kwa kipindi cha miaka kumi. Nchi ikawa kama imesimama. Nini kilimtokea Doe?  Ndugu msomaji, ngoja nifanye mengine, kisa hiki nitaendelea nacho kesho….

Maggid Mjengwa.
Iringa.
0788 111 765

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*